Dr. Hamisi Kigwangalla, MB, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, alizaliwa Mwaka 1975, Mwezi Agosti, Tarehe 7 katika Hospitali ya Maweni, Kigoma. Akiwa ni mtoto wa kwanza wa Bwana Mahampa Kigwangalla na bibi Bagaile Lumola. Baba yake ni Mkimbu kutokea kijiji cha Goweko, Uyui, Tabora na Mama yake ni Mnyamwezi mzaliwa wa Nzega, huko huko Tabora. Wakati anazaliwa Baba yake alikuwa ni mtumishi wa benki ya NBC (ya zamani) na mama alikuwa ni mwalimu wa daraja la A. Alikulia mjini Nzega kwa babu na bibi yake baada ya wazazi wake kutengana.
Amesoma shule ya msingi Kitongo na Mwanzoli, Nzega. Sekondari alisomea Kigoma Secondary School, ambapo alifaulu vizuri masomo ya sayansi na kuchaguliwa kwenda kusoma Shinyanga Secondary School, kombinesheni ya Physics, Chemistry na Biology (PCB), ambapo alifaulu vizuri kwa division I na kuchaguliwa kusomea masomo ya Udaktari katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Muhimbili University College of Health Sciences. Mwaka 2004, alihitimu masomo ya Udaktari wa Tiba na kutunukiwa digrii ya 'Doctor of Medicine' ya chuo kikuu cha Dar es salaam. Alifanya internship katika hospitali ya taifa ya muhimbili na baadaye hospitali ya Mwananyamala. Baada ya hapo alipata fursa ya kusoma Masters of Public Health (MPH) katika Chuo Cha Karolinska Institutet na Master of Business Administration (MBA) akibobea zaidi kwenye Organization and Leadership, katika chuo kikuu cha Blekinge Institute of Technology - vyuo vyote hivi vipo nchini Sweden.
Sasa hivi, Dr. Kigwangalla anamalizia tasnifu yake ya shahada ya uzamivu (Ph.D.) kwenye Public Health, akibobea zaidi kwenye Health Economics. Anaandika tasnifu yake kuhusiana na haki, usawa na uhalali wa mchakato wa bajeti kwenye sekta ya afya nchini Tanzania.
Amewahi kushika nyadhifa mbalimbali. Daktari daraja la II, Mtafiti na mtaalamu mshauri wa kujitegemea. Pia ni Mkurugenzi mwanzilishi wa makampuni yaliyo wanachama wa MSK Group, na amewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Group hii kabla ya kuwa Mbunge wa Jimbo la Nzega. Kampuni ya MSK Group inaweza kukadiriwa kwa sasa kumiliki mali na madeni kwa kiwango cha TZS 10bn, na inazungusha kwa mwaka mtaji wa takriban TZS 4bn. Inaajiri watanzania wapatao 400 moja kwa moja (katika nyakati mbali mbali za mwaka), na zaidi ya 200,000 indirectly.
Dr. Kigwangalla amewahi kuanzisha na ama kushiriki harakati mbalimbali za kupambana na umaskini, maradhi, ujinga, ukosefu wa ajira kwa vijana, uonevu, utetezi wa wanyonge na wasiojiweza, mapambano dhihi ya VVU/UKIMWI, ulinzi wa raslimali za taifa na kuhakikisha watanzania wanafaidika na urithi wao n.k.
HK amewahi kushika nafasi mbali mbali za uongozi kwenye chama chake, CCM (ambacho alijiunga rasmi mwaka 1994); amewahi kuwa chipukizi na kiongozi wa chipukizi wilaya ya Nzega, ameshiriki makambi mbalimbali ya vijana na halaiki, amewahi kuwa kijana wa Green Guard wa CCM, amewahi kuwa Mwenyekiti wa Vijana wa CCM, tawi la Kigoma Sekondari na Mjumbe, Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya Sikonge akiwawakilisha vijana. Kwa sasa ni Mjumbe, Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM, Mkoa wa Tabora, Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya Nzega na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa. Hajawahi kujiunga na chama kingine chochote kile cha siasa. Amewahi kushiriki kampeni mbalimbali za uchaguzi na kujitolea kwa hali na mali kujenga chama chake.
Dr. Kigwangalla ni mwandishi mzuri wa vitabu, makala za kisayansi na makala za uchambuzi wa mambo mbali mbali ya kisiasa na kiuchumi kwenye magazeti mbali mbali ya ndani na nje ya nchi.
Ni mwanamichezo, akipendelea zaidi kucheza soccer, basketball, tennis na Golf. Anapendelea mijadala ya wazi kwenye mitandao ya kijamii na ni mpenzi wa kusoma vitabu.
Dr. Kigwangalla ana mke na watoto watatu, Sheila, Hawa na HK Jr
No comments:
Post a Comment