JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU (MB); WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, TAREHE 29 MACHI, 2016
Ndugu wanahabari,
Wizara yangu imejiwekea utaratibu wa kutoa taarifa kila wiki kwa umma kuhusu hali ya ugonjwa wa kipindupindu nchini pamoja na kueleza juhudi mbalimbali za kuudhibiti zinazoendelea kuchukuliwa. Ugonjwa wa kipindupindu umedumu hapa nchini kwa takribani miezi saba (7) sasa tangu uanze mnamo mwezi Agosti, 2015 ambapo hadi kufikia tarehe 27 Machi 2016, jumla ya watu 19,815 wameugua ugonjwa huo, na kati yao watu 312 wamepoteza maisha.
Takwimu za wiki iliyopita kuanzia tarehe 21 hadi 27 Machi 2016 zinaonyesha kuwa, kasi ya ugonjwa wa kipindupindu imepungua ambapo idadi ya wagonjwa wapya walioripotiwa wiki hiyo ni 685 ikilinganishwa na 738 wa wiki iliyotangulia. (Machi 14 hadi 20, 2016) ambapo ni punguzo kwa asilimia 7.2. Idadi ya vifo imepungua sana toka 16 wiki iliyotangulia hadi 4 wiki iliyopita, sawa na asilimia 75. Mikoa ambayo bado imeendelea kuripoti ugonjwa wa kipindupindu ni 13. Mikoa iliyopata wagonjwa wengi zaidi ni Kilimanjaro (162), Geita (97), Manyara (88), Mwanza (74) na Iringa (60).
Hadi sasa, mikoa ya Njombe na Ruvuma haijaripoti kuwa na mgonjwa wa Kipindupindu.
Ndugu wanahabari,
Wakati tunasubiri kipindi cha Masika kianze wakati wowote, tunaashiria ongezeko la ugonjwa ya Kipindupindu iwapo wananchi hawatazingatia kanuni za usafi binafsi na mazingira. Hivyo basi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea kusisitiza kuwa udhibiti wa ugonjwa wa Kipindupindu unahitaji juhudi kubwa zaidi ya wananchi na viongozi wa ngazi mbalimbali hususan wakati tunaelekea kipindi hiki cha masika.
Aidha Wizara inapenda kutoa pongezi kwa Mikoa na Wilaya zinazoendelea kutoa taarifa sahihi na kwa wakati pamoja na juhudi za kudhibiti ugonjwa huu. Ninaendelea kusisitiza kuwa ni lazima kwa Mikoa na Wilaya kutoa taarifa ya wagonjwa wapya wa Kipindupindu kwa kuzingatia mfumo wa ufuatiliaji wa magonjwa ujulikanao kama “Integrated Disease Surveillance and Response (IDSR)”, ambao unasimamiwa na Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya. Utoaji wa taarifa sahihi na kamili (ikiwa pamoja na linelist) kwa wakati utasaidia kuweka mikakati ya upesi ya kudhibiti ugonjwa huu usisambae kwa kasi na kuleta madhara zaidi. Hii pia inaambatana na uchukuaji wa sampuli za wagonjwa kwa vipimo kama mwongozo unavyosema ili kuweza kudhibiti ugonjwa huu kwa wakati muafaka.
Ndugu wanahabari,
Kufuatia tahadhari niliyotoa kwa mikoa yote nchini kwa Waganga Wakuu wa Mikoa kuhusu uwepo wa ugonjwa wa Homa ya Manjano nchini Angola na kuweka mipango thabiti ya utambuzi, wiki hii iliyopita, wataalam wetu waliweza kutambua wagonjwa wawili (2) ambao walionyesha kuwa na dalili za kutokwa damu katika sehemu za uwazi na kufariki dunia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Aidha vipimo vya wagonjwa hawa wawili vilichukuliwa na kudhibitishwa kuwa hawakuwa na ugonjwa wa Ebola au Homa ya Manjano. Taratibu za mazishi zilifuatwa kuzingatia miongozo ya Kitaifa. Hadi leo tarehe 29 Machi 2016, Wizara inafuatilia watu 55 waliokuwa karibu na wagonjwa hawa na hadi sasa hakuna mtu yeyote ambaye ameonyesha dalili kama za wagonjwa waliokwisha kufariki. Watu hawa watafuatiliwa kwa takribani siku 21 kama taratibu za magonjwa ya milipuko ya aina hii zinazoelekeza.
Ndugu wanahabari,
Nahimiza yafuatayo yazingatiwe katika kudhibiti magonjwa ya milipuko;
Utoaji wa taarifa mapema katika vituo vya kutolea huduma za afya pale wanapoona wagonjwa wana dalili za magonjwa ya milipuko
Kutilia mkazo usafi wa mazingira kwa ujumla
Watumishi wa afya waendeelee kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu na jinsi ya kujiepusha kupata maambukizi.
Ngazi mbalimbali ziendelee kuchukua tahadhari (Preparedness) kwa magonjwa haya.
Hitimisho
Wizara inaendelea kutoa wito kwa wadau wote katika ngazi zote kushirikiana kwa pamoja katika jitihada za kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu. Aidha, Wizara inaendelea kuwashukuru wataalamu wa sekta husika, Mashirika ya Kimataifa, Watumishi, Mikoa na Halmashauri pamoja waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla kwa kuendelea kushirikiana katika suala zima la kudhibiti ugonjwa wa Kipindupindu.
Asanteni sana
No comments:
Post a Comment