Mwandishi wa habari mchunguzi wa
Ugiriki amekamatwa kwa kuchapisha majina 2000 ya Wagiriki wanaosemekana
kuwa na akaunti za benki Uswiswi.
Shaka ilikuwa watu hao waliweka fedha zao ng'ambo ili kukwepa kodi.
Lakini serikali ya Ugiriki haikuchunguza watu hao kwenye orodha.
Orodha hiyo inaitwa orodha ya "Lagarde: jarida lenye majina 2000 ya Wagiriki wenye akaunti katika benki ya HSBC mjini Geneva.
Lakini mawaziri wawili wa fedha wa Ugiriki wanashutumiwa kuwa waliificha orodha hiyo, na kuzusha tetesi kwamba serikali imeshindwa kuchunguza kesi ambazo zinaweza kuwa za rushwa kubwa.
Sasa mwandishi wa habari maarufu wa Ugiriki, Kostas Vaxevanis, amekamatwa baada ya kuchapisha orodha hiyo.
Anatarajiwa kufikishwa mahakamani hapo kesho, kukabili mashtaka ya kufichua kitu cha faragha.
Mwandishi huyo anasema "badala ya kuwakamata wanaohepa kodi na mawaziri ambao walikuwa nayo orodha, wanajaribu kukamata ukweli na uhuru wa vyombo vya habari."
Kati ya majina hayo kuna wanasiasa, wafanya biashara na wengineo, na imesababisha hamasa kati ya wananchi wa kawaida wa Ugiriki ambao wamezongwa na matatizo ya kiuchumi.
Na swala hilo piya limezusha tena malalamiko kuwa kuhepa kodi nchini Ugiriki ni jambo lilozagaa, na kwamba wakuu bado hawakushughulikia swala hilo vilivyo.
No comments:
Post a Comment