Polisi huko visiwani Zanzibar wanachunguza tukio la kasisi wa kanisa katoliki kushambuliwa kwa tindikali.
Imeelezwa kuwa Kasisi huyo Anselmo Mwang'amba,
alimwagiwa tindikali akitoka mgahawa mmoja wa kutumia mtandao mjini
Zanzibar. Tukio hilo linatokea ndani ya mwezi mmoja tangu wasichana
wawili wa kiingereza kushambuliwa.Hili ni janga jingine kwa Zanzibar ambayo imekuwa ikizongwa na matukio ya aina hii kwa muda sasa.
Mkurugenzi wa upelelezi wa Zanzibar, Yusufu Ilembo ameieleza BBC kuwa bado hawajakamata mtu yoyote kuhusika na tukio hilo ingawa amethibitisha kuwa uchunguzi tayari umeanza.
Ameeleza kuwa Kasisi Mwang'amba aliungua usoni na mabegani na kwamba anaendelea kutibiwa.
Katika miaka ya karibuni Zanzibar imekabiliwa na mikasa ya watu kushambuliwa hivi na kuzua hisia kuwa chuki za kidini.
Mapema mwaka huu kasisi mwingine wa kanisa katoliki alishambuliwa kwa risasi na kuuawa.
Mwezi uliopita Zanzibar ilitikisika kutokana na wasichana wawili wangereza kushambuliwa kwa tindikali na watu wasiojulikana.
Kiongozi mmoja wa dini ya kiislamu pia alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana.
No comments:
Post a Comment