Misri inajiandaa kwa maandamano
ya mahasimu wa kisiasa kuhusu Rais Mohammed Morsi , huku maafisa wa
usalama nao wakijikita mijini kudhibiti hali ya usalama.
Taifa hilo linakumbwa na migawanyiko ya kisiasa na maandamano hayanishi huku pande pinzani zikitaka kuonyesha ubabe wao.Wakati huohuo, mtu mmoja aliuawa na wengine kujeruhiwa katika makabiliano Kaskazini Misri Alhamisi jioni.
Bwana Morsi kwenye hotuba yake aliyoifanya mwaka mmoja tangu kuwa mamlakani, alisema kuwa maandamano yanatishia uthabiti na demokrasia ya Misri.
Majeshi yameamrishwa kushika doria mjini Cairo na katika miji mingine.
Bwana Morsi, ambaye ni mwanachama wa chama cha kiisilamu cha Muslim Brotherhood, ni rais wa kwanza wa chama cha kiisilamu kuwahi kuchaguliwa Misri.
Mwaka wake wa kwanza mamlakani umekumbwa na ghasia na vurugu pamoja na maandamano ya kila mara huku uchumi nao ukiendelea kudorora.
Baadaye leo maelfu ya wafuasi wa Morsi wanatarajiwa kufanya maandamano makubwa kumuunga mkono huku wakipinga matakwa ya upinzani kumtaka ajiuzulu.
Baadhi ya makundi ya upinzani pia yanajiandaa kufanya maandamano baadaye mjini Cairo.
Muungano rasmi wa upinzani, mnamo Alhamisi ulikataa wito wa rais kufanya mazungumzo nao.
Kwenye taarifa yake chama cha National Salvation Front kilisema bado kinajiandaa kuitisha uchaguzi mkuu wa urais.
No comments:
Post a Comment