Pages
▼
Friday, November 1, 2013
Posho za wabunge: Zitto, Lema katika vita ya maneno
Wabunge Wawili Maarufu wa Chadema, Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini) na Godbless Lema (Arusha Mjini) wameingia katika vita ya maneno ambayo chanzo chake ni kauli ya Lema aliyotoa katika kikao cha wabunge (briefing) kilichofanyika mjini Dodoma Jumanne wiki hii.
Lema akizungumza katika kikao hicho, anadaiwa kutoa maneno ambayo yalitafsiriwa na wabunge wengi kuwa yalikuwa yakimlenga Zitto kuhusu hatua yake ya kukataa posho na kumtuhumu kwamba ana ukwasi ambao unapaswa kuhojiwa.
Nilimtafuta Lema nikirejea taarifa iliyotolewa na Zitto akilalamika kwamba Lema alimshambulia katika kikao hicho cha wabunge wote na kwamba alikuwa akimlenga yeye.
Lema, hata hivyo, alikiri kuzungumzia suala hilo akisema:
“Mimi sikumtaja mtu, kwahiyo kama kuna mtu analalamika hilo ni suala jingine, ila mimi nilimaanisha nilichokisema”.
Hata hivyo, Zitto alieleza kuwa msimamo wa Lema ulikuwa unapingana na wabunge wengine wa Chadema, ambao waliwahi kupendekeza kuwa posho zifutwe.
Zitto alisema kuwa yeye mwenyewe, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika waliwahi kupendekeza kuwa posho zifutwe.
“Mimi sipokei posho kabisa, posho za vikao na ndiye mbunge pekee ambaye hapokei posho ya vikao tangu mwaka 2011,” aliongeza Zitto, ambaye anahudhuria mkutano unaozungumzia uendeshaji wa Serikali kwa uwazi huko London, Uingereza.
Zitto alisema malipo ya wabunge mpaka sasa ni makubwa sana ukilinganisha na hali ya wananchi wakati Serikali ikishindwa kulipa vizuri walimu na wauguzi.
“Hatuwezi sisi kama wabunge kuanza kulilia posho, wakati wananchi wetu hawana maji, hatuwezi kulilia posho. Mbunge anayetaka posho zaidi akafanye kazi nyingine na awaachie wanaoweza kuwakilisha watu waendelee,” alisema Zitto.
Lema, hata hivyo, alisema kwamba katika mkutano huo aliweka bayana kwamba umasikini siyo uzalendo na kusisitiza kuwa wabunge wanapaswa kuwa na maslahi bora na wakati huohuo wana wajibu wa kuwatetea watumishi wengine wa umma.
“Nilisema huwezi kuzuia taasisi moja kupewa maslahi bora eti tu kwa sababu watumishi wengine hawalipwi vizuri, ni haki wabunge kulipwa vizuri na wakati huo wapiganie maslahi ya watumishi wengine,” alisema Lema na kuongeza:
“Kwahiyo nikasisitiza kwamba nawashangaa wale ambao wanakataa posho ya Sh80,000 na ukienda kuchunguza wanakatwa fedha zote kutokana na mikopo waliyochukua, lakini bado wakija sehemu kama Arusha wanalala kwenye hoteli ya gharama kubwa kati ya Dola za Marekani 150 na 600”.
Alisema katika mazingira hayo kunakuwapo maswali mengi yasiyokuwa na majibu na kwamba mbunge wa aina hiyo alitakiwa anapokuwa katika mji wowote nchini aishi katika hoteli yenye thamani kati ya Sh20,000, 30,000 na hata Sh50,000.
“Kwa hiyo ikiwa unakataa posho ya Sh80,000 halafu unalala chumba cha Dola 600 hustahili kupata credibility (sifa) stahili, ni unafiki tu na kutafuta sifa za kipuuzi,”alisema Lema.
Alisisitiza kwamba wabunge wa Tanzania hawalipwi ipasavyo na kwamba kudai malipo ya ziada hakuwaondolei wajibu wao wa kuwatetea watumishi wengine wa umma ambao pia malipo yao ni kidogo.
“Kuna hatari ya kuona kwamba Sh80,000 au Sh200,000 ni fedha nyingi, ni kwamba kama sisi wabunge tutalipwa Sh50,000 basi maana yake ni kwamba walimu au polisi tutaridhika wakilipwa hata Sh10,000,”alisema Lema.
Zitto Kabwe leo hii asubuhi aliandika hivi ktk ukurasa wake wa Facekook....!!
"Enyi Watanzania, wabunge wenu wanataka posho ziongezwe na mishahara. Mbunge mmoja wa upinzani kanisemea mbovu huko Dodoma kwenye kikao cha wabunge eti mimi ni kikwazo kwa wao kuongezewa posho. Kasema nikiwa Arusha nakaa chumba cha dola 600 kwa siku. Hivi Hoteli gani Arusha ina chumba dola 600 kwa siku? Albert Msando naomba msaada nikija Arusha unionyeshe hiyo hotel japo nione chumba cha dola 600 kinafafanaje...."
No comments:
Post a Comment