Pages

Monday, June 4, 2012

Chacha Marwa ajiweka sokoni

BEKI wa Yanga, Chacha Marwa amekaribisha mazungumzo na timu yoyote ya Ligi Kuu Tanzania Bara inayotaka kumsajili kwani hana imani kama atapewa mkataba mpya Yanga.

Marwa aliyejiunga na Yanga akitokea Mtibwa Sugar ya mjini Morogoro aliliambia Mwanaspoti jana Ijumaaa jijini Dar es Salaam kuwa; "Mkataba wangu na Yanga unamalizika mwezi huu (Juni), nipo tayari kufanya mazungumzo na klabu yeyote ya Ligi Kuu kwa lengo ya kusaini mkataba mpya."

Alisema: "Nafikiri ulikuwa ni msimu wangu mbaya kuliko yote, tumeshindwa kutetea ubingwa wa ligi na kumaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo, pia tumekosa nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao."

Beki huyo wa kati alisema; "Nafikiri ni wakati wangu mwafaka wa kutafuta maisha sehemu nyingine na kuendeleza kipaji changu cha soka, sikuwa mtu mwenye furaha kukaa benchi, napenda kucheza na kujifunza mengi kwa lengo la kulinda kiwango changu cha soka na kutimiza ndoto zangu nilizojiwekea kwa siku zijazo, siwezi kucheza soka milele, kuna mwisho wake."

Hata hivyo, benchi la ufundi la Yanga hivi karibuni lilikaririwa na vyombo vya habari likisema, wachezaji ambao walikosa nafasi katika kikosi cha kwanza wataachwa na wengine kutolewa kwa mkopo kwa lengo la kuushawishi uongozi kuwarejesha kikosini katika dirisha dogo la usajili mwakani endapo watapandisha viwango vyao.

Wachezaji waliotajwa kuachwa msimu huu ni mabeki ndugu, Zubery Ubwa na Abuu Ubwa na washambuliaji wa kigeni Kenneth Asamoah na Davies Mwape.

Wengine ni Julius Mrope, Chacha Marwa, Fredy Mbuna na Ibrahim Job wakati viungo Shamte Ally na Idrissa Rashid watapelekwa kwa mkopo Toto African ya Mwanza.


No comments:

Post a Comment