Ndugu wanahabari na waTanzania wenzangu,
Nimekuwa nikilazimika kujibu
maswali mbalimbali kutoka kwa wanahabari, ndugu, jamaa na marafiki
kuhusiana na namna mchakato wa kuandika katiba mpya ya Taifa letu
unavyoenda; wengi wakipenda kujua nini mtazamo wangu kuhusu mambo mengi,
haswa hili la serikali mbili ama tatu kwenye muungano wetu. Mara nyingi
nimekuwa nikikwepa kusema msimamo wangu ni nini kwa sababu niliona ni
vema nikajipa muda wa kutafakari kabla ya kuamua kujenga msimamo yangu.
Ila kwa kuwa wakati wa kwenda Bungeni umefika na mimi nimepata bahati ya
kuwa miongoni mwa wajumbe wa Bunge hili la kihistoria nimeona leo nitoe
mtazamo wangu.
Kwanza, nianze kwa kuonesha wasiwasi wangu kama
tutaweza kufika salama huko tuendako. Si kwa sababu za kitabiri kama
mnajimu, la, ni kwa sababu za kisayansi, ambazo nitaziweka wazi hapa
kama ifuatavyo:
(i.) Pamoja na kwamba tume imefanya
kazi nzuri ya kukusanya maoni na kuyaweka katika nyaraka ambayo
tutapaswa kuifanyia kazi, napata shida kama walikuwa makini katika
kuendesha zoezi hili. Kivipi, binafsi napata shida na methodology
iliyowawezesha kufikia ‘conclusion’ madhubuti kwamba watanzania asilimia
61 walitaka serikali tatu. Kwa sababu za kisayansi naona tume ya Mhe.
Jaji Warioba imepotoka na kwamba kusema hivyo ni kutaka kulazimisha
uhalali wa hoja hii nyeti kwenye dokumenti ya Rasimu ya Katiba
tunayopaswa kuipitisha bila kuwa na msingi wa kitakwimu unaotokana na
njia (methodology) za kisayansi za kukusanya ‘data’ na kutafuta
‘validity’ na ‘generalizability’ ya taarifa husika.
(ii.) Kwa jinsi mchakato ulivyo ni ngumu kusema kuwa leo
tutaweza kubadili jambo nyeti kama la ‘Muundo wa Muungano’ kuwa uwe ni
wa Serikali mbili, ama moja, wakati mapendekezo ya Tume, ambayo
‘yanaelezewa’ na Tume kuwa yanatokana na ‘maoni’ ya wananchi walio
wengi, 61% na pili mabaraza ya katiba [cf. Muundo katika mchakato huu ni
wa pyramid, kwamba unaanza na maoni ya wengi huku chini kwenye kitako,
baadaye mabaraza ya katiba hapo katikati na mwisho Bunge la Katiba,
kabla ya kura ya maoni]. Hivi inawezekana wapi Bunge Maalum la Katiba,
kwa hapa tulipofikia, likafanya mabadiliko kwenye mambo yanayohusu
‘muundo’ (structure) wa Katiba? Yaani, kwamba inawezekana vipi wajumbe
hawa 640 wabadilishe jambo zito la kimuundo kama hili? Kimantiki haingii
akilini. Uhalali huo unatoka wapi? Lakini pia hapa hatuwezi kuondoa
ukweli kwamba malalamiko na manung’uniko ya baadhi ya watu yana mashiko,
kuwa hivi kama hoja ya Chama Cha Mapinduzi ilikuwa ni kuilinda ‘status
quo’ ya muungano wa serikali mbili na kama walifanya kazi ya
kuwaelimisha wanaCCM nchini, na wanaCCM walikuwa wengi zaidi kwenye
mabaraza ya katiba ya wilaya [walishinda kwa zaidi ya asilimia 65,
inatokeaje asilimia 61 watake muungano wa serikali 3?]
Nini
tafsiri ya haya yote? Kwamba ukisema unabadili leo muundo wa Muungano
ukaleta wazo tofauti na lile linalotokana na mapendekezo ya tume, kama
yanavyosomeka kwenye Rasimu (sura ya 6), mfano ukasema, ziwe serikali
mbili tu badala ya tatu zinazopendekezwa, maana yake unaongelea kuanza
upya kutengeneza vifungu vipya vya ‘kimuundo’ vya serikali za mitaa,
wawakilishi wa wananchi, mambo ya wakuu wa mikoa ama majimbo(provinces) –
jambo ambalo litakuwa cumbersome! Vurugu mechi bila uwepo wa rasimu!
Swali la kujiuliza hapa ni kwamba – hivi tume hawakuliona hili? Pengine
wangeweka chaguzi (option) pembeni, maana maoni yote haya wanayo, ila
kwa sababu ya muundo wa Muungano ‘waliouchagua’ hawakupenda kuelezea
mambo binafsi ya serikali hizi ‘mbili’ za ‘iliyokuwa Tanganyika’ na
Zanzibar kwa madai kwamba jukumu lao ni kuandaa rasimu ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kinachoonekana hapa ni kwamba
walikwishaamua kuwa ziwepo serikali tatu kwa madai kuwa ndiyo maoni ya
wananchi na kwa kuzingatia msingi wa hoja kwamba Bunge la Katiba
haliwezi kuwa na uhalali wa kubadili mambo ya msingi ya kimuundo wa
katiba, kama hili la Muundo wa Muungano, bali ‘kuboresha’ tu yale
yaliyomo. Mtu makini atahoji kuwa ni kwa nini wamekwepa kuzungumzia
ukweli kwamba ‘Tanganyika’ hayupo? Na nini itakuwa hatma ya Katiba yake?
Na ni lini wabia hawa wa Muungano walikaa wakakubaliana washirikiane
kwenye mambo yapi kwenye huo muungano wa Shirikisho?
Sasa
wabunge wa Bunge maalum la katiba tukiukataa huu muundo wa serikali tatu
nini kitatokea? Maana yake sehemu kubwa ya rasimu hii italazimika
kubadilishwa.
(iii.) Jambo lingine ambalo litatusumbua
ni kuwa, vipi kama wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba tukiamua tujenge
msimamo kwenye hoja ya Serikali Moja itakuwaje? Maswali mengi yataibuka
bila kupata majibu hapa, kuwa ni nani atakuwa ‘Mpatanishi’ kwa niaba ya
Tanganyika (ama Tanzania bara)? Maana Zanzibar yupo na ana uhai wake
kamili, Tanganyika yuko wapi hapa?
Mhe. Jaji Joseph Warioba na wenzake wanapaswa wajibu maswali haya:
1. Ni njia (methodology) ipi ya kisayansi na kitakwimu walitumia
kufikia ‘conclusion’ hiyo madhubuti kabisa kuwa 61% ya watanzania
walitaka Muundo wa Serikali Tatu? Watueleze watanzania sample size,
sampling technique, sampling frame na namna walivyowafikia na kuwahoji
watu hao.
2. Watueleze ni nani aliyewatuma kwenda kubadilisha Muundo wa Muungano?
3. Ni nani sasa atakuwa na mamlaka ya kuandika Katiba ya Serikali ya
Tanganyika (ama Tanzania Bara – ambaye aliishakufa?), kama tukiamua
kwenye Bunge la Katiba kupitisha Rasimu hii yenye Muundo wa Muungano wa
Serikali tatu? Tunaanzia wapi kumfufua Tanganyika?
Maoni
yangu: Mtu yeyote mpenda demokrasia ataona wazi kwamba kuna utata
uliogubikwa na ukungu wa presha za kisiasa za kuona zoezi hili
linakamilika. Utata wa uhalali wa Bunge la Katiba kubadili hoja za
msingi kwenye rasimu ni jambo zito, na mashaka kwamba pengine Jaji
Joseph Warioba na wenzake walikuwa na ajenda yao ya siku nyingi ya
kuleta serikali tatu kinyume na matakwa ya Chama Tawala, CCM, ni jambo
zito zaidi. Hivyo, kuondoa mamlaka na madaraka ya wananchi (kama kweli
yapo kama inavyosema tume) kwenye jambo zito la kimsingi kama Muundo wa
Muungano ni jambo linalotishia usalama wa mchakato na ni jambo
lisilokubalika kwa kuwa linaondoa haki, wajibu, mamlaka na madaraka ya
wananchi kufanya maamuzi kuhusu katiba yao (an act of popular
sovereignity). Mkanganyiko huu unatia mashaka zaidi ya kuleta mwangaza
wa mabadiliko ya kutokea kwa maridhiano. Jaji Warioba na wenzake
walilijua hili na wameleta ‘chaos na frustration’ kwa maksudi kwa
kujificha chini ya kivuli cha ‘uhalali’ wa Bunge la katiba (yaani
‘legitimacy of rule or of law is based on the consent of the governed’)
na nadharia pana ya demokrasia yenye msingi kwenye kanuni za ‘popular
sovereignity’ wakijua kabisa wabunge tutashindana, tutatofautiana!
Mimi nina maoni kwamba, ili mchakato uishe salama, Mhe. Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete aingilie kati, atumie
mamlaka yake kusitisha mchakato huu mpaka itakapoundwa tume nyingine ya
kukusanya maoni ya wananchi kuhusu suala la Muundo wa Muungano na kisha
ipigwe kura maalum ya maoni kuhusiana na jambo hili ili watanzania
washiriki kikamilifu na waamue na siyo kufanya maamuzi ya kubadilisha
Muundo wa Muungano bila kutupa fursa ya kujadiliana na kushiriki kufanya
uamuzi kuhusu jambo hili. Ni jambo lisilo na busara hata kidogo kwenda
kujadili Rasimu ya Katiba bila kuwa na suluhu inayokubalika kuhusu
Muundo wa Muungano wetu.
Kama kuna presha ya muda wetu wa
miaka mitano kuisha kuna dirisha la kutokea; tusogeze mbele muda wa uhai
wa Uongozi wa awamu hii ama turudi nyuma tufanye mabadiliko ya sehemu
za katiba zinazohusiana na Tume ya Uchaguzi tu. Hatuna namna ya kukwepa
moja kati ya mambo haya kwa sababu hata tukifanikiwa kufunika kombe
mwanaharamu apite, tukapitisha Katiba hii, bado tutahitaji kufanya
mabadiliko makubwa ya Sheria mbalimbali nay a kitaasisi kutokana na
Katiba mpya itakayokuwa imepatikana, zoezi ambalo kwa kila namna
litahitaji muda wa kutosha na sioni kama upo! Demokrasia ni gharama na
haikwepeki!
Maswali ni mengi zaidi ya Majibu. Wasiwasi ni
mwingi kuliko uhakika. Tutafika salama kwenye kupata Katiba hii kweli?
Ni bora tukawie kuliko kuvurunda. Tusikimbie kwa kasi bila kutazama
tuendako, tutambae lakini macho njiani na mbele tunakoelekea.
Tamko hili limetolewa na Ofisi ya Mbunge, Jimbo la Nzega.
HK (Nimesaini)
Dkt. Hamisi Kigwangalla, MB.
No comments:
Post a Comment