Pages

Sunday, October 20, 2013

China kuleta Tanzania watalii 30,000


CHINA imeahidi kuleta nchini watalii 30,000 katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwakani.
Ahadi hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Wakala wa kutoa huduma za usafiri wa China na Hong Kong, Zhang Xuewu alipofanya mazungumzo na Waziri Mkuu Mizengo Pinda jijini Shenzen, China.
Alisema kampuni yake itawandaa mawakala wa usafirishaji watalii kuhakikisha kuwa watalii 10,000 wanapatikana kila mwaka ambao kiu yao ni kuja nchini.
“Wengi wanapenda kutembelea mbuga, lakini hapa nchini wamezoea kuona walio sakafuni, wakija watawaona wanyama live” (akimaanisha kuwa Wachina wamezoea kuona wanyama wa sanamu kwenye makumbusho yao hapa jiji la Shenzhen).
Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya China, alisema haelewi ni kwa nini kampuni hiyo imeweza kupeleka watalii Afrika Kusini na nchi jirani za Afrika Mashariki wakati haina urafiki nazo lakini imeshindwa kuwaleta Tanzania yenye uhusiano mzuri kwa muda mrefu.
Akizungumza na Xuewu pamoja na baadhi ya viongozi kutoka Tanzania alioambatana nao, Waziri Mkuu alisema amepewa maelekezo rasmi na Rais Jakaya Kikwete ya kufuatilia suala la watalii wa kutoka China, hasa ikizingatiwa kwamba mazungumzo ya jambo hili yalianza wakati wa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
“Katika bara la Afrika hakuna nchi yenye vivutio lukuki kama Tanzania. Na tovuti ya www.safaribooking. com imeitangaza Tanzania kuwa nchi inayofaa kwa safari za mbugani kama mtu anataka kuona vivutio vizuri na vya asili. Sasa ni kwa nini hatupati watalii wa kutosha na tunafanyaje ili kubadilisha hali hiyo?” alihoji.
Alisema njia mojawapo ni kuhakikisha kunakuwa na ndege ya moja moja kutoka miji ya China hadi Dar es Salaam, jambo alisema litasaidia kupunguza kero kwa wasafiri ambao hivi sasa inabidi waunge safari mara mbili hadi tatu ili kufika Tanzania.
“Tuangalie uwezekano wa kuwa na ndege ya moja kwa moja kutoka China hadi Dar es Salaam au Arusha... wenzetu Kenya na Afrika Kusini wameweza kupata watalii wengi sababu wana ndege za moja kwa moja,” alisema.
Alimshawishi mwenyekiti huyo aangalie pia uwezekano wa kujenga hoteli katika mikoa nchini kupunguza uhaba wa vyumba punde watalii wakianza kufurika.
Pia alimhakikishia fursa ya kujenga uwanja wa gofu chini ya mlima Kilimanjaro kwani yote mawili ni maeneo ambayo kampuni yake inao uwezo wa kufanya kama sehemu ya majukumu yake.

No comments:

Post a Comment