Pages
▼
Friday, March 21, 2014
Hotuba ya jk leo: Ni utulivu ama vurugu.............!!!!!!!!!!!
Leo ni siku ya Historia kuandikwa. maana ni siku ambayo ama mwanga utaonekana ama giza litatanda sana. Ni siku ambayo kila aliye na uhai katika taifa hili anatarajia ya kwake kutoka kwa Rais wa jamhuri ya Muungano wa tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete. Ni siku muhimu kwa JK yaani, ni karata yake muhimu ambayo ama ni ya ushindi ama ya kutuangusha. Na karata hiyo ni moja tu, nayo ni katika hotuba yake ya kulizindua Bunge maalum la Katiba Mjini Dodoma. Watu tuna matarajio mengi, lakini je atakidhi matarajio hayo katika hotuba hiyo? Au atatuacha tukiwa na njaa ambayo hatutajua ni nani, lini na kwa namna gani tutashiba? Tusubiri
Tanzania na watanzania tupo katika mchakato muhimu wa kutengeneza katiba mpya ya taifa itakayoiondoa ile ya mwaka 1977. kama taifa, si wa kwanza kufanya marejeo haya na kisha kuja na katiba kwa ajili ya mustakabali wa Tanzania. Katika miaka ya hivi karibunii tumeshuhudia nchi kadhaa ama kutengeneza katiba mpya kama ilivyofanyika Afrika Kusini (1996), Kenya 2010 na washirika wetu wa Jamhuri ya Muungano Zanzibar, 2010.
Kwa ujumla katiba ya kisasa iliyoandikwa, inatoa mamlaka maalumu kwa taasisi au mamlaka maalum zilizoanzishwa kwa masharti ya kimsingi ambayo yanakubaliana na mipaka ya katiba husika. Kwa mujibu wa mtaalam mmoja wa mambo ya katiba Scott Gordon, anasema "taasisi ya kisiasa ni ya kikatiba kwa kiwango ambacho ina mifumo ya kitaasisi yenye nguvu na mamlaka ya kulinda uhuru wa raia ikijumuisha wale wanaoweza kuwa katika makundi madogo madogo (minority groups) katika jamii." Hivyo katiba ndiyo sheria mama inayotoa maelekezo ya haki, wajibu, uhuru na usawa wa binadamu. Inatangaza mamlaka za serikali na namna zilivyo na wajibu wa kulinda raia wake na mali zao pamoja na kulinda misingi ya utaifa na kutunza tunu za amani, upendo, utu na mshikamano.
Historia ya dunia inatuonyesha wazi kuwa katiba zilikuwepo katika mataifa mbalimbali miaka mingi kabla ya kuzaliwa Kristo YESU. Hili linatupeleka mbali mwaka 621KK ambapo katika nchi ya Ugiriki kulikuwa na sheria kali iliyowalazimisha wananchi wa Jiji la Athens kuikariri. Mwaka 594KK utawala ulipobadilika mtawala mpya (Solon) aliandika katiba mpya (Written Solon Constitution).
Tutakuja na makala ya historia ya katiba katika makala zijazo, lakini kwa makala haya tutajaribu kuchambua tu yale ambayo ni matarajio ya wengi katika hotuba ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete leo atakapohutubia taifa katika uzinduzi wa bunge maalum la katiba. Katika ulimwengu uliostaarabika sasa (modern world), katiba ya India ndiyo katiba ndefu iliyoandikwa kuliko ya taifa lolote. Ina ibara 444 na sehemu 22 ikijumuisha majedwali 12 na imefanyiwa marekebisho mara 118. Katiba ya Marekani ndiyo katiba iliyoandikwa (written Constitution) ambayo ni fupi kuluko zote. Ina ibara 7 na imefanyiwa marekebisho mara 27 pekee. Kwa Tanzania, Katiba tuliyo nayo sasa (ya mwaka 1977), ina Ibara 152 zilizogawanywa sura 10 na imefanyiwa marekebisho mara 15. Rasimu ya Katiba tunayoishughulikia sasa ina ibara 271 ikiwa na sura 17 haina jedwali. Kiuhalisia, rasimu ina mambo mengi kuliko katiba iliyopo.
Hotuba ya Rais
Hotuba ya Rais leo ni ya Kihistoria. Hotuba yake inabeba uzito mkubwa maana ndiyo itatoa taswira halisi ya ni wapi tunakoelekea. Si mara ya kwanza kwa Rais kulihutubia taifa kuhusiana na masuala ya katiba, lakini kwa leo inaongeza umuhimu na unyeti maana atahutubia mbele ya wabunge wa bunge maalum la katiba ambapo kwa mara ya kwanza atahutubia Bunge, baraza la Wawakilishi na Wabunge Maalum wote kwa pamoja. Radha yake itakolezwa na uwepo wa viongozi wote wa kitaifa pamoja na viongozi wastaafu wa serikali ya Jamhuri ya Tanzania na wale wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Matarajio ya Watanzania kutoka katika Hotuba ya Rais
Kama ilivyo kawaida ya binadamu, kila mmoja huwa na shauku yake anapoona jambo fulani linakuja mbele yake hasa linapokuwa ni jambo zuri. Hakuna shaka kila mmoja wetu anatarajia Rais atakidhi matakwa ama yake binafsi, ama kundi la kijamii, kisiasa na kiutamaduni. Kwa mfano;
Vijana wanatarajia Rais atazungumzia masuala mtambuaka yawahusuyo wao hasa elimu na ajira. Wanatamani aweke msistizo kwamba liwe ni suala la kikatiba na kwa kuwa yeye ni Rais basi ana mamlaka tosha kuwezesha hayo yaingie katika katiba
Wanawake wanatarajia mengi kutoka kwa Mheshimiwa rais. Wapo wanaowaza Rais atasimamia suala la usawa wa kijinsia hasa katika utawala kufikia uwiano wa 50:50. Bado wanawaza labda atazungumzia hata uhamishaj na upokezanaji madaraka kwa kuzingatia jinsi.
Watoto wanatarajia azungumzie haki zao hasa afya na elimu, ambapo katika taifa ambalo watu wake kwa asilimia 50 wako chini ya miaka 17, basi haya wanayachukulia kama masuala nyeti rais ayaongelee leo.
Wazee wanamwangalia Rais kama mwokozi wao leo wakitarajia azungumzie haki za wazee na wajibu wa taifa kwa wazee. Wanalitazama suala lao kama ni nyeti ambalo ni budi likaingia katika katiba na Rais akalisemea.
Wapo wanasiasa na wasio wanasiasa wanaodhani na kuweka matarajio yao kwamba Mh. rais anakuja Bungeni, pamoja na kuzindua Bunge lakini anakuja kujibu hotuba ya Mwenyekiti wa Tume Maalum ya Katiba Mh. Jaji J.S. Warioba aliyoitoa jumanne wiki hii. Na kundi hili wanakwenda mbali zaidi kwa kuwaza kuwa Rais si muumini wa ama serikali tatu ama serikali moja, wanajua ni muumini wa serikali mbili na kwamba atatumia mamlaka yake kulisisitiza hilo.
Wapo wanaofikiria kuwa Rais katika hotuba yake atazungumzia masuala yaliyoleta mkanganyiko mwanzoni mwa Bunge hili hasa Posho. Na wengine wanategemea azungumzie msimamo ama kura ya siri au ya wazi.
Wapo wanaodhani, kwa kuwa Rais JK ni mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, basi leo anakuja kueeza msimamo wa chama kwa masuala yanayohusu muundo wa serikali, serikali, muundo wa muungano, na mambo yanayowasumbua. Lakini wapo wanaojiandaa kugomea hotuba ya Rais kwa maana anakuja kwa kazi moja tu, kumaliza Upinzani.
Makundi maalum yenye uwakilishi katika bunge hili maalum kila moja lina matarajio yake ambayo ama yanakinzana na kundi jingine (Mfano wakulima na wafugaji). Haya yote ni matarajio, na katika matarajio haya, ama zitakuwa Mbivu ama Mbichi.
Wataalam wa masuala ya Katiba nao wako katika kusubiri mwelekeo wa hotuba ya Rais kuona utaalamu wao unawekwaje, ama Rais ataonyesha dalili za kulikatisha Bunge na kuwarudishia wataalam, ama kuhitaji ushauri wa kitaalamu. Haya ni matarajio yao na wanaweza kudhani ni matarajio mapana kubeba mustakabali wa taifa.
Changamoto anazokabiliana nazo
Akiwa Kiongozi mkuu (CEO), Rais na Amir Jeshi Mkuu wa Taifa hili, hii ndiyo siku aliyopewa mtihani mkubwa ambao utamweka kwenye nafasi yake sawasawa kama kiongozi mwenye maono (vision), mwenye uwezo wa kuona mbali (foreseer) na mwenye uwezo wa kuenenda kwa kadri ya mahitaji ya Tanzania na Watanzania kwa ujumla wao na kupuuza matarajio na mahitaji ya makundi, mahitaji ambayo hayatakuwa na tija wala faida kwa taifa.
Changamoto nyingine ni kuwa anao wajibu unaomlazimisha kutimiza malengo na mtarajio yote ya watanzania kwa makundi yao ama bila makundi, waliopo bungeni na wasiokuwepo. Hii ndiyo dhamana kubwa aliyo nayo, ambayo si tu kuwa haitaleta mang'ung'uniko, bali itaweka misingi ya utekelezaji wa dhamira safi ya kufikia malengo na matarajio ya wengi
Changamoto ya tatu ni kuachana na matarajio yote ya makundi, watu mmoja mmoja na kila kila kitu, bali kuja na mambo yake ambayo Tanzania inatarajia kutoka kwa kiongozi mwenye maono.Changamoto hii ndiyo inayotarajiwa, ndiyo itaweka dira mwongozo wa taifa kuelekea miaka 50 ya uhuru, 150 hadi 200. Hatutarajii kuwa na katiba tutakayoifuta baada ya miaka ishirini au thelathin tu, bali. Katiba tuliyonayo ina umri wa miaka 37 tu tunaibadilisha. Tungetarajia Rais Kikwete asimamie kuhusu kuunda katiba hii.
Kwa Nini Changamoto hizi?
Kwanza ieleweke wazi kuwa Tanzania ni nchi changa ambayo inakuwa kwa kasi ikitishiwa na ongezeko kubwa la watu, ongezeko la watu mijini kwa miaka michache ijayo. Taifa lenye idadi ya watu milioni 49 karibu nusu ya watu wake ni watoto wenye umri chini ya miaka 15. Takwimu zinaonyesha, idadi kubwa ya watanzania ni watoto wa umri chini ya miaka 15 ambapo kati ya Watanzania milini 49, asilimia 44.8% (kiasi cha milioni 23) ni watoto chini ya umri wa miaka 15, na asilimia 64.2% wana umri chini ya miaka 25.Wastani wa umri Tanzania bado ni mdogo (miaka 17.3) ukilinganisha na nchi kama Namibia (37.2), Uholanzi (41.8) na Marekani 37.2. Ongezeko la watu Katika Miji na Majiji ni asilimia 4.77% huku hali ya utegemezi Tanzania ikiwa katika kiwango kikubwa ambacho ni asilimia 92.5% (Yaani sawa na watu milioni 45 si wazalishaji. Hii ni hatari). Ikiwa hakutakuwa na juhudi za makusudi, basi tujue taifa litaingia katika migogoro ya kiuchumi katika muda wa chini ya miaka 15 ijayo maana hakutakuwa na ajira, hakuna huduma za jamii na kiuchumi na miunddombinu ni tatizo. Hii ni changamoto ambayo taifa linamtarajia Rais kuligusa.
Huduma za afya kwa ujumla ni duni, taarifa za afya na huduma za afya vijijini bado ni kitendawili. Huduma za afya kwa Mama na Mtoto, uhakika wa lishe, maji safi na salama vijijini ni mdogo. Umbali kutoka mkazi wa mwisho hadi zahanati au kituo cha afya, hali ya huduma kule ziliko, changamoto ya UKIMWI na wastani wa umri wa kuishi (Life Expectancy), ni changamoto ambazo ni matarajio ya Tanzania.
Elimu bado ni kikwanzo: Pamoja na uduni wake, bado inatolewa kwa matabaka. Katiba ya sasa inatoa haki ya Elimu na Mafunzo, rasimu nayo pia inatoa haki hiyo lakini bado tuna changamoto za miundombinu. Katika taifa ambalo idadi kubwa ya watu wake ni watoto, elimu ni suala la msingi linalotakiwa kupewa kipaumbele.
Wito Wetu kwa Ujumla
Rais anao uamuzi hii leo;
Ama akidhi matarajio ya wale wenye hisi za kisiasa; jambo ambalo litazaa katiba yenye kero nyingi ambazo zitaanza kutusumbua hata kabla ya kumaliza mwaka mmoja. Kuwaudhi wanasiasa leo litakuwa ni jambo la heri kwa taifa maana wao hawatafurahi, lakini taifa litafurahi kwa kupata katiba bora.
Kuegemea nguvu zenye ushindani wa kichaguzi: Hii itakuwa ni hatari nyingine ambayo Rais ataliweka taifa Rehani maana atakuwa anawafurahisha wale wenye nguvu ya kuchagua na kuchaguana. Kuenenda na matarajio haya, tutaishia kuwa na katiba isiyokidhi matakwa ya Taifa kwa ujumla.
Mtazamo na Mwongozo wa Rais Mwenyewe: Yeye ndiye mkuu wa Taifa, Amiri jeshi Mkuu na Kiongozi Mkuu. Anao wajibu wa kuwa na maono kwa manufaa ya taifa. Uamuzi huu utakuwa na manufaa kwa taifa maana baada ya hapo hakuna mtu wala kikundi cha watu kitakachoibuka na kudai rais alikuwa upande wao, mwisho wa siku Bunge hili litakuja na Rasimu Bora kabisa.
Mwisho
Mwisho kabisa tumtakie rais wa jamhuri Afya njema na Misimamo thabiti iliyo na nia njema na dhamira safi ya kulilinda na kuliimarisha taifa hili.
Mungu Ibariki Tanzania
PAUL C. MAKONDA
MBUNGE MTEULE BUNGE MAALUM LA KATIBA - 2014
No comments:
Post a Comment