Pages

Wednesday, December 3, 2014

CAG Prof Mussa Assad Amesema ataanza Kazi kwa Moto Ule Ule.

Rais Jakaya Kikwete akibadilishana mawazo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Musa Assad (kulia) baada ya kumwapisha
Ikulu Dar es Salaam jana. Katikati ni Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib
Bilal. Picha na Anthony Siame wa Mwananchi

Dar es Salaam . Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) mpya, Profesa Mussa Assad amesema ataanza kazi kwa
moto uleule ulioachwa na mtangulizi wake, Ludovick Utouh
aliyestaafu.
Akizungumza jana mara baada ya kuapishwa na Rais Jakaya
Kikwete Ikulu, Profesa Assad aliyeteuliwa Novemba 5 kushika
wadhifa huo alisema: “Ninasubiri niingie ofisini nianze kazi…
nitaendeleza yote yaliyoachwa na mwenzangu, sitatoka nje ya
mstari.”
Profesa Assad alisema yuko tayari kusimamia utendaji kazi wa
kisasa kwa kusimamia misingi ya ofisi yake, ili kulinda hadhi na
heshima aliyopewa na Rais katika uteuzi huo.
Kuhusu Ripoti ya Akaunti ya Escrow, Profesa Asaad alisema
anasubiri kukabidhiwa rasmi taarifa hiyo na maagizo yote
yaliyotolewa na Bunge kwa ajili ya kutekeleza yale yaliyopo chini
ya ofisi yake na kuendeleza yale ambayo yalishaanza
kutekelezwa.
Alisema moja ya mambo ambayo atayafanyia tathmini na
kupatia majibu ni kutotajwa moja kwa moja katika Ripoti ya
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kama fedha za
Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa kwa pamoja na Tanesco
na IPTL ni za umma au vinginevyo.
Utoh anena
Akizungumza katika hafla hiyo, Utouh alisema kuwa
amemkabidhi Profesa Asaad ofisi yenye watendaji wanaofanya
kazi kwa ari na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.Alisema
amefurahishwa na uteuzi wake na kusema anaamini ataendeleza
uwajibikaji na umadhubuti wa ofisi hiyo kwa manufaa ya Taifa.
Utouh alimkabidhi Profesa Asaad mwongozo maalumu wenye
kurasa 78 na kueleza kwamba utampa mwelekeo wa namna ofisi
hiyo ilivyo na iwapo kuna upungufu yuko tayari kutoa
ushirikiano.
Spika Makinda
Akimzungumzia Profesa Asaad, Spika wa Bunge, Anne Makinda
alisema mtikisiko uliolikumba Taifa kutokana na Kashfa ya
Escrow umelifanya lijenge misingi mizuri zaidi ya kiutendaji na
uwajibikaji katika kuhakikisha matumizi mazuri ya fedha za
umma.
Alisema anaamini CAG mpya ataingia na mfumo wa kisasa zaidi
na kusaidia kuweka miundo bora zaidi ya kuhakikisha kunakuwa
na nidhamu ya hali ya juu katika kusimamia mapato na
matumizi ya Serikali.

No comments:

Post a Comment