Home »
kitaifa
,
siasa
» DK, Hamisi Kigwangala awajibu Mhe. Deo Filikunjombe na Mwenzie.....!!!!?
DK, Hamisi Kigwangala awajibu Mhe. Deo Filikunjombe na Mwenzie.....!!!!?
Nimeona hawa nisiwaache wapotoshe umma kwa maslahi yao binafsi, acha niwajibu.
Kwanza, niseme hapa wazi kwamba, ni mwendawazimu tu ama mtu asiyeelewa
mahusiano ya Mhe. Deo Filikunjombe (Mb.) na Mhe. Spika Anne Makinda
(Mb.) ama na Mhe. Kangi Lugora (Mb.), atakayepata tabu kuelewa kwa nini
watu hawa wamenishambulia kwenye magazeti na mitandao ya kijamii. Deo
Filikunjombe ni 'mtoto wa mama' Anne Makinda!
Pili, niseme pia
kwamba watu wa aina hii hawakustahili kujibiwa lakini kwa ushauri wa
wabunge wengi wanaoniunga mkono nimeamua niwajibu. Hawa wabunge wenye
kuja na nyoka wa dhahabu bungeni na kujigamba wao ni majasiri kwa kuwa
'walisaini karatasi ya hoja ya kumng'oa Waziri Mkuu na baada ya
kushughulikiwa na wabunge wenzao wa CCM walianza kulia lia kwa
Mwenyekiti wa Chama kuwa wasamehewe kwa kuwa waliasi chama kwa sababu
wamebanwa sana majimboni mwao na wanaCCM wenzao na pia na wapinzani',
kwa hakika hawakustahili majibu toka kwangu. Tabia za ukinyonga namna
hii ni ujasiri, udandiaji hoja ama kutokujua wanalofanya ndani ya Bunge?
Hawa wabunge wanaopiga makelele kutetea CHC kumbe wamelambishwa mzigo.
Hawa wabunge wanaojidai wao ni wazalendo wanaojipambanua kwa kupinga
ufisadi wa mawaziri kumbe wenyewe wanachukua hela za mashirika
wanayoyakagua. Huu ni uzalendo ama kudanganya wananchi wasiojua ukweli
na uhalisia wa sura za watu hawa?
Tatu, naomba nitumie fursa
hii kusema kuwa hoja yangu, inayoungwa na wabunge wengi inajikita zaidi
kwenye kumuwajibisha Spika wa Bunge kwa kukiuka masharti ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 63 (2), ibara ya 100, kwa
kutuzuia wabunge tusiiingize jedwali la marekebisho wakati wa kutunga
sheria ya fedha kwa kututaka tuyapeleke mbele ya Kamati ya Mhe. Andrew
Chenge (Mb.) kinyume na Kanuni za Bunge, na hivyo kusababisha vifungu
vyenye mambo ya hovyo kama ya 'kodi ya simcard' vipite bila kupingwa na
wabunge. Wachunguzi wa mambo kasomeni hansard za Bunge za kuanzia tare
26 Juni 2013 mje mkanushe kama kuna mbunge aliruhusiwa kuleta Bungeni
jedwali la marekebisho. Mimi nilikuwa na jedwali lenye mapendekezo ya
marekebisho 19, Mnyika vile vile, Wenje, Sakaya, Soni, Mangungu na
wengineo - sote sisi tulikataliwa kuleta majedwali yetu Bungeni.
Kasomeni pia na nyie Kanuni zinasemaje kuhusu namna ya kupitisha Sheria
wakati wa muswada kusomwa kwa mara ya pili Bungeni?!
Binafsi,
nimeishawasilisha hoja binafsi zifuatazo, ya madini Nzega (nimeipeleka
Bungeni zaidi ya mara 8 na sikupewa nafasi), ya kuzuia ugawaji vitalu
vipya vya gesi (mara 3), ya madawa ya kulevya (mara 2), ya kuzuia
uingizaji wa Genetically Modified Organisms, ya kufanya marekebisho ya
mifuko ya hifadhi ya jamii (mara 2), ya kuanzisha mfuko wa kulinda bei
za wakulima (price stabilisation fund), na pia muswada binafsi
nikishirikiana na wabunge wengine 8 (kuanzisha parliamentary budget
office). Waluizeni wabunge wenu wameishawasilisha hoja zao mara ngapi na
wameruhusiwa mara ngapi?
Hoja yangu inajikita kwenye kumwondoa
Spika madarakani kwa kushindwa kusimamia Sheria ya Bunge ya mwaka 2008,
kushindwa kuzilinda Kanuni za Bunge; mfano anapozuia hoja binafsi na
miswada binafsi ya wabunge isiingizwe bungeni kwa kisingizio hakuna muda
ilhali sababu kubwa ni kuwa hana bajeti na anafanya kazi kinyume na
utaratibu wa Sheria ya Bunge ya mwaka 2008 inayotaka Bunge liwe na mfuko
wake ili lisiendeshwe na namna serikali inavyotaka. Bunge linapokuwa
tegemezi kwa serikali maana yake ile 'doctrine ya separation of power'
inakuwa majaribuni. 'Mfuko wa Bunge' ambao ungemwezesha kupanga shughuli
za bunge kwa kadri anavyoona inafaa badala ya kutegemea apate pesa
kutoka serikalini ambapo humpa za kutosha kushughulikia shughuli za
serikali tu na hivyo kuwanyima wabunge haki ya uwakilishi haupo hadi leo
wakati unapaswa kuwepo kwa mujibu wa sheria niliyoitaja hapo juu.
Mfano mwingine ni pale anavyotumia Kanuni ya 48, inayohusu mambo ya
dharura, vibaya na hivyo kukataa mijadala yote ya dharura - mfano pale
boti ya MV Skagit ilipozama kandoni mwa kisiwa cha Chumbe na yeye Spika
akaona hili si jambo la dharura. Watu wanakufa, wabunge wanataka
tusitishe shughuli za Bunge tujadili jambo la dharura, yeye anadai hilo
si jambo la dharura! Kuna mambo mengi zaidi ya haya machache
niliyoyataja hapa. Kuna la kuteua Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Mhe
Andrew Chenge (Mb.) kinyume na Kanuni na taratibu za Bunge. Kesho
tunaweza kufanya mkutano na waandishi wa habari na hivyo kuweka
hadharani hoja yenyewe na kujibu maswali kwa waandishi wa habari ili
suala hili lieleweke vizuri.
Nne, hoja hii haizungumzii posho
hata kidogo, ni watu wa aina ya hawa wawili tu wanaoweza kupata tabu
kuelewa muktadha wa hoja nzito kama hii. Na hawa wanapata upofu huu
aidha kwa kuwa wana 'maslahi binafsi' ama uelewa mdogo wa Kanuni za
Bunge. Ningewashauri waje wahudhurie kikao tutakachofanya kesho kujadili
namna tutakavyoipitisha hoja hii na kufanikisha kumwondoa madarakani
Spika Makinda kwa kukiuka Kanuni mara nyingi zaidi katika historia
kuliko maspika wote waliomtangulia!
Tano na mwisho, wabunge
hawa 'waoga na wanafiki' wakome kuvamia mambo wasiyoyajua na wafahamu
mimi huwa sidandii hoja za watu kama wao. Aina ya siasa zangu si kama za
kwao, za kukurupuka na kusema maneno mepesi mepesi ilimradi tu
waonekane wanapinga serikali kwenye kila kitu.
Ahsanteni,
HK.
Post a Comment