Pages

Tuesday, February 12, 2013

Mjadala wa kwanza kwa wagombea wa Urais Kenya



Mjadala wa kwanza kati ya wagombea wa urais kuwahi kufanyika Kenya ulifanyika Jumatatu usiku kati ya wagombea 8 wanaowania wadhifa huo.
Ingawa wagombea wote walishiriki kwenye mjadala huo, kura ya maoni inaonyesha kuwa kinyang'anyiro kitakuwa kikali kati ya Naibu waziri mkuu Uhuru Kenyatta na waziri mkuu Raila Odinga.
Akihutubia wakati wa mjadala huo Bwana Kenyatta, alisema kuwa ukabila umekuwa donda sugu ambalo limekumba nchi nzima kwa muda mrefu.
Zaidi ya watu elfu moja waliuawa wakati wa ghasia za kikabila baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007 uliokumbwa na utata.
Kenyatta anakabiliwa na kesi ya uhalifu wa kivita katika mahakama ya uhalifu wa kivita ICC, baada ya kuhusishwa na ghasia hizo. Mgombea mwenza wake William Ruto pia anatakiwa na mahakama hiyo kwa kuhusika na ghasia hizo.
Wakenya walikusanyika kwenye vituo mbali mbali kushuhudia mjadala huo. Hoja kuu kwenye mjadala huo ilikuwa swala la ICC ambalo wagombea wengine walitaka Uhuru kuelezea atakavyoongoza nchi ikiwa atapatikana na hatia kwa makosa anayokabiliwa nayo.
Kenyatta alisema kuwa haoni kama kesi yake katika mahakama ya ICC haitaathiri kwa vyovyote atakavyoongoza nchi ikiwa atashinda uchaguzi huo.
Lakini mpinzani wake mkuu Raila Odinga, alipuuza hilo akisema kuwa Uhuru atakuwa na wakati mgumu kuongoza nchi kupitia kwa mtandao wa kijamii wa Skype wakati kesi yake ikisikilizwa Hague.
Wagombea wote walizungumzia swala la ukabila wakisema ni moja ya changamoto kubwa katika uongozi wa nchi kwani tatizo hilo limekita mizizi.

No comments:

Post a Comment