Pages

Monday, June 4, 2012

Katalay aleta mastraika, Kocha Mfaransa Yanga




Kocha Mankour Boualem anayetalajiwa kuja Yanga

 




STRAIKA wa zamani wa Yanga, Patrick Katalay, amefanya mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo ya Jangwani na kuahidi kuwaletea mastraika wawili matata na beki mmoja wa kati.

Tena Yanga wasiwe na wasiwasi kwani wachezaji hao watatu watafika Juni 16 na tayari Mwanaspoti limepata majina yote.

Si hao tu, Katalay ambaye kwa sasa yupo Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, ameithibitishia Mwanaspoti kuwa Kocha Mfaransa aliyezaliwa Algeria, Mankour Boualem, amemwambia yupo tayari kuifundisha Yanga muda wowote atakaohitajika na kwamba viongozi wamemwambia atulie kwanza mpaka hali iwe shwari Jangwani.

Mankour Boualem ndiye aliyeiongoza FC Lupopo mwaka 2010 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na straika wa Simba, Felix Sunzu na kuifunga Yanga jijini Dar es Salaam na hata katika mechi ya marudiano mjini Lubumbashi.

Katalay aliiambia Mwanaspoti jana Ijumaa kwa simu kutoka Kinshasa akisema: "Nimezungumza na Yanga tukakubaliana kwamba nitawaletea mastraika wawili ambao ni Bebe Sangwa (FC Lupopo) na Eziane (Motema Pembe). Pia kuna beki wa kati Eliche kutoka Lupopo.

"Wachezaji hao ni wazuri na ambao wakicheza Yanga wataisaidia kwa vile wanajua wanachokifanya, wakija hapo Dar es Salaam ndiyo mtaona mambo yao.
"Nakuja nao Juni 16 kwa kuwa viongozi wa Yanga wameniambia kwamba nitulie kwanza hali ikae sawa klabuni.

"Kuhusu kocha ni Mfaransa, Mankour Boualem yule ambaye tulikuwa naye Lupopo mwaka 2010 wakati tulipoifunga Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, ni kocha mzuri kwa sasa yupo kwao.

"Aliondoka Lupopo kwa vile alikuwa halipwi vizuri, lakini nimezungumza naye amesema atakuja Yanga muda wowote wakimuita na anapenda kuweka ujuzi wake hapo Yanga.

"Anasema kuna watu wenye fedha na wanaopenda mpira ambao watamrahisishia mazingira ya kufanya vizuri na Yanga."

Aliongeza: "Niliwaambia viongozi wakamkubali na wakaniambia wakiwa tayari watamuita aje Tanzania kuifundisha Yanga, anafundisha soka fulani ya kushambulia, watampenda sana kama wakimpa mkataba."

Kocha huyo aliondoka Lupopo baada ya klabu hiyo kuyumba kiuchumi na kushindwa kumlipa mshahara uliokuwa wa dola 2,500 (Sh 3.5 milioni) kwa mwezi.

Yanga haina kocha kwa sasa baada ya kuondoka kwa Mserbia, Kosta Papic na tayari viongozi wa sekretarieti wamethibitisha kwamba mchakato wa kujaza nafasi hiyo unaendelea.

No comments:

Post a Comment