HOTUBA YA MHE. UMMY MWALIMU (MB), WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO WAKATI WA MAKABIDHIANO YA GARI LA HUDUMA ZA DHARURA (AMBULANCE) LA KITUO CHA KITAIFA CHA KURATIBU MATUKIO YA SUMU ZINAZOFANYIKA WAKALA WA MAABARA YA MKEMIA MKUU WA SERIKALI MAKAO MAKUU DAR ES SALAAM TAREHE 10 FEBRUARI 2016
Mhe. Balozi wa Japan nchini Tanzania.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa.
Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Mkemia Mkuu wa Serikali.
Watumishi wa Wakala.
Wanahabari.
Wageni Waalikwa.
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya njema. Pia, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kupata nafasi hii ya kutembelea Taasisi hii nyeti chini ya Wizara yangu pia, kuzindua rasmi cheti cha Ithibati (Accreditation) ISO 1705:2005 ambayo inaitambulisha Maabara hii kimataifa lakini pia kuwa Mgeni Rasmi kwenye hafla ya makabidhiano ya gari la huduma za dharura (Ambulance) kwa kituo cha kuratibu matukio ya sumu nchini kwa ajili ya Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Wageni Waalikwa,
Serikali inatambua umuhimu na unyeti wa majukumu yanayotekelezwa na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika kulinda afya, usalama wa watu na mazingira na hivyo kuleta utengamano katika jamii. Hali hii inawezekana kutokana na Wakala kutekeleza majukumu iliyonayo Wakala ya ya Kisheria yanayohusu uchunguzi wa kimaabara na kutoa ushauri wa kitaalamu unaosaidia mamlaka nyingine kutoa maamuzi ambayo hupelekea utoaji wa haki katika vyombo vya Kisheria. Ili Taasisi hii iendelee kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi, uwepo wa miundo mbinu kama vile vifaa ikiwemo mitambo, vitendea kazi kama vile magari na majengo bora ni suala ambalo halina budi kupewa kipaumbele.
Wageni Waalikwa,
Kwa taarifa niliyonayo, Taasisi hii ilianzishwa miaka 120 iliyopita (1895), umri ambao unaifanya kuwa taasisi kongwe zaidi na iliyojijengea sifa na weledi mkubwa hapa nchini. Katika kuendeleza sifa na weledi huo, Serikali kupitia Wizara yangu imekuwa ikifanya jitihada za kuboresha huduma za Wakala kulingana na uwezo uliopo ili kuhakikisha kuwa Wakala unaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Baadhi ya jitahada hizo ni pamoja na, kuanzisha Maabara za Kanda ili kusogeza huduma karibu na wananchi na kuendeleza ujenzi na ukarabati wa majengo ya Wakala. Wizara itaendelea na jitihada hizi ikiwa ni pamoja na kuthamini michango na misaada ya nchi wahisani na rafiki.
Wageni Waaalikwa,
Kama nilivyoeleza hapo awali na vile ambavyo sote tunajua umuhimu wa Taasisi hii, suala la kufanya uchunguzi wa sampuli zinazohusiana na makosa ya jinai kama vile, dawa za kulevya, utambuzi wa sumu, watu wanaojihusisha na uhalifu, utambuzi wa vinasaba vya watu, utambuzi wa watu waliopotea wakati wa majanga kama vile moto, kuanguka kwa majengo, mafuriko na ajali mbalimbali ni baadhi ya mambo nyeti yanayofanywa na taasisi hii muhimu.
Wageni Waalikwa,
Baada ya Maabara hii kupata ithibati (Accreditation) zinazoitambulisha kimataifa, napenda kusema kuwa Wizara yangu itaendelea kuimarisha Maabara hii ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaid. Aidha, naiomba jamii na Taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi kuendelea kuiamini Maabara hii, kushirikiana nayo na kuitumia vema ili iweze kuihudumia kwa kulinda afya na mazingira yake.
Wageni Waalikwa,
Katika ulimwengu wa sasa ambapo matumizi ya kemikali zenye sumu kwenye shughuli za kila siku za mwanadamu ni makubwa, suala la kuwa na kituo cha kitaifa chenye kuratibu matukio hayo kwa lengo la kulinda afya za watu na mazingira halina budi kupewa kipaumbele. Wizara imeongeza jukumu kwa Wakala la kuanzisha Kituo cha kuratibu matukio ya sumu nchini hapa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kutokana na uwezo na weledi wa taasisi hii na watumishi wake.
Hivyo, Serikali kuanzisha kituo hiki cha kitaifa kuratibu masuala ya sumu ni mojawapo ya jitihada za kukabiliana na madhara yanayosababishwa na sumu ili kulinda afya za wananchi. Natambua kuwa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imekuwa ukifanya kazi kubwa ya kubainisha na kutoa majibu juu ya sumu mbalimbali zinazotumika kudhuru watu na siku hizi hadi wanyama ambapo imekuwa ikipelekea hata wengine kupoteza maisha.
Hivyo kituo hiki kitaifa ni kitovu cha kukusanya taarifa husika kwa kuanza na zile zinazotokana na kazi za Wakala kwenye eneo hilo na pia taarifa za matukio ya sumu kutoka maeneo mengine zikiwamo hospitali ili mwisho wa siku tuwe na taarifa za matukio ya sumu ya kila namna kwa lengo la kusaidia jamii kwa kutoka huduma za dharura haraka inavyowezekana.
Mambo mengine muhimu ambayo Wizara yangu itaendelea kushughulikia ni pamoja na kudhibiti unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto na jamii kwa ujumla pia mauaji ya Albino na vikongwe,kwa kutumia ushahidi unaotokana na vipimo vya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Wageni Waalikwa,
Napenda kutumia nafasi hii tena kuipongeza Serikali ya Japan kupitia Taasisi ya “Japanese Fire Fighters” ambao wametoa Msada wa gari hili. Wizara kwa kutambua umuhimu wa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu Serikali na pia umuhimu wa kituo hiki kwa Serikali na jamii kwa ujumla, itaendelea kuuwezesha Wakala kutimiza majukumu yake kadri itakavyohitajika.
Wageni Waalikwa,
Natambua kuwa Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali umekuwa ukiendesha shughuli zake chini ya Sheria ya Wakala za Serikali ya mwaka 1997. Pia Wakala umekuwa ukisimamia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Kemikali za Viwandani na Majumbani Namba 3 ya mwaka 2003 na Sheria ya Udhibiti wa Teknolojia ya Vinasaba vya Binadamu ya mwaka 2009.
Kutokana na kupanuka kwa majukumu ambayo Wakala inapaswa kuyatekeleza na kuwa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ndiyo Maabara ya Rufaa ya Kitaifa, Serikali imepeleka Muswada Bungeni wa kutungwa kwa Sheria itakayoainisha moja kwa moja majukumu na mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Kukamilika kwa Sheria hii kutaipa Wakala mamlaka ya Kisheria katika kufanya kazi na kutekeleza majukumu yake kwa uhakika na ufanisi.
Wageni Waalikwa,
Kama nilivyoeleza hapo awali, Wakala pamoja na majukumu ya uchunguzi wa kimaabara, inasimamia utekelezaji wa Sheria za Vinasaba vya Binadamu Namba 8 ya mwaka 2009. Katika utekelezaji wa Sheria hii, Sheria inamuelekeza Mkemia Mkuu wa Serikali kuanzisha na kuratibu. Kanzidata (Database) ya Watanzania wote. Suala hili likikamilika litakuwa na manufaa sana katika kukabiliana na uhalifu na wahalifu hasa wale wanaojirudia kwenye kufanya uhalifu, watoto walio katika mazingira magumu, masuala ya majanga, ambapo itakuwa rahisi kuwatambua wazazi wao pamoja na masuala mengine yanayohusiana na utambuzi wa mtu binafsi. Katika kufanikisha suala hili, Wizara yangu itahakikisha kuwa inaiwezesha na kuijengea uwezo Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Wageni Waalikwa,
Kama nilivyoeleza hapo awali, shughuli yetu ya leo pamoja na maekelezo niliyoyatoa ni:
Kukabidhiana gari la huduma za dharura (Ambulance) kwa ajili ya Kituo cha Kitaifa cha Kuratibu Matukio ya Sumu (National Poison Control Centre). Ni matumaini yangu kuwa, baada ya makabidhiano ya gari hili kutaleta hamasa kwa upande wa Wakala na wadau wengine katika kukabiliana na matukio ya sumu hapa nchini.
Kuzindua rasmi cheti cha Ithibati (Accreditation) ISO 1705:2005 ambayo inaitambulisha Maabara hii kimataifa.
Baada ya kusema hayo, sasa natamka kuwa:
Gari la huduma za dharura (Ambulance) kwa ajili ya Kituo cha Kitaifa cha Kuratibu Matukio ya Sumu kutoka Serikali ya Japan limekabidhiwa rasmi kwa ajili ya kazi ya kituo.
Cheti cha Ithibati (Accreditation) ISO 1705:2005 imezinduliwa rasmi.
Asanteni kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment