YUMO MGEJA, LEMBELI, MKONO, BASHE, KINGWANGALLA, PREMJI.
-------------------------------------------------------------------
MOJAWAPO
ya sifa kubwa atakayokumbukwa nayo Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni kutoa kauli tata
ambazo hubakia katika mjadala kwa muda mrefu.
Tofauti
kidogo na kauli za hawali safari hii kauli yake imeondoka na vigogo wa
chama hicho na kuwatupa nje ya kinyang’anyiro cha kuwania nafasi za
uongozi wa jumuiya za chama na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Habari kutoka ndani ya NEC,
ziliwataja walioenguliwa kuwa ni pamoja na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi
Kigwangalla na Mjumbe wa Baraza Kuu la Vijana la CCM Taifa (UVCCM),
Hussein Bashe.
Mbali
ya hao, hasira za mwenyekiti huyo wa chama tawala zimemwangukia
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na Mbunge wa Kahama,
James Lembeli.
Wengine
waliokumbwa na kadhia hiyo ni pamoja na Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina
na Mbunge wa Ludewa, Deo Filukunjombe. Wabunge hao ni miongoni mwa
waliotia saini kutaka Waziri Mkuu Pinda ang’oke. Duru za siasa zinasema
kuwa msimamo wa wabunge hao kuhusu Pinda, ndio ulisababisha wakatwe
kuwania NEC.
Athari
za saini za kutaka kumng’oa Pinda ambazo zilisababisha Baraza la
Mawaziri lipanguliwe na kuundwa upya, zimeonekana pia kumgusa Mbunge wa
Musoma Vijijini, Nimrod Mkono, ambaye ametupwa nje kuwania nafasi ya
uenyekiti wa wazazi CCM taifa.
Hali ya mkosi bado inaendelea
kumwandama Mbunge wa zamani wa Nyamagana, Antony Diallo na Mwenyekiti wa
CCM Mkoa wa Mwanza aliyekuwa akitetea nafasi yake, Clement Mabina ambao
nao majina yao yamengolewa.
Wakati
vigogo hao wakiugulia machungu ya kutoswa, Rais Kikwete ametoa kauli
nzito ambayo moja kwa moja inaonekana kuwalenga wahanga hao ya kutaka
wagombea waliopata kutoa kauli za vitisho dhidi ya chama hicho kufanya
kile walichokusudia kukifanya.
Akizungumza kwa ukali, Kikwete
ambaye juzi alitamba akisema CCM haitakufa kama inavyotabiriwa na baadhi
ya watu, alihitimisha kauli yake kwa kusema watu wenye kauli za namna
hiyo walikuwa hawafai kuendelea kuwa wanachama wa chama hicho.
Alisema
hivi sasa wagombea wengi wamekuwa wakijitokeza kuwania nafasi
mbalimbali za uongozi ndani ya CCM na kung’ang’ania kupata ushindi kiasi
cha wengine kufikia hatua ya kutoa kauli za vitisho kwa kusema
wasipopata nafasi ‘patachimbika’.
“Inashangaza kuona kugombea NEC tu watu wanataka kuuana, wanakimbilia nini huko ndani?” alihoji Rais Kikwete.
“Ina
maana watu hawa wanaonyesha dhahiri kuwa hawana nia njema na chama, bali
wanaingia kwa maslahi yao binafsi, hivyo tuna kila sababu ya kuwakataa
ili tujenge timu ya ushindi ambayo ndiyo nia yetu,” aliongeza mwenyekiti
huyo.
Rais Kikwete alisema kama kuna
wagombea ambao watajitoa ndani ya CCM na kuhamia chama kingine kutokana
na majina yao kutopendekezwa, wajitoe.
“Hatuchagui
wagombea wenye ndimi mbili ambao wanasema kama hatutapitishwa tutahamia
chama kingine, hao tunawatakia kila la heri waende tu, kwani hawana nia
njema na chama hiki,” alisema.
Mwenyekiti huyo ambaye alikuwa
akizungumza kwa ukali, alisema anajua suala la kuwaengua baadhi ya
wagombea litazua mjadala, lakini nia ya chama ni njema katika kuleta
sura mpya na uhai.
“Kufanya
hivyo ni pamoja na kupata viongozi watakaokiletea chama ushindi katika
chaguzi za Serikali za Mitaa 2014 pamoja na Uchaguzi Mkuu mwaka 2015,
hivyo lazima watu hao watambue kuwa kazi wanayoifanya ni kuunda timu ya
ushindi wa chama na si wa watu.
“Najua kuna ndugu na marafiki
ambao hawatateuliwa kutokana na kujaa kwa nafasi na mapungufu na
madhaifu ambayo yalionekana baada ya Kamati ya Maadili kupitia majina
yao, hivyo wasione kama wameonewa bali wajue kama ndio utaratibu wa
chama wa kuhitaji viongozi shupavu, hodari na mwenye uwezo wa kukitetea
na kukipigania chama na kukipa ushindi,” alisema Rais Kikwete.
Aliwatahadharisha
wagombea watakaotumia rushwa kwenye kampeni zao watambue kuwa Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wanafanya kazi yao muda
wote, hivyo atakayekamatwa asije akamlaumu mtu.
Habari hii na MPEKUZI BLOG
No comments:
Post a Comment