Pages

Tuesday, October 2, 2012

Mlipuko, majeshi yakidhibiti Kismayo



Wenyeji wakiuhama mji wa Kismayo
Mlipuko mkubwa umesikika mjini Kismayo huku wanjeshi wa Somalia wakishirikiana na majeshi ya AU, ambao wamedhibiti maeneo muhimu ya mji wa Kismayo.
Wenyeji wanasema kuwa mlipuko huo ulisikika kama bomu lililokuwa limetegwa kando ya barabara ingawa hakuna majeruhi wameripotiwa.
Shambulizi hilo linakuja baada ya wapiganaji wa Al-Shabab wanaohusishwa na kundi la kigaidi la al-Qaeda, kuondoka Kismayo ambayo ndiyo ngome yake kubwa mwishoni mwa wiki.
Jeshi la Somalia limesema vikosi vyake vikishirikiana na wanajeshi wa kudumisha amani wa Muungano wa Afrika, AMISOM tayari vimeuteka Mji wa Kismayo, ambao ndiyo ngome kuu ya mwisho ya kundi la wapiganaji la Al - Shabaab.
Kamanda wa Jeshi katika eneo hilo Ismael Sahardiid ameiambia BBC kwamba wanamiliki taasisi zote za Serikali, Bandari pamoja na Uwanja wa ndege.
Jumamosi iliyopita, kundi la Al Shabaab lilisema limetumia mbinu ya kujiondoa kutoka kwenye Mji huo na linaendelea kutekeleza mashambulizi ya kujitolea muhanga katika maeneo wasioyamiliki tena.
Kwa mujibu wa msemaji wa Jeshi la Kenya Meja Emmanuel Chirchir, majeshi ya Kenya na Somalia sasa yanasimamia Kituo kikuu cha Polisi cha Kismayo na Uwanja mpya wa ndege. Aliongezea kuwa pindi tu hali itakapokuwa shwari na salama, ndege zitaruhusiwa kutua katika Uwanja huo wa ndege.
Chirchir amesema kuwa wataalamu wa mabomu wametegua vilipuzi vilivyokuwa vimetegwa katika uwanja huo wa ndege na wapiganaji wa Al-Shabaab wenye uhusiano na kundi la Al-Qaida.
Vikosi vya Muungano wa Afrika vinaisaidia Serikali changa ya Somalia kudumisha amani katika Nchi hiyo iliyokumbwa na misukosuko tangu mibabe wa kivita walipoupindua Utawala wa muda mrefu wa kidikteta mwaka 1991.

HABARI HII NA  Mwandishi wa BBC

No comments:

Post a Comment