Pages

Sunday, November 3, 2013

DK, Hamisi Kigwangala awajibu Mhe. Deo Filikunjombe na Mwenzie.....!!!!?

Nimeona hawa nisiwaache wapotoshe umma kwa maslahi yao binafsi, acha niwajibu.

Kwanza, niseme hapa wazi kwamba, ni mwendawazimu tu ama mtu asiyeelewa mahusiano ya Mhe. Deo Filikunjombe (Mb.) na Mhe. Spika Anne Makinda (Mb.) ama na Mhe. Kangi Lugora (Mb.), atakayepata tabu kuelewa kwa nini watu hawa wamenishambulia kwenye magazeti na mitandao ya kijamii. Deo Filikunjombe ni 'mtoto wa mama' Anne Makinda!

Pili, niseme pia kwamba watu wa aina hii hawakustahili kujibiwa lakini kwa ushauri wa wabunge wengi wanaoniunga mkono nimeamua niwajibu. Hawa wabunge wenye kuja na nyoka wa dhahabu bungeni na kujigamba wao ni majasiri kwa kuwa 'walisaini karatasi ya hoja ya kumng'oa Waziri Mkuu na baada ya kushughulikiwa na wabunge wenzao wa CCM walianza kulia lia kwa Mwenyekiti wa Chama kuwa wasamehewe kwa kuwa waliasi chama kwa sababu wamebanwa sana majimboni mwao na wanaCCM wenzao na pia na wapinzani', kwa hakika hawakustahili majibu toka kwangu. Tabia za ukinyonga namna hii ni ujasiri, udandiaji hoja ama kutokujua wanalofanya ndani ya Bunge?

Hawa wabunge wanaopiga makelele kutetea CHC kumbe wamelambishwa mzigo. Hawa wabunge wanaojidai wao ni wazalendo wanaojipambanua kwa kupinga ufisadi wa mawaziri kumbe wenyewe wanachukua hela za mashirika wanayoyakagua. Huu ni uzalendo ama kudanganya wananchi wasiojua ukweli na uhalisia wa sura za watu hawa?

Tatu, naomba nitumie fursa hii kusema kuwa hoja yangu, inayoungwa na wabunge wengi inajikita zaidi kwenye kumuwajibisha Spika wa Bunge kwa kukiuka masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63 (2), ibara ya 100, kwa kutuzuia wabunge tusiiingize jedwali la marekebisho wakati wa kutunga sheria ya fedha kwa kututaka tuyapeleke mbele ya Kamati ya Mhe. Andrew Chenge (Mb.) kinyume na Kanuni za Bunge, na hivyo kusababisha vifungu vyenye mambo ya hovyo kama ya 'kodi ya simcard' vipite bila kupingwa na wabunge. Wachunguzi wa mambo kasomeni hansard za Bunge za kuanzia tare 26 Juni 2013 mje mkanushe kama kuna mbunge aliruhusiwa kuleta Bungeni jedwali la marekebisho. Mimi nilikuwa na jedwali lenye mapendekezo ya marekebisho 19, Mnyika vile vile, Wenje, Sakaya, Soni, Mangungu na wengineo - sote sisi tulikataliwa kuleta majedwali yetu Bungeni. Kasomeni pia na nyie Kanuni zinasemaje kuhusu namna ya kupitisha Sheria wakati wa muswada kusomwa kwa mara ya pili Bungeni?!

Binafsi, nimeishawasilisha hoja binafsi zifuatazo, ya madini Nzega (nimeipeleka Bungeni zaidi ya mara 8 na sikupewa nafasi), ya kuzuia ugawaji vitalu vipya vya gesi (mara 3), ya madawa ya kulevya (mara 2), ya kuzuia uingizaji wa Genetically Modified Organisms, ya kufanya marekebisho ya mifuko ya hifadhi ya jamii (mara 2), ya kuanzisha mfuko wa kulinda bei za wakulima (price stabilisation fund), na pia muswada binafsi nikishirikiana na wabunge wengine 8 (kuanzisha parliamentary budget office). Waluizeni wabunge wenu wameishawasilisha hoja zao mara ngapi na wameruhusiwa mara ngapi?

Hoja yangu inajikita kwenye kumwondoa Spika madarakani kwa kushindwa kusimamia Sheria ya Bunge ya mwaka 2008, kushindwa kuzilinda Kanuni za Bunge; mfano anapozuia hoja binafsi na miswada binafsi ya wabunge isiingizwe bungeni kwa kisingizio hakuna muda ilhali sababu kubwa ni kuwa hana bajeti na anafanya kazi kinyume na utaratibu wa Sheria ya Bunge ya mwaka 2008 inayotaka Bunge liwe na mfuko wake ili lisiendeshwe na namna serikali inavyotaka. Bunge linapokuwa tegemezi kwa serikali maana yake ile 'doctrine ya separation of power' inakuwa majaribuni. 'Mfuko wa Bunge' ambao ungemwezesha kupanga shughuli za bunge kwa kadri anavyoona inafaa badala ya kutegemea apate pesa kutoka serikalini ambapo humpa za kutosha kushughulikia shughuli za serikali tu na hivyo kuwanyima wabunge haki ya uwakilishi haupo hadi leo wakati unapaswa kuwepo kwa mujibu wa sheria niliyoitaja hapo juu.

Mfano mwingine ni pale anavyotumia Kanuni ya 48, inayohusu mambo ya dharura, vibaya na hivyo kukataa mijadala yote ya dharura - mfano pale boti ya MV Skagit ilipozama kandoni mwa kisiwa cha Chumbe na yeye Spika akaona hili si jambo la dharura. Watu wanakufa, wabunge wanataka tusitishe shughuli za Bunge tujadili jambo la dharura, yeye anadai hilo si jambo la dharura! Kuna mambo mengi zaidi ya haya machache niliyoyataja hapa. Kuna la kuteua Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Mhe Andrew Chenge (Mb.) kinyume na Kanuni na taratibu za Bunge. Kesho tunaweza kufanya mkutano na waandishi wa habari na hivyo kuweka hadharani hoja yenyewe na kujibu maswali kwa waandishi wa habari ili suala hili lieleweke vizuri.

Nne, hoja hii haizungumzii posho hata kidogo, ni watu wa aina ya hawa wawili tu wanaoweza kupata tabu kuelewa muktadha wa hoja nzito kama hii. Na hawa wanapata upofu huu aidha kwa kuwa wana 'maslahi binafsi' ama uelewa mdogo wa Kanuni za Bunge. Ningewashauri waje wahudhurie kikao tutakachofanya kesho kujadili namna tutakavyoipitisha hoja hii na kufanikisha kumwondoa madarakani Spika Makinda kwa kukiuka Kanuni mara nyingi zaidi katika historia kuliko maspika wote waliomtangulia!

Tano na mwisho, wabunge hawa 'waoga na wanafiki' wakome kuvamia mambo wasiyoyajua na wafahamu mimi huwa sidandii hoja za watu kama wao. Aina ya siasa zangu si kama za kwao, za kukurupuka na kusema maneno mepesi mepesi ilimradi tu waonekane wanapinga serikali kwenye kila kitu.

Ahsanteni,
HK.

No comments:

Post a Comment