SAKATA LA KUVULIWA ZITTO UANACHAMA NA VYEO VYOTE HILI HAPA...!!
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakitashughulikia
rufaa iliyokatwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, kwa Baraza
Kuu kupinga uamuzi wa Kamati Kuu (CC) wa kumvua nyadhifa zake katika
chama, hadi hapo itakapopitia utetezi wake na kuamua hatima ya uanachama
wake katika chama hicho.
Pia kimethibitisha kupokea utetezi
dhidi ya mashitaka 11 yanayohusisha usaliti dhidi ya chama na kuwachafua
viongozi wakuu kupitia waraka wa mabadiliko.
Mashtaka hayo
yanamkabili Zitto, pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa CC, Dk. Kitila Mkumbo
na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Victor Kimesera, alisema hayo alipozungumza na NIPASHE, ofisini kwake, jijini Dar es Salaam jana.
Kimesera, ambaye ni Katibu Mtendaji Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chadema,
alisema rufaa hiyo ni kitu kidogo, hivyo haiwezi kuanza kushughulikiwa
na chama katika sakata la Zitto na watuhumiwa wenzake.
“Kuna
(kitu) kikubwa cha mbele yake (rufaa),” alisema Kimesera akijibu swali
la NIPASHE lililotaka kujua nini kinaendelea kwenye chama baada ya Zitto
kukata rufaa.
Kimesera alisema kitu kikubwa kuliko rufaa, ambacho
kitaanza kushughulikiwa na chama ni maelezo ya utetezi wa Zitto na
watuhumiwa wenzake.
Alisema hiyo ni kwa sababu tayari kuna hoja
ya CC, ambayo inataka ijiridhishe kama Zitto na wenzake waendelee kuwa
uanachama au la.
Kwa mujibu wa Kimesera, baada ya Zitto na
wenzake kuwasilisha utetezi wao, CC itaitishwa na kuyapitia na kisha
itatoa maamuzi juu ya uanachama wao.
“Sasa huwezi kuongea juu ya rufaa wakati hujajua uanachama wao kwanza,” alisema Kimesera.
Hivyo, alisema rufaa ya Zitto itaendelea kuhifadhiwa kwenye jalada
hadi hapo hatua ya kwanza ya kupitia maelezo yao ya utetezi na kuyatolea
maamuzi itakapochukuliwa. “Lazima twende kwa hatua. Kwa hiyo, hiyo
(rufaa) imekaa,” alisema Kimesera.
Mwanasheria wa Zitto,
Albert Msando, alitaja sababu mbili za mteja wake kukata rufaa kuwa ni
kukiukwa kwa taratibu za kuchukua hatua za nidhamu na sababu
zilizotolewa kutokuwa sahihi.
Msando alitaja kifungu cha 6.5.6
cha Kanuni ya Uendeshaji ya chama hicho, akisema utaratibu uliotakiwa
kufuatwa kabla ya kumchukulia hatua za kinidhamu kiongozi kwa mujibu wa
Katiba na Kanuni ni kupewa kwanza mashtaka kwa maandishi ili apate
nafasi ya kujibu.
Alisema kiongozi yeyote hatachukuliwa hatua
za kinidhamu bila kwanza kupewa mashtaka yake kwa maandishi na mamlaka
husika na kupewa nafasi ya kujibu mashtaka kwa maandishi.
Alitaja ibara ya 5.4.3 na 5.4.4 ya Katiba kwamba mwanachama yeyote
hatachukuliwa hatua za kinidhamu ama kuonywa ama kuachishwa ama
kufukuzwa uanachama bila kujulishwa makosa yake kwa maandishi na
kutakiwa kutoa majibu katika muda usiopungua wiki mbili.”
Alitaja vipengele vingine ni kupewa nafasi ya kujitetea mbele ya kikao
kinachohusika na atajulishwa kwa maandishi uamuzi wa kikao ndani ya wiki
mbili baada ya kusikilizwa.
Katika hatua nyingine, Kimesera
alisema Chadema imepeleka majibu baada ya Mwigamba kupeleka barua yenye
malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa dhidi ya uongozi wa chama
hicho.
Katika malalamiko yake, Mwigamba anadai kuwa katiba ya
Chadema ilivurugwa na viongozi wa chama kwa kuondoa kinyume cha taratibu
maelezo ya kifungu cha katiba ya chama yaliyokuwa yakiainisha ukomo wa
vipindi viwili vya uongozi.
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini,
Jaji Francis Mutungi, alithibitisha kupokea barua hiyo ya Mwigamba na
kusema ofisi yake inaifanyia kazi.
Kimesera jana, kuwa
walipeleka majibu dhidi ya malalamiko ya Mwigamba baada ya kuagizwa na
msajili kufanya hivyo kabla ya Desemba 19, mwaka huu.
Katika
barua yake, Mwigamba amemuomba msajili kutoa mwongozo kuhusu anachodai
kuwa ni mgogoro wa kikatiba uliopo ndani ya Chadema kufuatia kipengele
cha katiba kinachogusia ukomo wa uongozi kubadilishwa kinyume cha
utaratibu.
Novemba 22, mwaka huu, CC iliwavua madaraka
viongozi hao na kuwataka wajieleze kwa maandishi ndani ya siku 14 baada
ya kudaiwa kuhujumu chama kwa kuandika waraka wa siri unaodaiwa pamoja
na mambo mengine, kuwadhalilisha viongozi wakuu wa Chadema.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment