Pages

Tuesday, January 12, 2016

UVCCM waitaka CCM kumvua Uwanachama Rais Mstaafu wa SMZ Aman Abeid Karume

HOTUBA YA MWENYEKITI WA UMOJA WA VIJANA WA CCM  SADIFA J. KHAMIS AKIMKARIBISHA MAKAMU M/KITI WA CCM ZANZIBAR AMBAE PIA NI RAIS WA ZANZIBAR (MBLM) KATIKA KILELE CHA MATEMBEZI YA UVCCM KUADHIMISHA MIAKA 52 YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR JUMATATU 11 JANUARI 2016.
Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye ni Makamu Mwenyekiti  wa CCM Zanzibar.  Dk Ali Mohamed Shein
Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Balozi Seif Ali Idd.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM  Zanzibar  
Mama zetu wapendwa Mama  Mwanamwema Shein na Mama Asha Suleiman Idd.
Ndugu  Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM  Taifa
Vijana kutoka katika maeneo mbalimbali Visiwani Zanzibar, Wazee, maveteran wa UVCCM , Waasisi  wetu  wageni waalikwa Mabibi na Mabwana .
Asalam  Aleykum.
Bwana Yesu Asifiwe.
Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti
Leo tumekusanyika ikiwa imetimia miaka 52 tangu pale wazazi wetu walipoamua kwa dhamira moja ya kuukata mzizi wa fitna kwa kuudondosha utawala wa mabwenyenye na usultan uliovikalia visiwa vya Zanzibar toka mwaka 1804 hadi mwaka 1964.

Ndungu zangu, Kukusanyika kwetu hapa katika viwanja vya Maisara Suleiman tunalenga kukumbuka wazee  na  waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wao wa kujitoa muhanga kwa ajili ya kupigania ukombozi wa nchi yetu, na hatimae kufanikisha mapinduzi matukufu.

Ndugu mgeni Rasmi, Tunapenda ifahamike kuwa jambo la kufanya Mapinduzi  halikuwa  jambo jepesi na rahisi kama inavyoonekana au kutaka kuchukuliwa na baadhi ya watu ambao sasa wanaonekana wamelishwa urojo na kuanza kusahau tulikotoka na kuanza kutamani kurejesha makovu ya ukoloni ambao wanataka kuurudisha kwa  mlango wa uani.
MSIMAMO WETU UVCCM
Sisi Vijana wa CCM, kwetu Mapinduzi yapo na yanaendelea ndani ya Chama na nje ya Chama, na sasa tunakitaka chama kwa sasa kukaa tayari kwa ajili ya mapinduzi makubwa ambayo yataendana na kauli mbiu yetu ya HAPA KAZI TU.

Aina ya watu na viongozi hao baadhi yao wako nje na ndani ya CCM. Wengine kati ya hao ni wale wenzetu ambao ndiyo  waliofaidi mno matunda ya Mapinduzi na sasa wamejivika ngozi ya usaliti  na kuwa maadui wa kuyayateketeza Mapinduzi yetu kwa kushirikiana na wakoloni wapya ambao ni maadui wa asili wa Mapinduzi ya Zanzibar.
TAMKO LETU UVCCM
Tunataka Tanzania isikie, Afrika itambue na dunia ijue kuwa UVCCM kwa sauti ya juu na umoja wetu tunatamka  wazi wazi kwamba viongozi wote wanaokihujumu chama na kutaka kurejesha utawala wa kikoloni visiwani Zanzibar VIONGOZI HAO TUNAWAJUA  na wao WANAJIJUA VIZURI NA WANATUSIKIA HIVI SASA, Tunataka dunia ijue na kila mmoja wetu hapa tulipo ajue. T
Sisi vijana tunatamka kwamba, tunachotaka kwanza ni usalama wa Chama chetu, uhai wa kudumu kwa Mapinduzi yetu matukufu, CCM KWANZA MTU BAADAE.
MHESHIMIWA MGENI RASMI KWA RUHUSA YAKO NAOMBA KUTUMBUA JIPU LEO, NA KUANZA LEO TUNAANZA SAFARI YA KUTUMBUA MAJIPU
Tunakitaka Chama chetu kuchukua hatua muhimu kama zile zilizochukuliwa mwaka 1987 wakati ambapo chama kilitumbua majipu ya aliyekuwa Waziri Kiongozi Seif Sharif Hamad na wenzake sita, akafuatia Mansoor Yussuf Himid , Hassan Nassor Moyo kwa kuvuliwa uanachama na kufukuzwa katika chama.
NA LEO KWA KAULI MOJA SISI VIJANA WA CCM TUNATAKA AVULIWE UANACHAMA NA KISHA AFUKUZWE MARA MOJA Amani Abeid Karume ndani ya CCM.
NARUDIA TENA
NA LEO KWA KAULI MOJA SISI VIJANA WA CCM TUNATAKA AVULIWE UANACHAMA NA KISHA AFUKUZWE MARA MOJA Amani Abeid Karume ndani ya CCM.
Kwa sababu tumebaini ya kuwa yeye ni kirusi cha AMANI YETU, UMOJA WETU NA MSHIKAMANO  ndani ya Chama na sasa ni wakati wa kuweka ANTI-VIRIUSI

Ndugu Mgeni rasmi ieleweke kwamba miti siku zote haiwezi kuteketezwa na shoka bila kuanza kufanya ushirikiano au ushirika na mti ukawa mpini.

Amani Karume ameamua kuwa mpini unaoshirikiana na shoka ili kuteketeza na kukimaliza  Chama Cha Mapinduzi, sasa kabla hajakimaliza Chama basi ni wakati wa kumweka pembeni ili chama kisonge mbele.
Rai yetu kwako mheshimiwa mgeni rasmi, Kama mnaona na hamtaki kuchukua hatua za kinidhamu na kimaadili, sisi UVCCM tutatumia njia  nyingine  ya kufikisha kilio chetu bila aibu wala muhali.

Mapinduzi ya Zanzibar hayana nembo ya mtu, na si miliki ya  familia yoyote ya mtu,  bali ni urithi na tunu, halali za kila Mzanzibari na Mtanzania. Kuheshimu, kulinda na kuyaenzi Mapinduzi ni jukumu la kila mmoja wetu na si dhamana ya mtu mmoja.

Ndugu mgeni rasmi, ikumbukwe kuwa Ishara, vigezo na dalili za kuyaheshimu Mapinduzi matukufu, zinaoonekana bila ya mwanga wa tochi kwa mtu au kiongozi kadri inavyoonekana, anavyotenda na aina ya mwelekeo wa matendo yake, na ya familia yake na watoto wake .
Kamwe, wananchama na viongozi Wanaoheshimu Mapinduzi yetu hawawezi kushirikiana na maadui wa Mapinduzi, Unapomuona mwenzenu au motto wake ameamua kushirikiana  na Mpinzani  wenu,  pika pakua , ahlan wasahlan bila kujali wala kukubali, hapo mjue sasa shoka limetiwa mpini na miti yote itateketea na ardhi kubaki jangwa.

Ndugu mgeni rasmi, Uamuzi wa kufanya Mapinduzi lilikuwa ni jambo la kufa au kupona. Hadi watu wanyonge wanapofikia  uamuzi  wa kufanya hivyo, aidha wamechoshwa na kukithiri kwa madhila, ukandamizaji, kunyimwa haki na usawa  , kukosa fursa mbali mbali katika nchi  yao ikiwemo na  kutopatiwa  huduma bora  za elimu ,afya, matibabu huku wakinyimwa  wasitumie rasilimali za nchi yao,  ardhi au kutokuwepo kwa uhuru wa kujitawala.

Miaka 52 iliopita waafrika katika Visiwa vyetu hawakuonekana binadamu wenye hadhi, heshima na hawastahili kupata jambo lolote lenye stahiki kama binadamu wengine.
Wapo viongozi ambao waliopewa nafasi za juu Serikalini wakachana  kumbukumbu  za vitabu, picha za historia za mateso walioyapata bibi, Babu , shangazi na mama zetu wakati wakitumikishwa kwenye kazi ngumu kwa maslahi ya kuutajirisha ukoloni wa ufalme.

Baada ya kutekeleza mradi wao huo wakapata sasa wanapigana hata historia ya kweli ya ukandamizaji na ubaguzi wa kikoloni usielezwe wala wanafunzi wasifundishwe mashuleni kwa madai kuwa kutarudisha chuki, hasira na hasama.

Wakati wao wakikataza jambo muhimu lisifanyike wanapita huko huko wakisema wanataka nchi yao, wanapigania uhuru wao jambo linalothibisha kwamba  hata mapinduzi yetu ambayo ndiyo uhuru na ukombozi wetu hawayatii na kuyaheshimu ipasavyo  .

Ndugu Mgeni rasmi.
Naomba nitumie nafasi hii muhimu kuwaeleza kinagaubaga vijana wenzangu mahali popote walipo watambue kuwa wakoloni wote walioondoka katika nchi kadhaa za Afrika wamerudi kwao lakini wakoloni wa zanzibar bado wapo na wanakesha usiku na mchana kutaka kutupora Mapinduzi yetu. Wamepania kutupora kwa kushirikiana na mamluki waliomo ndani na nje ya chama chetu.

Sisi vijana wa UVCCM, Tunawaambia wale wote wanaojidanganya huku wakiota na kufikiria kwamba siku moja watatunyang'anya urithi wetu ili kuitawala tena nchi yetu. Jambo hilo nasema halitatokea na iwapo likitokea basi huyo mtawala ataitawala mikarafuu, minazi na miembe na si wanadamu.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, Leo sio siku ya hotuba kwangu naomba nichukue FURSA hii kutoa Shukrani kwa Mheshimiwa Rais kwa kukubali mwaliko wetu.
Shukrani kwa Mama Mwanamwema Shein kwa kukupa mawazo mazuri ya kutufikiria wanao kwa kila jambo.
Shukrani kwa Balozi Seif Ali Idd na mama Asha kwa busara na ushauri wa wao kwetu UVCCM.
Shukrani kwa Mhe. Otien Igogo Naibu Kamanda Mkuu – Bara kwa ushirikiano mzuri anaotuonyesha ndani ya Jumuiya yetu.
Shukrani kwa wake zangu wawili mama Salma Sadifa na Wastara kwa maliwazo na ushauri mzuri kwangu namna ya kuwaongoza UVCCM na Jimbo la Donge
Mwisho napenda kumshukuru kwa dhati kabisa Kaimu Katibu Mkuu Shaka Hamdu Shaka na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM - Zanzibar Abdulghafari na Ndugu Kizigo Naibu Katibu Mkuu Bara kwa kazi kubwa na nzito wanayoifanya ya ndani ya UVCCM.
Naomba nichukue fursa hii adhimu kumualika Balozi Seif Ali Idd Naibu Kamanda Mkuu wa UVCCM Zanzibar, MZEE SHUPAVU NA MWELEDI, AMBAE KWETU TUNAMUONA NI MWAROBAINI AMBAO HATA KAMA NI MCHUNGU LAZIMA WAPINZANI WAUNYWE TU, aje hapa kwanza asalimie kisha uweze kukukaribisha wewe kuja kuzungumza na umati wa Vijana.
Karibu sana.

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment