Pages

Thursday, February 6, 2014

Kamati yakataa ripoti ya Jiji la Mwanza


Mwanza. Ripoti ya mapato na miradi ya maendeleo ya Jiji la Mwanza, imekataliwa tena na Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, baada ya ripoti hiyo kushindwa kufafanua jinsi mabilioni ya fedha yaliyotengwa kwa miradi ya maendeleo, yalivyotumuka.


Kukataliwa kwa ripoti hiyo kumempa wakati mgumu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Halifa Hida, ambaye amehamishiwa jijini hapa hivi karibuni.
Chini ya uenyekiti wa Dk Hamis Kigwangalla, kamati hiyo ya bunge licha ya kubaini matumizi mabaya ya fedha za miradi iliyokusudiwa, pia ilibaini kutokuwepo kwa umakini katika utendaji wa kazi wa maofisa wa Jiji la Mwanza, ambalo ni la pili kwa ukubwa nchini.
Kutokana na mkanganyiko huo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Kigwangalla alidai kuwa ripoti iliyotayarishwa kwa mara ya pili kama ilivyokuwa ya awali, haieleweki.
Akizungumza katika ukumbi wa halmashauri hiyo jana, Dk Kigwangalla alisema majibu yaliyotolewa baada ya taarifa ya awali kuhusu miradi mbalimmbali ya maendeleo, si ya kweli na kwamba yanaipotosha kamati.
Aliwataka watendaji kuandaa nyaraka zote za miradi ukiwemo ule wa ujenzi wa Kituo cha Biashara cha Kimataifa cha Mwanza.
“Kamati imesikitishwa sana na namna ya uandaaji wa taarifa ya halmashauri ya jiji hili, hii ni pesa ya umma inakuwaje mtu unakosea kujumlisha hesabu na kutoa takwimu ambazo si sahihi kabisa,” alihoji Dk Kigwangalla.

No comments:

Post a Comment