Pages

Sunday, January 12, 2014

ILI KUKABILIANA NA MADAWA YA KULEVYA KAMATI YAUNDWA KIA



Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro, (KIA)
 
Kilimanjaro, (KIA), imeunda Kamati ndogo ya Ulinzi na Usalama wa uwanja ili kukabiliana na uingizwaji wa dawa za kulevya.

Mkurugenzi Huduma wa Kadco, Bakari Murusuri, alisema kuundwa kwa kamati hiyo ni moja ya utekelezaji wa maagizo ya Mamlaka ya Usafirishaji wa Anga Tanzania (TCAA).

“Tumeunda kamati ndogo ya ulinzi na usalama inayokutana kila wiki kuweka mikakati ya pamoja na kubadilishana taarifa. Kamati hii ndogo imeundwa kuzingatia maagizo ya TCAA na moja kati ya ajenda zake ni namna ya kukabiliana na dawa za kulevya,” alisema wakati akisoma taarifa fupi ya shughuli za maendeleo za KIA kwa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe mwishoni mwa wiki iliyopita.

Alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama wa uwanja pia imeamua kuiweka agenda ya dawa hizo kama ya kudumu katika vikao vya kila mwezi.

Hali kadhalika alisema wameongeza ushirikiano na mashirika ya ndege kwa namna ya kubadilishana taarifa za kihalifu hasa kwa kuangalia mapito ya abiria wanaohisiwa kusafirisha dawa za kulevya.

Alisema kwa mfano, Agosti 15 mwaka jana, waliomba kuwa wanachama katika Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Taifa ambapo wamekubaliwa ili waweze kubadilishana mbinu na mikakati ya kukabiliana na vitendo vya uvunjaji wa sheria na wadau wengine.

“Tumeimarisha vifaa vya doria kama vile CCTV pamoja na viona mbali kwa ajili ya kufuatilia nyendo za watu mbalimbali uwanjani na maeneo yanayotuzunguka.

“Kampuni ipo katika mchakato wa kununua ving’amuzi vya kubeba vitakavyobaina aina ya milipuko kwa ajili ya kunusa milipuko ya aina zote na kwamba wamepeleka ombi la kupewa mbwa wa kunusa dawa za kulevya katika kikao cha Ulinzi na Usalama wa Taifa ili watusaidie katika mapambano dhidi ya usafirishwaji wa dawa za kulevya,” alisema.

Akizungumzia mikakati mingine ya ulinzi, Murusuri, alisema wameanza kuvishirikisha vikundi vya kijamii kutoka vijiji sita vinavyozunguka kiwanja katika ulinzi shirikishi na doria, pamoja na kufanya vikao vya mara kwa mara.

Pia alisema wanawaelimisha wafanyakazi wote wa uwanja kuhusu madhara yanayojitokeza kutokana na matendo ya kigaidi, namna ya kutoa taarifa pale wanapohisi mtu kuwa na viashiria vya kigaidi, pamoja na kuimarisha upekuzi wa abiria na mizigo yao kabla hawajasafiri kwa ndege.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment