Pages

Wednesday, February 22, 2012

MAUAJI SONGEA

Mauaji Songea  Send to a friend
Wednesday, 22 February 2012 21:16 
Askari wa kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) mkoani Ruvuma wakiwa wamewakamata baadhi ya wananchi wakazi wa Lizabon ambao walikuwa wakifanya vurugu kwa kurusha mawe na kuchoma moto matairi barabarani jana wakati wa maandamano.Picha na Joyce Joliga
POLISI WAUA RAIA WANNE WAJERUHI 41
Waandishi Wetu
MJI wa Songea na viunga vyake jana ulikumbwa na machafuko makubwa yaliyofanya polisi waue watu wanne baada ya wananchi kuandamana wakipinga mauaji yanayodaiwa kuambatana na imani za kishirikina tangu Novemba mwaka jana.

Katika machafuko hayo watu wengine 41 walijeruhiwa, wawili wakiwa katika hali mbaya huku shughuli za kiuchumi na kijamii zikisimama kwa muda.

Hata hivyo, idadi hiyo ya vifo na majeruhi inatofautiana kati ya ile iliyotolewa na jeshi la polisi, uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Wakati polisi ikisema waliokufa ni wawili na majeruhi ni 10, uongozi wa hospitali ya mkoa umesema umepokea maiti nne na majeruhi 41 na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa inasema waliokufa ni wawili na majeruhi ni 20.

Tukio hilo la kwanza kutokea katika historia ya Mji wa Songea, lilitokana na hatua ya wananchi kuamua kuandamana kuelekea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuelezea kilio chao baada ya kuwepo kwa mauaji ya mara kwa mara ya raia tangu Novemba mwaka jana ambao baada ya kuuawa wamekuwa wakinyofolewa sehemu zao za siri.
Hadi jana, imeripotiwa kwamba watu tisa wameshapoteza maisha katika mazingira hayo kwa nyakati tofauti. Habari zilizopatikana mjini Songea zinasema kwamba mauaji hayo yanayohusishwa na imani za kishirikina yakidaiwa kufanywa na wachimba madini wa migodi iliyoko nchi jirani.
Maandamano na vurugu

Maandamano hayo yaliibuka baada ya jana asubuhi mtu mmoja wa kiume kukutwa amekufa kwa kukatwa mapanga eneo la Makarawe huku pia sehemu zake za siri zikiwa zimenyofolewa.

Baada ya kuuona mwili huo wa marehemu, umati wa watu ulianza kukusanyika na kuamua kuandamana wakisema kwa amani ili kuwasilisha kilio chao kwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Maandamano hayo yalivuta umati watu na mamia ya wananchi walijiunga na kuanza kutembea kwa miguu huku wengine wakiwa katika pikipiki maarufu kwa jina la 'Yeboyebo,' kuelekea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa zilizo jirani na Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Ruvuma.

Kadri wananchi hao walivyokuwa wakiendelea kuandamana, habari zilitapakaa mitaa mbalimbali na kuwafanya wananchi wengi zaidi kuungana nao, hali iliyowalazimu polisi nao kujipanga kuwazuia kwa kutumia mabomu ya mchozi.

Hata hivyo, wananchi walizidi kuongezeka wakipinga hatua hiyo ya polisi kuwazuia kufikisha ujumbe wao kwa Mkuu wa Mkoa. Katika hatua hiyo, ndipo vurugu zilipoanza kwani wakati polisi watumia mabomu ya kutoa machozi, baadhi ya waandamanaji walianza kuvurumisha mawe hali iliyowafanya watu kukimbia huku na huko.

Vurugu zilishika kasi hali iliyowafanya polisi kuanza kutumia risasi za moto katika kile ilichodai baadaye kwamba ni katika kujilinda na ndipo vifo hivyo vilipotokea na idadi hiyo kubwa ya majeruhi. Hata hivyo, haikuelezwa mara moja kama miongoni mwa majeruhi hao alikuwamo askari polisi.

Baada ya mauaji hayo, vurugu zilizidi kusambaa katika mitaa mbalimbali ya Mji wa Songea huku wananchi wakianza kurusha mawe kuelekea Kituo Kikuu cha Polisi. Lakini wengine waliendelea kupigia kelele madai yao ya msingi huku wakilishutumu jeshi hilo kwa kushindwa kudhibiti mauaji hayo kwa muda mrefu.
Vurugu hizo zilisababisha ofisi za Serikali na taasisi binafsi mkoani Ruvuma kufungwa kwa muda yakiwemo maduka, masoko na huduma za kifedha katika mabenki kusimama kwa muda.

Huduma za usafiri katika stendi kuu ya mabasi yaendayo mikoani nazo zilisimama, huku madereva wa mabasi na abiria wakikimbia kujificha kuepuka mabomu ya machozi na risasi za moto zilizokuwa zikipigwa hewani.

Pia huduma za matibabu katika Hospitali ya Mkoa zilisimama kwa muda baada ya walinzi wa hospitali hiyo kufunga lango kuu, kutokana na wananchi wengi kukimbilia huko wakikimbia mabomu.

Habari zaidi kutoka eneo la tukio zimeeleza kuwa maandamano hayo yalichochewa na taarifa ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa juzi kwamba mauaji hayo yanahusiana na masuala ya kipenzi. Ilielezwa kwamba wananchi walikuja juu wakipinga madai hayo ambayo pia yaliripotiwa jana na gazeti hili.

Utetezi wa Polisi
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Michael Kamhanda alisema polisi ililazimika kutumia nguvu ya ziada baada ya wananchi kukaidi amri ya kuwataka watawanyike.
Alidai waliopoteza maisha kutokana na vurugu hizo ni wawili na majeruhi 10 akisema watu hao walifariki dunia kwa kupigwa risasi za moto baada ya kukaidi amri ya polisi kutawanyika.

“Tulilazimika kutumia risasi za moto baada ya hawa vijana kukataa kutii amri ya polisi,” alisisitiza Kamanda Kamhanda.
Kamanda Kamhanda alisema watu 56 wamekamatwa kwa ajili ya kuhojiwa kutokana na tukio hilo.
Kamanda Kamhanda alisema ingawa bado uchunguzi unaendelea, taarifa za awali zinaonyesha kuwa chanzo cha vurugu hizo ni imani za kishirikina na siasa. Hata hivyo, hakufafanua ushirikina wala siasa zilivyochochea maandamano hayo.
RC atoa amri ya kutombea usiku

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu alisema vurugu hizo zilizodumu kwa saa sita zimesababisha uharibifu mkubwa wa mali na kuhatarisha usalama katika mji huo.

Kutokana na hali hiyo, alitoa amri ya kutotembea usiku akisema msako wa kuwasaka watuhumiwa wa maandamano hayo bado unaendelea.

“Kama watakuwa hawana shughuli za muhimu wabakie tu majumbani mwao ili kuepuka usumbufu. Polisi itaendelea kuwasaka watuhumiwa usiku ili kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria,” alisema.

Mkuu huyo wa Mkoa alitoa kauli hiyo baada ya kuongoza kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kilichoitishwa ghafla kutokana na machafuko hayo makubwa.

Hospitalini
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma, Dk Benedicto Ngaiza alisema kati ya watu nne waliokufa na miili yao kupokewa, miwili ilikuwa na majeraha ya risasi na majeruhi wawili  kati ya hao 41, walipelekwa chumba cha upasuaji kwa kuwa walikuwa na majeraha ya risasi pia.
“Hii miili ilikuja kwa awamu, mara ya kwanza ulikuja mmoja na mara ya pili ikaja mitatu. Yote ililetwa kwa magari ya polisi,” alisema Dk Ngaiza na kuongeza:
“Katika hii mitatu iliyokuja kwa pamoja miwili ilikuwa na majeraha ya risasi na mmoja alikuwa ni kijana aliyegonga mti na pikipiki akikimbia vurugu hizo. Kati ya majeruhi hao wawili wamepelekwa chumba cha upasuaji shida yao pia ni majeraha ya risasi.”

Kisa cha maandamano
Tangu Novemba mwaka jana, kumekuwa na matukio ya mauaji katika Mji wa Songea kwa nyakati tofauti hadi sasa ambayo yamekuwa yakitokea katika mazingira ya kutatanisha huku miili ya marehemu ikiwa imejeruhiwa kwa kukatwa mapanga, shoka au marungu na kunyofolewa sehemu za siri.

Hali imekuwa mbaya zaidi mwishoni mwa wiki ambako kwa siku tatu mfululizo mauaji hayo yalitokea hali iliyochochea hasira za wananchi hadi kufikia uamuzi wa kuandamana.

Watuhumiwa wanne wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo wanashikiliwa na polisi. Watuhumiwa ni Johari Kassim (16), Onesmo Hinju (14), Samason Haule (22) na Mussa Fuala (20) wote wakazi wa Mtaa wa Lizaboni mjini Songea.

Kilio chasikika

Kamati hiyo ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa imewataka watendaji na wenyeviti wa mitaa na mabalozi kuanzisha ulinzi wa doria za usiku katika maeneo yao kuanzia sasa na kwamba ambaye tukio la mauaji hayo ya kishirikina yatatokea katika mtaa wake atakamatwa na kuchukuliwa hatua.

Katika kikao cha kamati hiyo kilichowashirikisha pia viongozi hao, imeamuliwa pia kwamba watendaji hao wa ngazi ya msingi ya Serikali za Mtaa watalazimika pia kuwatambua wageni wote watakaofika katika maeneo yao ni pamoja na kuwataka waonyeshe vitambulisho vyao na wale watakaokuwa na shaka nao watoe taarifa zao katika vyombo vya sheria.

SHERE THISE ON.; www.peterdafi.blogspot.com; www.facebook.com ; www.twitter.com

No comments:

Post a Comment