Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Uganda cha Forum for democratic
change –FDC-kanali Kiiza Besigye, amekamatwa na polisi mjini Kampala kwa
kile polisi wanasema ni kushawishi wananchi kujiunga katika maandamano
haramu.
Amekamatwa katika barabara za mjini Kampala akiwa anatembea kwa miguu huku akifuatiwa na umati wa watu.Hata hivyo polisi iliwazidi nguvu na kumuingiza katika gari lao na kumpeleka kituo cha polisi.
Baadaye naibu msemaji wa polisi Vicent Ssekatte aliwaambia wandishi habari kuwa Besigye amekamatwa kutokana na hatua ya kuchochea wananchi kufanya fujo.
Hatua hii imekuja baada ya Besigye na viongozi wengine wa upande wa upinzani chini ya vuguvugu la 4GC (For God and My country) kutangaza mwishoni mwa juma kuanzisha walichoita mchakato wa matembezi ya uhuru- Walk to freedom kupinga walichoita ufisadi, utawala mbaya na mengine. Ilikuwa imepangwa kuanza Jumatatu.
Lakini polisi walikuwa wamepiga marufuku maandamano na mikutano yote ya hadhara hadi Oktoba 10 baada ya sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya uhuru.
Wengine waliokamatwa ni Meya wa jiji la Kampala Elias Lukwago ambaye alizuiliwa nyumbani kwake.Lukwago ni mwanachama wa chama cha upinzani cha Democratic Party DP.
No comments:
Post a Comment