Huduma za CT Scan, MRI na Mammograph kupatikana Benjamin Mkapa Hospital, Dodoma
Dodoma. 28-02-2017
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mhe Ummy Mwalimu amewathibitishia wananchi wa kanda ya Kati wakiwemo watumishi wa umma wanaohamia mkoani Dodoma kuwa huduma zote za matibabu ya kibingwa sasa zitapatikana katika Hospitali ya Kisasa ya Benjamin Mkapa iliyopo UDOM - Dodoma.
Mhe Ummy ameyasema hayo leo wakati alipokagua ufungaji wa Vifaa vya kisasa katika Hospitali hiyo ikiwemo CT Scan, MRI, Mammograph na Digital X-ray mashines ambazo zimefungwa katika Hospitali hiyo. Mhe Ummy ameagiza kazi ya ufungaji na majaribio ikamilike haraka ili huduma zote muhimu zitolewe kwa ukamilifu kuanzia tarehe 1 April 2017
Akiongea mbele ya Waziri Ummy, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dr Chandika alieleza kuwa kazi ya ufungaji vifaa hivyo imekamilika na kesho tar 1 Machi wataalam wa vifaa wataviwasha kwa majaribio. Pia tayari wameshawaandikia Wataalam wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (Tanzania Atomic Energy Commission) kuja kukagua vifaa hivyo ili kujiridhisha endapo ufungaji wa vifaa hivyo umekidhi vigezo vya Tume hiyo.
Hata hivyo, Mkurugenzi alieleza kuwa Changamoto kubwa iliyopo sasa ni Watumishi. Akijibu hoja hiyo, aliahidi kufanya uhamisho wa ndani wa Wataalam kutoka Wizarani ili kuimarisha huduma katika Hospitali hii sambamba na kuendelea kuwasiliana na Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kupata watumishi wakutosha kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watumishi ya Hospitali hiyo.
Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyoko UDOM imefungwa vifaa vya uchunguzi vya Tiba vya kisasa ikiwemo MRI ambao ndio ya kisasa zaidi kupatikana eneo la ukanda wa Afrika Mashariki.
Kukamilika kwa Hospitali hii kutakuwa na mchango mkubwa sana kwa wananchi wa Mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Manyara na Iringa ambao wanalazimika kwenda umbali mrefu kufuata huduma za matibabu ya kibingwa hasa Dar es salaam.
-----
No comments:
Post a Comment