Pages

Thursday, February 27, 2014

JABIRI OMARY AJIBU TUHUMA ZA WIZI WA SIMU DHIDI YA PAUL MAKONDA

 Jabiri Omary


TUHUMA YA SIMU DHIDI YA MAKONDA: MCHAKATO WA KATIBA MPYA  VIJANA TUSIMAME  PAMOJA.

Nimesoma taarifa ambazo zinasambazwa, kwenye mitandao ya kijamii ikimtuhumu Mbunge wa Bunge Maalumu la Katiba ndugu Paul Makonda kuhusika katika upo tevu wa simu ya Mjumbe wa Bunge la Katiba Bi Rehema. Huu ni mfululizo wa mashambulizi ambayo yamekuwa yakielekezwa kwake tangu kuanza kwa mchakato huu wa Bunge maalumu la Katiba.

Itakumbukwa kwamba, wiki iliyopita ilisambazwa taarifa dhidi yake kwamba ni miongoni mwa wajumbe ambao walikuwa wanataka nyongeza ya posho jambo ambalo alilikanushi kupitia mitandao ya kijamii na baadae kulitolea ufafanuzi kupitia Radio Clouds.

Binafsi sikutarajia hasa kwa kipindi kama hiki ambacho kinahitaji umoja na mshikamano wa vijana, kuibuka kundi la watu ambao watatumia muda wao na rasilimali zao kuwavunja moyo wajumbe wetu wa Bunge la katiba hasa vijana waliopata fursa ya kutuwakilisha katika Bunge hili la katiba, badala ya kuwatia moyo, kuwashauri na kuwasaidia katika mambo ya msingi ambayo tunaamini yana tija na maslahi kwa taifa letu. Kwa mtu mwelevu na mwenye akili timamu haiingii akilini kwa kijana Paul Makonda au mjumbe yeyote wa Bunge la katiba kuchukua simu ya Mjumbe mwingine. Ukumbi wa Bunge una kamera, ambapo hakuna jambo lolote ambalo litafanyika ndani ya ukumbi wa Bunge bila kujulikana au kuonekana.

Tukumbuke kwamba, katiba tunayoiandika leo, tutadumu nayo zaidi sisi vijana ambao kibaiolojia tuna umri mrefu kuliko wazee. Aidha, takwimu zinaoneshwa kwamba vijana ndiyo kundi kubwa kuliko kundi lingine lolote katika taifa letu. Pia kundi hili ndilo linakabiliwa na changamoto lukuki katika maisha yao ya kila siku yakiwemo kutumika katika matumizi ya madawa ya kulevya, uuzaji wa miili na tatizo la ajira. Matarajio yetu ni kuona kwamba katiba mpya inajibu changamoto au inaweka mazingira rafiki ya kisheria ambayo yatachochea uwajibikaji zaidi kwa serikali na taasisi za vijana kujibu changamoto zinazowakabili vijana.

Rasimu ya katiba ibara ya 44 inasema "Kila kijana ana haki na wajibu wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Jamhuri ya Muungano pamoja na jamii kwa ujumla na kwa mantiki hiyo, Serikali ya Muungano, serikali za nchi washirika na Jamii zitahakikisha kuwa vijana wanawekewa mazingira mazuri ya kuwa raia wema na kupatiwa fursa za kushiriki kikamilifu katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni".

Je, Ibara hii inatosha kusimama mbele ya vijana wa taifa hili na kusema kwamba katiba imewatambua vijana? Je, ukilinganisha hali halisi ya vijana kwa sasa, je Ibara hii inatosha kujibu changamoto za vijana wa sasa na miaka 50 ijayo? Kwa nini tusitumie muda huu kufanya tafiti za namna gani katiba za nchi nyingine duniani zimewagusa vijana na namna ambavyo wamefanikiwa kujenga mifumo ambayo inawezesha vijana na watu wote kunufaika na rasilimali za nchi kama vile madini, kudhibiti mianya ya rushwa na ufisadi ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa kurejesha nyuma  maendeleo ya taifa letu sambamba na kujenga mazingira mazuri ya kikatiba ambayo inawapa mamlaka wananchi kuwa na maamuzi juu ya hatma ya taifa lao.

Kwa nini vijana tujengeane chuki eti kwa sababu ya tofauti zetu za kiitikadi au kimtazamo? Binafsi nachukizwa na napata taabu kuona vijana ambao ndiyo msingi wa ujenzi wa taifa letu tunakubali kugawanywa katika makundi aidha ndani ya vyama vyetu vya siasa au nje ya vyama vya siasa. Hatuwezi kuwa na nguvu kama hatutakubali kuwa wamoja.

Kwa maoni yangu wajumbe wa Bunge la katiba wanahitaji mchango wetu, tuwaunge mkono, tuwashauri na tushirikiane nao ili wafanye maamuzi ya sahihi kwa hatma ya Tanzania ya miaka 100 ijayo. Majungu siyo kazi ya vijana.

Yours
Jabiri Omari


 


No comments:

Post a Comment