Pages

Friday, February 5, 2016

Mtatiro Julius Amtaja Anatropia Theonest kama Kikwazo cha UKAWA kusindwa Segelea na Uwongo wake Bungeni.

KILICHOTUKOSESHA UBUNGE WA SEGEREA KISIFUKULIWE TENA!

Na. Mtatiro Julius

Ndugu Zangu,

Nilidhani suala la matokeo ya UBUNGE jimbo la Segerea kwenye uchaguzi wa Oktoba 25, 2015 limeshafungwa? Kumbe bado liko “ONLINE” na “LIVE” na leo (Jumatano, 03 Februari 2015) nimemsikia ndugu yangu Anatropia Theonest (MB) akilitolea ufafanuzi mwingine na “kujaribu” kuilaumu tume kwa makosa ya hovyo la kurejesha jina lake kwenye “karatasi ya kupigia kura”! Anatropia anasema “UONGO” na mimi hapa leo ntasema UKWELI! Akiendeleza mjadala huu ntasema makubwa zaidi ambayo siwezi kuyasema leo, yapo mengi tu! Nataka Mjadala huu ufungwe, kwa sababu amelisema BUNGENI na mimi si mbunge ninayo FORUM ya kueleza ukweli hapa! (MAELEZO NI MAREFU NA YAKINA!).

Kwanza, mimi na Anatropia sote kwa pamoja tulipitishwa na vyama vyetu kuwa wagombea ubunge wa jimbo la Segerea (siwezi kuongelea STATUS ya kupitishwa kwake ndani ya chama chake kwa sababu ina MENGI yasiyonihusu). Tarehe ya mwisho ya urudishaji fomu za serikali ilikaribia wakati jimbo la SEGEREA halijaamuliwa ndani ya UKAWA, vyama vyetu vikatuelekeza sote tuchukue fomu. Tukachukua na kurejesha kisha tukateuliwa na TUME YA UCHAGUZI kuwa wagombea halali wa kila chama.

Tarehe 29 Agosti 2015 kwenye Mkutano wa Uzinduzi wa Kampeni za UKAWA pale JANGWANI, wakati wagombe wa DSM wanatambulishwa - kwa jimbo la Segerea tuliitwa mimi na Anatropia, Mwenyekiti Mbowe akaeleza hadharani kuwa tunatambulishwa wawili kwa hatua ile lakini baada ya siku mbili UKAWA itakuwa imeamua jimbo linabakizwa kwenye chama gani kati ya CUF na CHADEMA na Mbowe akasisitiza kuwa maamuzi yatakayotolewa na UKAWA yatapaswa kufuatwa na pande zote kama yalivyo.

Kwa sababu nimezoea kufanya siasa za “UAMINIFU na USTAARABU” niliwajibika kuandika kwenye ukurasa wangu wa FACEBOOK kwamba ntapokea maamuzi yoyote na nikasisitiza ikiwa atakayepewa jimbo ni mwenzangu ntampa ushirikiano wote na ikiwezekana hata kuwa MENEJA WAKE wa kampeni (Nyote mnakumbuka). Sikuwa na kinyongo hata kidogo!

Tarehe 31 Agosti 2015 viongozi wakuu wa UKAWA walifanya mkutano na vyombo vya habari na kumaliza utata wa “majimbo viporo”, jimbo la Segerea likawekwa chini ya CUF na mimi kuwa mgombea rasmi. Mwenzangu alipojua maamuzi hayo AKAYAPUUZA na kuita vyombo vya habari, akaeleza kuwa yeye ndiye mgombea halali na kuwa atapambana na vyama vyote kwenye kampeni (bila kujali kuwa maamuzi yameshafanyika)! Waandishi walipombana kuwa “wamehudhuria PRESS CONFERENCE ya UKAWA iliyotangaza jimbo kuachiwa CUF kwenye mkutano huo na vyombo vya habari, akasisitiza kuwa yeye hafanyii kazi habari za kwenye MAGAZETI na tena akasema IKIWA atapewa barua rasmi na CHAMA CHAKE, basi atafuata maamuzi hayo – vinginevyo akasisitiza anaendela kujipanga kuzindua kampeni!

Katibu Mkuu wa CHADEMA akamuandikia barua mwanzoni mwa mwezi Septemba kumjulisha kuwa jimbo la Segerea limeachwa chini ya CUF na mgombea ni JULIUS MTATIRO. Baada ya kupokea barua hiyo Anatropia akaniandikia ujumbe mfupi (ninao kwa kumbukumbu na niliwahi kuuweka ONLINE) akinijulisha kuwa alitaka “viongozi wa juu wafuate taratibu na kumuandikia rasmi” akaliweka sawa na kuniambia “ntaungana nawe kuiondoa CCM Segerea, ntakuunga mkono”, hii ilikuwa tarehe 02 Septemba.

Siku mbili baadaye, (tarehe 04 Septemba) nikaandika taarifa ya kumpongeza Anatropia kwa kupokea na kukubali maelekezo na kunithibitishia kuwa amekubali kufuata maelekezo na maamuzi ya UKAWA, taarifa ile niliipa kichwa cha “A Woman of My Day – (Mwanamke wa Siku Yangu)”. Siku hiyo hiyo jioni (tarehe 04 Septemba) nikaletewa taarifa kuwa Anatropia amebadili maamuzi yake na kwamba anaendelea na uzinduzi wa kampeni (mtoa taarifa aliyehudhuria kikao cha Anatropia na watu wanaomuunga mkono ndani ya chama chake).

Kuona hivyo nikamtumia ujumbe kumuuliza kulikoni “uendelee na kampeni” wakati barua umeshapokea na maelekezo umeyakiri? Anatropia akaniambia walionipa taarifa hizo ni WAONGO na WACHONGANISHI, akasisitiza kuwa yeye hana nia na haendelei na kampeni (Wakati huo mimi nilishapanga kuzindua kampeni tarehe 06 Septemba 2015). Baadaye nikamsikia anahojiwa na redio moja akiwa amebadilisha msimamo KWA MARA YA PILI akidai hakubaliani na uamuzi huo kwa sababu yeye amelijenga sana jimbo la Segerea na tena akisisitiza kuwa chama chake (CHADEMA) ndicho kilistahili kuachiwa jimbo – akaendelea kuapa kuwa anazindua kampeni zake. Nikastaajabu sana! mtu unamuuliza anakuhakikishia hivi halafu redioni anasema VILE!

Tarehe 05 Septemba (siku ya Jumamosi) majira ya USIKU, magari ya Matangazo ya Anatropia yalianza kazi jimboni, kutangaza uzinduzi wake, yakaendelea hadi kesho yake (tarehe 06 – Jumapili) nadhani aliamua kuzindua siku hiyo hiyo ili atuharibie. Tuliwajulisha viongozi wa juu hali ile lakini hawakuwa na maamuzi zaidi, mapambano yakabaki ndani ya JIMBO. Jambo hili nililitolea taarifa kwa umma kupitia kichwa cha habari “HUJUMA ZA UKAWA JIMBO LA SEGEREA” – nilitoa taarifa hii usiku wa tarehe 05 Septemba.

Tarehe 06 Septemba ilipotimu mimi nikaelekea viwanja vya Vingunguti kuzindua kampeni (nikiungwa mkono na Viongozi wa CHADEMA na CUF wa wilaya na kata zote na madiwani wote – isipokuwa viongozi wachache wa kata ya Liwiti). Yeye Anatropia akaendelea na uzinduzi wake katika viwanja vya Shule ya Msingi Liwiti. Bahati nzuri wananchi walishaamua kuhudhuria uzinduzi wetu kule Vingunguti, hata hivyo Anatropia aliendelea na mkutano wake akajitangaza kama mgombea halali wa UKAWA na akanadiwa.

IKUMBUKWE; Nyakati zote hizi tokea niteuliwe rasmi na UKAWA nilikuwa nampa wito wa KUOMBA KUONANA kila mara bila mafanikio, kila nikimuomba tuonane anakwepa! (Ninazo meseji zote za majibu yake nilipomuomba tuonane)!

Baada ya uzinduzi wangu mimi na madiwani wote 13 tulianza kazi kubwa ya kunadi sera za UKAWA, Anatropia aliendelea na vikao visivyo rasmi vya NDANI kujiombea kura hasa baada ya baadhi ya viongozi wa juu wa chama chake kumuonya kwa tukio la uzinduzi wa kampeni kinyume na maelekezo ya UKAWA. Baadaye akapata mbinyo wa pili kwamba ni lazima akatoe jina lake NEC ili chama chake kimfikirie kwenye ujazaji wa fomu za Ubunge wa Viti Maalum (Taarifa nilizopewa na kiongozi wa juu wa CHADEMA), ndipo Anatropia akaenda kujitoa LAKINI akafanya makusudi makuu, HAKUTIMIZA MASHARTI YA KUJITOA!

Anatropia alifanya jaribio la kujitoa kugombea Segerea tarehe 14 Septemba 2015 kwa kuwasilisha kwa msimamizi wa Uchaguzi KIAPO CHA MAHAKAMA kilichosainiwa tarehe hiyo hiyo. Hakuwasilisha BARUA YA KUJITOA kwa Msimamizi wa Uchaguzi wala kuonesha kuwa amepeleka nakala ya kujitoa kwake kwa Katibu wa Tawi la Chama lililomdhamini kama inavyoelekezwa na kifungu cha 5.10 cha Maelekezo kwa Vyama vya Siasa na Wagombea juu ya “NAMNA YA KUJITOA” (Alikuwa anajua anachokifanya), kwa bahati mbaya mimi sikujua ujanja alioufanya.

Siku tano baadaye (tarehe 19 Septemba) nilipigiwa simu na mtu mwenye nia njemakutoka kwenye Taasisi Muhimu iliyo karibu na NEC akinijulisha kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haitaondoa jina la Anatropia kwa sababu hakutimiza masharti ya kujitoa na kwamba hakuwasilisha BARUA YA KUJITOA. Ili kujinusuru na hali hiyo nikashauriwa kuwa haraka sana Anatropia apelike barua TUME kabla ya tarehe 25 Septemba ambapo tume watakuwa wanaelekeza UCHAPISHAJI WA KARATASI za kura uanze. Nikashangaa sana (MJINI SHULE!).

Haraka sana nilimtafuta Anatropia nikazikosa simu zake hewani, nilipowauliza viongozi wenzake wakaniambia yuko MIKOANI anasaidia kampeni za huko, baadaye nikatuma ujumbe mfupi kwenye simu zake zote mbili (AIRTEL na TIGO) ujumbe ukapokelewa haukujibiwa. Ikanipasa niwasiliane haraka (kwa SIMU) na baadhi ya viongozi wa juu wa CHADEMA (Makao Makuu)akiwemo Kaimu Katibu Mkuu wa wakati huo JULIUS MWITA ili wamjulishe kuwa tume haijapokea BARUA YAKE YA KUJITOA na kwamba haiwezi kufanyia kazi KIAPO peke yake kwani ni kinyume na mwongozo wa kujitoa. Julius Mwita akanihakikishia kuwa watawasiliana na viongozi wa kanda na wengine ili wamsisitize Anatropia mwenyewe achukue hatua na baadaye Julius Mwita alinipa Mrejesho kuwa Anatropia ameshaelezwa achukue hatua za haraka.

Kwenye mchakato huu pia nilichukua hatua ya kuwasiliana na Mabina (Mratibu wa Kanda wa CHADEMA na kumjulisha hatari inayotukabili Segerea na nikamuomba amsisitize Anatropia kwa sababu hajibu simu zangu). Mabina akanijibu kwa ujumbe mfupi (ninao) kuwa wao (Viongozi wa Kanda) wamekwishasawazisha hali ya Segerea na Anatropia ameshajitoa kwa hiyo mambo yaliyobaki yanapaswa kushughulikiwa na MIMI na ANATROPIA. Nikamuelewesha Ndugu. Mabina kuwa mimi sina Mamlaka ya Ki-Uongozi juu ya Anatropia lakini akaonesha kutoliingilia suala hili.

Tarehe 01 Oktoba NEC ikatoa karatasi za mfano ili wagombea na vyama wakague na kutoa taarifa ikiwa majina ya wagombea, nembo za vyama, picha za wagombea au kingine chochote kimekosewa kwenye fomu zile – kwenye karatasi ya Ubunge wa Segerea, Jina na Picha ya Anatropia Theonest vilijitokeza. Nilipompigia simu Mkurugenzi wa Uchaguzi wa wilaya ya Ilala akanieleza kuwa Anatropia hakutimiza masharti ya kujitoa ambayo yameelezwa kwa wazi kabisa kwenye muongozo, akaniambia yeye pia hana matumaini kama tume itamtoa tena kwani huwenda karatasi zimeanza kuchapishwa kwani walihakiki MAJINA na kila kitu kwa uhakika.

Kati ya tarehe 8 hadi 10 Oktoba 2015 nikapigiwa simu na Bi. Anatropia, akiwa nje ya DSM akanijulisha kuwa “INAMPASA AREJEE DSM HARAKA” ili tuonane na kuchukua hatua za pamoja ili NEC iondoe jina lake. Nikamwambia “Mbona nimekutafuta sana hewani na nimekutumia ujumbe tangu tarehe 19 Septemba ukawa haujibu chochote? Na hata viongozi wako wanasema wanajaribu kukufikia bila mafanikio?”.  Anatropia akakana kupokea ujumbe wangu wowote au wa kiongozi yeyote akajitetea kuwa yeye ameiona hatari hiyo baada ya karatasi ya kupigia kura ya SEGEREA kubandikwa kwenye mitandao ya kijamii ndipo akaona anitafute. Nikamkubalia tuonane haraka na akaniambia angekuwa Dsm.

Tarehe 09 na 10 Oktoba 2015 nikakutana na Bi. Anatropia majira ya jioni eneo la Mwenge wilaya ya Kinondoni, yeye alikuwa na wanachama wengine wawili wa CHADEMA na mimi nikiwa na msaidizi wangu anayenisaidia kwenye eneo la utafiti. Tulifanya mazungumzo kwa saa nne, mkazo ukiwa namna gani anawajibika kupeleka barua ya kujitoa inayoonesha kuwa amepeleka nakala kwenye tawi lake pamoja na KIAPO CHA MAHAKAMA kipya!

Mimi binafsi nilimuelezea Anatropia wasiwasi wangu kuhusu jina lake kuondolewa kwani tarehe aliyokuwa anakusudia kujitoa rasmi kwa kukamilisha masharti ilikuwa ni siku 12 tu kabla ya uchaguzi. Ni Tume gani ya Uchaguzi ambayo inakuwa haijachapisha karatasi za wapiga kura kwenye jimbo lenye wapiga kura zaidi ya laki tatu? Anatropia alinitoa wasiwasi na kunipa taarifa zaidi kuwa jina lake litaondolewa tu hata dakika za mwisho kwani wapo wanasheria walioko karibu na mume wake ambao wamemhakikishia hivyo. Nikampa ushirikiano wote uliohitajika na tarehe 12 Oktoba (Siku 10 za kazi kabla ya siku ya uchaguzi) ndipo AKAKAMILISHA MASHARTI YA KUJITOA RASMI kwa kuwasilisha vielelezo vilivyokamilika kwa msimamizi wa Uchaguzi.

Taarifa nilizonazo zinaonesha kuwa tarehe 14 Oktoba (siku 8 kabla ya uchaguzi) msimamizi wa uchaguzi wa Ilala aliwasilisha nyaraka mpya za Anatropia kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (SIKU 8 KABLA YA SIKU KUPIGA KURA). Kwa nini leo hii Anatropia aanze kusimama bungeni kuilaumu NEC kwa jambo ambalo “amelilea yeye mwenyewe” kwa siku 50 nzima?

Kwa nini akumbuke kwenda kukamilisha masharti wiki moja kabla ya uchaguzi? Kwamba NEC ingelikuwa na kazi kiasi gani ya kuanza kuchapisha mamilioni ya karatasi mpya za kupigia kura kwa ajili ya wagombea waliojitoa kwenye uchaguzi wiki ya mwisho? Anatropia ni msomi wa ngazi ya Shahada ya Uzamili, jambo hili lingetendekaje? Mfano mwingine ni vipi ikiwa na mgombea urais anajitoa wiki moja kabla ya uchaguzi? Alikuwa wapi kufanya hivyo tangu ateuliwe? Hii ni ajabu.

NEC ILITIMIZA WAJIBU WAKE?

Ndiyo, kwa mtizamo wangu NEC kwenye jambo hili ilitimiza wajibu wake na kuna ushahidi. Mathalani, aliyekuwa mgombea wa CHADEMA jimbo la TEMEKE Ndugu Mwakyembe, naye alichukua fomu na akateuliwa na NEC kuwa mgombea wa CHADEMA, chama chake kilipomuelekeza akajitoe ili kumuachia mgombea wa CUF, Abdallah Mtolea, Mwakyembe alienda kufanya hivyo tarehe 04 Septemba 2015 (akawasilisha BARUA YA KUJITOA pamoja na KIAPO), NEC Makao makuu ilipokea taarifa za kujitoa kwa Mwakyembe tarehe 07 Septemba 2015 (siku ya Jumatatu) na kwenye karatasi za mfano za kupigia kura ya Ubunge wa Temeke zilizotoka tarehe 01 Oktoba 2015, NEC ilikuwa imeondoa jina la Mgombea wa CHADEMA wa TEMEKE na siku ya Oktoba 25 haikulirejesha.

KWA NINI MGOMBEA WA CHADEMA JIMBO LA TEMEKE ALIFANIKIWA KUJITOA HUKU WA SEGEREA AKISHINDWA?

Ni kwa sababu Mgombea wa CHADEMA wa Temeke hakuwa MSUMBUFU wala MBISHI na alijua wajibu wake mapema, hakuwa na mipango binafsi. Pili, alifanya hivyo kwa kutimiza MASHARTI ya mwongozo wa kujitoa kwa kuwasilisha nyaraka mbili (BARUA NA KIAPO) na tatu alijitoa kwa wakati -  muda ambao tume ilikuwa haijafikia hatua za mwisho za kuhakiki na kuagiza uchapishaji wa karatasi uanze.

Segerea tulifeli kwa sababu KWANZA Mgombea wa CHADEMA wa Segerea Bi. Anatropia Theonest alikuwa MSUMBUFU, MBISHI na MWENYE MIPANGO MINGI ISIYOJULIKANA (na wala sihitaji kuieleza hapa). PILI tulifeli kwa sababu Anatropia alianza mchakato wa kujitoa tarehe 14 Septemba (bila kukamilisha masharti ya kujitoa) na akaumalizia tarehe 12 Oktoba, na ndio maana wanasheria kadhaa walinisisitiza kuwa NEC isingelikuwa na uwezo wa KUFUTA uchapishaji wa karatasi ili ianze upya kwa ajili ya mgombea aliyeamua kujitoa wiki mbili za mwisho.


SIKU YA UCHAGUZI OKTOBA 25 -  NINI KILIJIRI?

Siku ya Oktoba 25, 2015 mambo makubwa matatu yalijitokeza;

Mosi, Anatropia (BILA AIBU) alipita kwenye vituo vya kupigia kura akijinadi kwa wapiga kura kuwa HAJAJITOA na kwamba yeye ndiye anastahili kupigiwa kura na siyo MIMI. Niliitwa haraka katika mtaa wa Kisiwani ulioko Tabata kwenye kituo cha kupigia kura ambapo alikuwa amewakusanya vijana na kina mama akisisitiza wampigie kura, wengi walishangazwa na hali ile. Nilipopaki Gari eneo la jirani na kituo cha kupigia kura yeye na Mumewe wakaondoka haraka eneo lile. Mchezo huu wa kujinadi aliuendeleza kwenye vituo na kata zingine kadhaa.

Pili, bila aibu – Bi. Anatropia Theonest aliweka vijana kwenye vituo vya kupigia kura katika kila kata, wakiwa ndani ya mistari wanasisitiza UBUNGE NA URAIS kura zipigwe CHADEMA, tulikuja kuushtukia mchezo huu saa 4 asubuhi kwamba kuna kampeni kali inaendelea vituoni ikifanywa na vijana wasioondoka kwenye mistari kuwa UBUNGE apigiwe Anatropia wa CHADEMA. Ilipofika saa 7 mchana viongozi na madiwani wa kata 11 kati ya 13 za Segerea wa vyama vya CHADEMA na CUF waliripoti kwenye kituo chetu (NGOME YA JIMBO) juu ya mwenendo wa kampeni hiyo MBAYA DHIDI YA USHINDI WA UKAWA.

Tatu, bila aibu – Bi. Anatropia alituma vikosi vya vijana wake wakamrekodie matokeo yanayobandikwa nje vituoni huku pia vikosi hivyo vikitafuta mawakala wa CHADEMA waliokuwa vituoni kwa njia za simu kwa ajili ya kuwapa taarifa za matokeo yake. Kwa hiyo alifanya kazi kubwa ya kusaka ushindi akiamini kuwa kwa sababu nembo ya CHADEMA ni maarufu na wapiga kura wengi huyumba na huenda vituoni bila kujua wanamchagua nani – kwamba wangeliipigia CHADEMA kura za kutosha ikiwa wangeliambiwa na kusisitizwa dakika za mwisho wakafanye hivyo. Mmoja wa watu wake waliokuwa wanaongoza kurekodi matokeo yake vituoni alithibitisha kuwa Anatropia alikuwa anaamini kuwa huwenda angeshinda uchaguzi wa Oktoba 25 kwa sababu ya kuuzika kwa nembo ya “VIDOLE VIWILI”.

Matukio haya ya tarehe 25 Oktoba 2015 ni uthibitisho mwingine mkubwa kuwa Segerea ilijiendea kwenye uchaguzi wa Ubunge kukiwa na HUJUMA KUU na ZISIZOMITHILIKA.

Matokeo yalipokuja kutangazwa CCM ilishinda Ubunge wa Jimbo la Segerea kwa kura takribani 100,000, mimi mgombea kupitia CUF nikapata kura takribani 80,000 na Anatropia wa CHADEMA akapata takribani kura 50,000. Matokeo hayo yalikuwa na maana kuwa kura zangu na za Anatropia zingeipa UKAWA mbunge kwa ushindi wa zaidi ya kura 30,000 dhidi ya CCM. Hilo halikutokea!

Baada ya kulikosa jimbo la Segerea nilitoa taarifa kadhaa nikisihi kuwa Uchaguzi umekwisha na tunaye mbunge. Bahati nzuri Bi. Anatropia aliteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum na CHAMA chake (kwa kufuata vigezo vya chama) na kuna watu walitaka kuanza kuponda uteuzi huo, nilijitokeza hadharani nikasisitiza kuwa anayo haki kama mwanamke ndani ya CHADEMA na kama amefikisha vigezo kupewa ubunge na nilisisitiza hayo yasifungamanishwe na mimi kukosa ubunge.

Baadaye wanasheria walinisisitiza kuona haja ya kufungua kesi kupinga matokeo ya ubunge wa Segerea, nikawasiliana na Anatropia ili anikabidhi nyaraka za kujitoa kwake za tarehe 12 Oktoba 2015, akazipitishia kwa mwanasheria wa CHADEMA zikanifikia, nikakabidhi na kiapo chake cha terehe 14 Septemba 2015 na baada ya mapitio ya wanasheria wanne, watatu kati yao waliona huwenda NEC itatushinda mahakamani kwa hoja kisheria, kimantiki, kimaelekezo na kiuhalisia wa utendaji wa chombo hicho, baadaye nilimjulisha Anatropia kuwa hatutafungua kesi yoyote.

USHAURI WANGU KWA BI. ANATROPIA THEONEST;

Kwanza namshauri kuwa mara nyingine anapopata nafasi ya kuchangia ndani ya Bunge, aachane kabisa na UTOAJI WA MAELEZO ya uchaguzi wa Ubunge wa Segerea kwa sababu kila atakapoongelea jambo hilo sitasita kutoa ufafanuzi wa kile alichosema. Hivi sasa yeye ni mwakilishi wetu ni mbunge wetu, aongelee matatizo ya wana Segerea, wana Ilala na wana DSM – Mambo ya uchaguzi na yaliyotokea vilishapita na watu walishaanza kusahau, mimi nilishasamehe na inatosha kabisa! Asifukue MAKABURI KWA SABABU ANAWEZA KUKUTANA NA MAITI MBICHI!

Pili, Ikiwa Anatropia ataendelea kuongelea masuala ya Uchaguzi ulionikosesha ubunge wa Segerea kimakusudi bado ninayo mengi tu ya kuweka hadharani ikiwemo kuelezea UHUSIANO wake na Mgombea wa CCM Bi. Bonah Kalua wakati wa Kampeni na namna ambavyo TIMU YOTE ya Anatropia ilivyofanya kazi na Bonnah Kaluwa chini ya usimamizi wa ANATROPIA usiku na mchana. Haya ntayaeleza kwa TAARIFA na USHAHIDI wa meseji za makundi ya WHATSUP, SAUTI ZILIZOREKODIWA kwenye mikutano ya BONA KALUA na kundi la ANATROPIA. Napokaa kimya nisionekane mjinga!

Mwisho, Mbunge wetu Anatropia hajui madiwani 13 wamepatikanaje hapa Segerea, huwenda aliwahi kutoa mchango wa ujenzi wa UKAWA kabla ya kampeni lakini WAKATI WA KAMPENI yeye alikuwa mikoani (Jemedari anakikimbia kikosi chake wakati vita inaanza TENA AKIWA NI KATIBU WA JIMBO) – Aliwahi kujitokeza kuninadi kwenye mikutano miwili tu (Ule wa Lowassa na Ule wa Juma Duni Haji), nilimuona pia kwenye mkutano mmoja wa Diwani wa Kimanga, nikamsikia kwenye mikutano mingine miwili ya diwani wa Kipawa na mmoja wa diwani wa Bonyokwa.

Mimi na madiwani tumetembea usiku na mchana jimboni tumefanya mikutano takribani 170 na yeye hakuhudhuria hata saba (7) – tumefanya vikao vya ndani vya mbunge madiwani zaidi ya 200 na hakufika hata kwenye kikao kimoja – ndio kwanza alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha baadhi ya madiwani wa chama chake akiwemo Patrick Assenga wa kata ya Tabata hawapati ushindi (Ushahidi uko wazi sana).

Nataka kumalizia kwa kusema, kama kuna mtu alitukosesha jimbo la Segerea, Bi. Anatropia Theonest alichangia kwa asilimia 99 na NEC anayoilaumu bungeni ilichangia kwa asilimia 1. Kama ni mnyama alikuwa anachinjwa basi yeye ndiye alimshikilia na kumuelekeza KIBRA na NEC walipitisha tu kisu!

Napenda sana kumuomba mwana UKAWA huyu mwenzangu aongelee MATATIZO ya wananchi kama alivyofanya kwenye sehemu ya pili ya hotuba yake ya leo, HEBU ASIGUSIE MASUALA YA UCHAGUZI WA OKTOBA 25, 2015 na HEBU ASIWADANGANYE WANANCHI JUU YA KILICHOTOKEA SEGEREA!

Mtatiro Julius,
Segerea.
02 Februari 2016.

No comments:

Post a Comment