Rwanda
imemkataa Balozi mteule wa Tanzania, Mussa Siwa, ambaye alitakia na
serikali kwenda kufanya kazi kwenye ubalozi wa Tanzania nchini
humo.Taarifa kutoka Rwanda na duru za ndani ya serikali ya Tanzania
zimeeleza serikali ya nchi hiyo imemkataa balozi huyo kwasababu
mbalimbali zikiwemo za kiusalama.
Habari kutoka ndani ya Ikulu ya Rwanda zinaeleza kuwa serikali ya nchi
hiyo imemkataa balozi Siwa, baada ya kumshuku kuwa ni jasusi. Siwa kabla
ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, alikuwa ofisa katika ubalozi wa
Tanzania nchini Ujerumani.
Tazania kwa sasa haina balozi nchini Rwanda tangu Dr.Marwa Matiko
amalize muda wake wa kufanya kazi hiyo. Nafasi hiya kwa sasa inakaimiwa
na Francis Mwaipaja,ambaye kabla ya kupelekwa Rwanda alikuwa msaidizi wa
katibu mkuu kiongozi, Ombeni Sefue.
Ofisa mmoja mwandamizi wa Ikulu ya Rwanda aliliambia MTANZANIA kuwa
viongozi wa nchi hiyo wanachukuwa tahadhari dhidi ya wanadiplomasia wa
Tanzania wanaofanya kazi nchini Rwanda , tangu nchi hizi mbili ziingie
katika vita ya maneno mwaka jana.
‘’Viongozi hapa wamekuwa na hofu kubwa na Tanzania na kufanya wawe
macho na watanzania wanaoishi hapa na hasa maofisa ubalozi na ndio maana
wamemkataa balozi huyo mteule’’. Alisema mtoa taarifa wetu.
Wafuatiliaji wa maswala ya kidiplomasia wametafsiri kitendo hicho kuwa
ni mwendelezo wa kutofautiana kati ya serikali za nchi hizi mbili.
Rwanda iliingia katika mgogoro na Tanzania baada ya kuchukizwa na
ushauri uliotolewa na Raisi Jakaya Kikwete wa kuitaka serikali ya nchi
hiyo kufanya mazungumzo na kundi la waasi la FDLR, ambalo limejichimbia
ndani ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Rais kikwete alitoa ushauri huo mbele ya katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa
Ban Kin-Moon na Raisi wa Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini-Zuma,
wakati wa mkutano wa viongozi wa ukanda wa maziwa makuu ya afrika
uliofanyika mjini Addis Abab, Ethiopia, Mei, mwaka jana.
Ushauri huo ulipokelewa vibaya na Rais Kagame na waziri wa mambo ya nchi
za nje wa nchi hiyo, Louise, Mushikiwabo, ambao walitoa kauli za
kumdhalilisha Rais Kikwete.
Mkataba wa Vienna
Hata hivyo, Rwanda
ina uhuru wa kisheria wa kumkataa balozi mteule wa kigeni kama inaona
hafai kwenda kuishi nchini humo. Kifungu cha nne cha mkataba wa
kimataifa wa Vienna wa mwaka 1961 unaozungumzia masuala ya kidiplomasia
baina ya mataifa,kinatoa uhuru wa nchi kumkubali balozi mteule wa
kigeni. Mathalani Tanzania , mwaka jana ilimkataa balozi mteule wa
Ujerumani, Margit Hellwig – Boette, ambaye alitakiwa kuja kuwa balozi
hapa nchini mara baada ya kumaliza muda wake nchini Kenya.
Sefue asema hana taarifa
Akizungumzia suala
hilo, Sefue alisema taarifa hizo hajazipata na kwamba wizara ya mambo
ya nje ndiyo inayoweza kufahamu vizuri suala hilo. ‘’Mimi sifahamu
chochote kwakweli, nadhani watu wa wizara ya mambo ya nje ndiyo wanajua
process (taratibu) hizi ndiyo maana hata jina la huyo balozi
aliyekataliwa silijui’’ alisema.
Wizara ya mambo ya nje washangaa
Nae mkuu wa
kitengo cha mawasiliano cha wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa
kimataifa, Mkumbwa Ally, alishangaa na kuhoji kuwa hizo taarifa
tumezipata wapi kwani ni habari za ndani.
‘’Hizo taarifa mmezipata wapi, ni taarifa za ndani, chanzo chako cha habari ni nani’’,alihoji
ally. Hata hivyo, alipoombwa kuzungumzia swali la msingi alisema suala
hilo lipo nje ya uwezo wa wizara yake kwani Rais Kikwete ndiye mwenye
mamlaka ya kuteuwa na kutangaza jina la mteule huyo.
“Kiujumla sijapata taarifa za uhakika kuhusu suala hilo kwa sababu
uteuzi wa balozi yeyote ni ‘process’ utaratibu’’ , hivyo hatuwezi kujua
jina lake mpaka uteuzi wake ukamilike ndipo tutangaziwe na mwenye
mamlaka hayo ni Rais, hivyo siwezi sema chochote ‘’ alisema.
MTANZANIA lilifanya jitihada za kumtafuta Siwa bila mafanikio kuzungumzia suala hilo.
Katika siku za hivi karibuni uhusiano baina ya Tanzania na Rwanda
umeonekana kusuasua na hata viongozi wa nchi hizi mbili wamekuwa
wakidaiwa kukwepana katika hafla mbalimbali zinazohusu nchi zao pamoja
na zile za jumuiya ya Africa mashariki(EAC).
Wiki mbili zilizopita, Rais kagame alikacha kuhudhuria sherehe za
maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na zanzibar
zilizofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na marais wote
wanachama wa ( EAC).
Mbali na Kagame kutokuhudhuria maadhimisho hayo, pia aliukacha mkutano
wa wakuu wa nchi za EAC uliofanyika jijini Arusha, lakini alikwenda
nchini Kenyana kuhudhuria kikao cha viongozi wa nchi za Afrika
Mashariki wanaounganishwa na mradi unaoitwa ‘ Northern Corridor
Infrastructure Project’. Waziri Mkuu Pinda aliiwakilisha Tanzania katika
mkutano huo.
Source: Gurudumu la Habari
No comments:
Post a Comment