Pages
▼
Saturday, October 19, 2013
AG asema kesi dhidi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ni batili.
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali amedai mbele ya Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kuwa kesi ya Kikatiba inayomkabili Waziri Mkuu Mizengo Pinda, iliyofunguliwa mahakamani hapo inakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano na haikustahili kuletwa mbele ya mahakama hiyo.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju na jopo lake, jana waliwasilisha sababu tano za msingi za pingamizi hilo, ambapo alielezea sababu ya kwanza na ya tano.
Masaju alidai kuwa shauri hilo ni batili kwa kuwa linakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano na sheria ya haki, mamlaka na kinga za wabunge, ambapo alidai linakiuka ibara ya 100 ibara ndogo ya kwanza na ya pili.
Katika ibara ya 100 ibara ndogo ya kwanza inasema, nanukuu mheshimiwa ‘kutakuwa na uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano.
“Katika Mahakama au mahali pengine nje ya Bunge’ mwisho wa kunukuu mheshimiwa,” alisema Samaju. Aidha akinukuu ibara ndogo ya pili alieleza kuwa, ‘Bila ya kuathiri Katiba hii au masharti ya sheria nyingine yoyote inayohusika, Mbunge yeyote hatashtakiwa au kufunguliwa shauri la madai mahakamani kutokana na jambo lolote alilolisema au kulifanya ndani ya Bunge au alilolileta Bungeni kwa njia ya maombi, muswada, hoja au vinginevyo’.
Alidai msingi wa shauri hilo linatokana na jambo lililosemwa Bungeni na mmoja wapo wa wabunge wakati wa shughuli za bunge, Katiba inakataza jambo lolote linalotokana na utekelezaji wa shughuli za bunge haliwezi kuhojiwa na chombo chochote au mahakama na ndiyo sababu ya kudai kuwa shauri hilo ni batili.
“Tunachoshauri mahakama hii tukufu, hii si mara ya kwanza kwa Mahakama hii kupata shauri la aina hii, kulikuwa na shauri la Agustino Lyatonga Mrema dhidi ya Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya mwaka 1999, ambapo Mahakama iliamua kuwa maamuzi ya bunge hayawezi kuhojiwa nje,” alidai Masaju.
Masaju alidai waleta maombi wana njia mbadala ya kuwasilisha maombi yao kulingana na kanuni za kudumu za Bunge katika vifungu vya 71 na 73 toleo la Aprili 2013, ambapo zimeweka utaratibu wa kushughulikia mambo yanayotokea bungeni na uwajibikaji utafanyika ndani ya bunge.
Aidha Wakili mwingine wa upande wa Serikali, Gabriel Malata alidai shauri hilo lilifunguliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) ambapo walitakiwa kuzingatia masharti lakini hati hizo zinaonesha kusainiwa Dk Hellen Kijo Bisimba na Francis Stola na si wahusika wa taasisi hizo mbili.
Kwa hisani ya Habari leo.
No comments:
Post a Comment