Ubalozi wa Marekani
Dar es Salaam
TANZANIA
Taarifa kwa vyombo vya Habari
Desemba 11, 2014
Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia: Mkataba wa Pili wa MCC na Tanzania Utategemea Hatua Zitakazochukuliwa Dhidi ya Ufisadi na Mageuzi ya Kisera
Dar es Salaam, Tanzania - Hapo tarehe 10 Desemba 2014 Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Marekani la Changamoto za Milenia (MCC) ilikutana katika mkutano wa kila mwaka wa kuchagua nchi zitazopatiwa fedha na MCC. Katika mkutano huo Bodi ilielezea hofu na masikitiko yake kuhusu hali ya rushwa nchini Tanzania, ikiwa ni pamoja na yale yaliyojitokeza hivi karibuni katika suala linalohusu kampuni ya kuzalisha umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL). Japokuwa bodi ilipiga kura ya kuiruhusu Tanzania iendelee na maandalizi kwa ajili ya mkataba wa pili, kwa dhati kabisa inaihimiza serikali ya Tanzania kuchukua hatua thabiti na mahsusi za kukabiliana na rushwa kama sharti la msingi kwa bodi hiyo kufanya maamuzi ya mwisho ya kuidhinisha mkataba huo.
Tamko kamili la mkutano huo wa tarehe 10 Desemba 2014 wa Bodi ya Wakurugenzi inapatikana katika tovuti ya MCC kwa anuani ifuatayo: http://www.mcc.gov/pages/press/statement-121014-tanzania-selection
Katika tamko hilo kwa umma, Bodi ilieleza kutambua umuhimu wa kusubiri na kuona utekelezaji kamilifu wa tamko lililotolewa na Ikulu ya Tanzania hapo tarehe 9 Disemba kwamba itachukua hatua za haraka na kutoa maamuzi dhahiri na thabiti kuhusu maazimio ya Bunge juu la suala la IPTL.
Naye Balozi wa Marekani nchini Tanzania alisema kuwa “Kupigwa hatua katika mapambano dhidi ya rushwa ni muhimu sana kwa mkataba mpya kati ya MCC na Tanzania na katika kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini Tanzania. Tumetiwa moyo na tamko lililotolewa na Ikulu hapo tarehe 9 Disemba kwamba hivi karibuni itashughulikia maazimio ya bunge kuhusu IPTL. Tunatoa wito kwa serikali kuchukua hatua za haraka kuhusu suala hili hasa kutokana na uzito wake katika masuala muhimu kadhaa ya maendeleo.”
Hali kadhalika, Bodi iligusia makubaliano kadhaa yaliyofanyika ambapo Tanzania iliahidi kufanya mageuzi ya kisera, kimuundo na kitaasisi ili kuongeza ufanisi na uwazi katika taasisi zake na katika sekta ya nishati kwa upana wake. Balozi Childress aliendelea kusema kuwa, “tunafurahi kwamba mchakato wa majadiliano ya maandalizi ya mkataba wa pili utaendelea kwa miezi kadhaa ijayo. Tunapenda kusisitiza kuwa ni lazima ahadi hizi zitekelezwe kabla Marekani haijafanya maamuzi ya mwisho kuhusu mkataba wowote mpya na Tanzania.”
Tanzania ilikuwa mojawapo kati ya nchi kumi zilizojadiliwa na Bodi ya MCC iliyokutana kuangalia kama nchi hizi zimekidhi vigezo vya kuendelea na mchakato wa kuandaa mikataba mipya. Iwapo utapitishwa, huu utakuwa mkataba wa pili wa MCC kwa Tanzania. Kati ya mwaka 2008 na 2013 MCC ilitekeleza mkataba wa uwekezaji wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 698 uliowezesha utekelezaji wa miradi ya maji, barabara na nishati ya umeme nchini kote Tanzania. Chini ya mkataba huo mtandao wa nyaya za umeme wenye zaidi ya kilomita 3000 ulijengwa, jumla ya kilomita 450 za barabara pia zilijengwa, hali kadhalika, mitambo mikubwa miwili ya usafishaji maji na njia ya kurukia ndege katika kiwanja kimoja cha ndege ilijengwa.
Shirika la Changamoto za Milenia ni taasisi ya Serikali ya Marekani inayotoa misaada kwa nchi zinazoendelea. Shughuli za MCC zinajengwa katika msingi kwamba msaada utaleta ufanisi na matokeo makubwa zaidi pale tu unapoimarisha utawala bora, uhuru wa kiuchumi na uwekezaji katika watu ambao unakuza uchumi na kuondoa umasikini.
686 Old Bagamoyo Road, Msasani, P.O. Box 9123, Dar es Salaam
Telephone +255-22-229-4000, Fax +255-22-229-4722
http://tanzania.usembassy.gov
No comments:
Post a Comment