Pages

Monday, June 4, 2012

Vifaa vipya 12 vyamwagika Simba




SIMBA imethibitisha kwamba ina majina ya wachezaji wapya 12 kutoka katika nchi za Uganda, Rwanda, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na katika hao itachagua mmoja tu kujaza nafasi iliyobaki ya mchezaji wa kigeni.

Klabu hiyo pia imethibitisha kupata mrithi wa kuziba pengo la kiungo, Patrick Mafisango, baada ya kumpangia majukumu mapya, Mussa Mudde wa Uganda aliyetokea Sofapaka ya Kenya.

Simba imewasajili, Kanu Mbiyavanga kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Mudde watakaoungana na Mzambia Felix Sunzu na Emmanuel Okwi wa Uganda. Imebakisha nafasi moja ya mchezaji wa kigeni.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu', ameliambia Mwanaspoti kuwa mbadala wa Mafisango, amepatikana baada ya mabadiliko waliyofanya.

"Tulimsajili Mudde kwa madhumuni ya kucheza beki ya kati, lakini kutokana na matatizo hayo, sasa tumembadilisha na atacheza kiungo akishirikiana na Mbiyavanga kwa nafasi ya namba sita na nane," alisema Kaburu.

Nafasi hizo ndizo Simba walikuwa wakimtumia, Mafisango, ambaye alifariki kwa ajali ya gari mwezi uliopita.

Kaburu alisema kutokana na mabadiliko hayo, Simba sasa itaziba nafasi hiyo kumpata mchezaji wa kimataifa kwa nafasi ya beki wa kati.

"Tumebakisha nafasi moja ya mchezaji wa kimataifa, hiyo ni maalumu kwa ajili wa beki wa kati na tunatarajia atatoka katika moja ya nchi za Uganda, Rwanda, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo," alisema Kaburu.

"Tayari tuna majina ya wachezaji 12 kutoka katika nchi hizo na mmoja kati ya hao atakuja kuichezea Simba."

Kocha msaidizi wa kikosi hicho, Richald Amatre alisema: "Tunaye, Mbiyavanga ni kiungo, yupo
pia, Mudde wote wanaweza kucheza nafasi ya Mafisango bila tatizo."

Katika hatua nyingine, Kaburu aliweka wazi suala la wachezaji wao, Juma Nyosso, Juma Jabu na Uhuru Suleiman na kusema wapo huru baada ya kumaliza mikataba yao.

"Wote wako huru, lakini suala lao liko katika kamati zetu za Ufundi na Usajili na linashughulikiwa, wao watatufikishia na sisi tutalitolea maamuzi,"aliongeza.

Simba inaendelea na mazoezi yake ya gym katika kujiandaa na michuano mbalimbali ikiwemo ya Kagame inayoanza mwisho wa mwezi huu pamoja na Ligi Kuu Bara.

No comments:

Post a Comment