Pages

Thursday, January 2, 2014

Zitto Kabwe Aenda Korti Kuu


Zitto Kabwe na wakili wake Albert Msando 
WAKATI Kamati Kuu (CC) ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ikitarajia kukutana leo jijini Dar es Salaam, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amekimbilia Mahakama Kuu kuomba mkutano huo uzuiliwe kumjadili.
Kutokana na ombi hilo, Mahakama Kuu imekubali kwa muda kusitisha uamuzi wa CC ya CHADEMA kujadili uanachama wa Zitto  mpaka itakapotoa uamuzi leo katika kesi ya msingi iliyofunguliwa na mbunge huyo.
Uamuzi huo ulitolewa jana majira ya saa 12:37 jioni na Jaji wa Mahakama hiyo,  John Utamwa.
Katika amri hiyo, Jaji Utamwa alisema kwa kuzingatia masilahi ya pande zote mbili ni vema walalamikiwa wakasitisha uamuzi wowote wa kujadili uanachama wa Zitto mpaka shauri hilo litakapotolewa uamuzi na mahakama.
Uamuzi wa mahakama unatarajiwa kutolewa leo kuanzia saa 3:30 asubuhi huku Kamati Kuu ya CHADEMA ikiruhusiwa kuendelea na kuwajadili wanachama wengine wawili; Dk. Kitilla Mkumbo na Samson Mwigamba, ambao nao walivuliwa uongozi kwa madai ya kukisaliti chama hicho.
Mara baada ya uamuzi huo, wanasheria wa pande zote mbili kwa nyakati tofauti walizungumza na waandishi wa habari na kueleza kuwa wameridhishwa na hatua ya awali ya uamuzi huo.
Kamati Kuu ya CHADEMA inatarajia kukutana leo jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo ambao una ajenda kuu tatu, pamoja na mambo mengine ulipanga kumhoji Zitto na wenzake kutokana na tuhuma za kukisaliti chama zilizosababisha avuliwe nyadhifa zake zote za uongozi, huku akilimwa barua ya kutaka ajitetee ndani ya siku 14.
Wengine waliosimamishwa uongozi na kutakiwa wajitetea ni pamoja na Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Arusha, Samson Mwigamba na Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) ya CHADEMA taifa, Dk. Kitila Mkumbo.
Awali katika maombi yake katika kesi hiyo inayovuta hisia za wengi iliyopewa namba moja ya mwaka 2014, Zitto anayetetewa na wakili Albert Msando, anaiomba Mahakama Kuu kuwazuia washtakiwa kwa pamoja na Kamati Kuu ya CHADEMA na chama au chombo chochote kwa makusudi, kujadili au kuamua suala la uanachama wake.
Maombi mengine ni kutaka apatiwe nakala ya uamuzi wa Kamati Kuu iliyoketi hivi karibuni na kumvua uanachama ili aweze kukata rufaa kwa Baraza la Uongozi la CHADEMA.
Katika ombi jingine, Zitto anaiomba mahakama iwazuie washtakiwa kuingilia kati wajibu na majukumu yake ikiwemo ya ubunge wa Kigoma Kaskazini.
Katika kesi hiyo mshtakiwa wa kwanza ni Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu wa CHADEMA.
Kwa upande wa CHADEMA walisimamiwa na Mwanasheria wao Mkuu, Tundu Lissu, akishirikiana na wakili, Peter Kibatala, ambao waliieleza mahakama hiyo kuwa hati ya kiapo iliyotolewa ina upungufu wa kisheria.
Pia walidai kuwa kisheria migogoro ya chama inamalizwa ndani ya chama husika, likiwemo suala la rufaa yake kurudishiwa uongozi, halipo katika mkutano unaofanyika leo.
Lisu alisema Zitto aliitwa ili kutetea nafasi yake ya uongozi, Naibu Katibu Mkuu Bara, hoja ya kukataa rufaa ili arejeshewe uongozi haviusiani na mkutano huo.
Pia mawakili hao walidai kuwa sheria iliyoomba Mahakama Kuu kuingilia kati mkutano huo haikuwa sahihi, hivyo haiwezi kuifanya mahakama kuisikiliza  kesi hiyo.
Novemba 22, mwaka jana, Kamati Kuu iliyoketi kwa siku mbili jijini Dar es Salaam ilifikia uamuzi wa kumvua nyadhifa za uongozi Zitto na wenzake,  kwa madai ya kukisaliti na kukihujumu chama.
Zitto anadaiwa alikuwa kinara wa mkakati wa kuleta mabadiliko haramu ndani ya chama hicho, huku waasisi hao wakijipa majina ya MM, M1 na M2, ambao ndani yake anadaiwa kuwamo Dk. Mkumbo, mjumbe wa CC na NEC.
Chanzo:- Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment