Pages

Friday, September 30, 2016

MHE UMMY MWALIMU AWEKA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA WODI ZA WATOTO KATIKA HOSPITALI YA KANDA YA RUFAA MBEYA

MHE UMMY MWALIMU AWEKA JIWE LA MSINGI LA UJENZI WA WODI ZA WATOTO KATIKA HOSPITALI YA KANDA YA RUFAA MBEYA

* Aguswa na mchango wa Bodaboda katika kufanikisha ujenzi huo.

* Aeleza huduma za chanjo kwa watoto kuimarika kuanzia wiki ijayo

* Ujenzi wa Jengo la Uchunguzi (Diagnostic Centre) uliokwama kwa miaka 7, sasa kukamilika ndani ya mwaka mmoja.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Mb.) ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa *wodi za watoto* katika Hospitali ya kanda ya Rufaa Mbeya ambapo alieleza kuvutiwa na ushiriki wa Umoja wa BodaBoda katika kuchangia ujenzi wa wodi 3 za watoto katika Hospitali hiyo ambapo Bodaboda wamechangia mifuko 75 ya sementi katika hatua za awali ya ujenzi huo.

"Kwa niaba ya Serikali nawashukuru wadau wote waliochangia ujenzi huu ila niseme nimevutiwa sana na mchango wa Umoja wa Bodaboda Mbeya kwa kushiriki katika ujenzi huu.  Wamefanya jambo la zuri, jambo jema na la kizalendo katika kutatua changamoto za utoaji huduma za afya kwa watoto ktk Hospitali hii ya Rufaa ya Kanda inayohudumia mikoa 7 ya Tanzania Bara." Alieleza Mhe Ummy.

Mhe Ummy ametoa rai kwa jamii na makundi mengine ya jamii hasa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kuiga mfano huu mwema wa Bodaboda wa Mbeya na hivyo kuchangia kukamilisha ujenzi huu ili ifikapo January 2017 jengo hilo lianze kutumika na hivyo kupunguza mrundikano wa wagonjwa katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa Mbeya ambayo inahudumia mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Ruvuma, Songwe, Katavi na Rukwa.

Mhe Ummy ameipongeza Bodi ya Ushauri na Viongozi wa Hospitali ya kanda ya Rufaa Mbeya kwa jitihada walizochukua katika kutatua changamoto alizokutana nazo  wakati alipotembelea Hospitali hapo mwezi April 2016 ili kujionea hali ya utoaji huduma ambapo alikutana na kero ya wagonjwa kulala chini.  "Nimefurahi kuona Uongozi umeyafanyia kazi maagizo yangu. Nawapongeza sana. Na kwa kweli hawa ndio viongozi wa Taasisi za Afya tunaowataka katika awamu hii ya "Hapa Kazi Tu". Alieleza Mhe Ummy.

Waziri Ummy pia alitumia hadhara hiyo kueleza hali ya upatikanaji wa chanjo za watoto nchini ambapo alisema kuwa huduma za chanjo kwa watoto zitaimarika ndani ya wiki moja kuanzia leo kwa kuwa *dozi milioni 2 za chanjo za Kifua kikuu (BCG) na Pepopunda (TT) zitaingia nchini tarehe 3 Octoba* na *dozi milioni 2 za chanjo za Polio (OPV) tarehe 5 Octoba 2016*. Aliahidi kuwa mara tu chanjo hizo zitakapoingia nchini zitasambazwa mikoani mara moja.

Mhe Ummy pia alieleza jitihada za Serikali za kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi wa kanda ya nyanda za juu kusini ambapo Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa ujenzi wa jengo la Uchunguzi (Diagnostic Centre) lililokwamwa kwa takriban miaka 7 unakamilika ndani ya mwaka mmoja. Kukamilika kwa jengo hili kutaboresha utoaji wa huduma za uchunguzi wa magonjwa na hivyo kuwaondolea wananchi wa nyanda za juu kero ya kwenda Dar es salaam kwa ajili ya vipimo vya uchunguzi wa magonjwa kama ct scan. Pia Wizara imepanga kuhakikisha kuwa matibabu ya Saratani kwa njia ya dawa (Chemotherapy) yanaanza kutolewa katika Hospitali hii mwanzoni kwa mwaka kesho ili kuwapunguzia wananchi kero ya kwenda Taasisi ya Saratani ya Ocean Road iliyoko Dar es salaam.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa Jengo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya kanda ya Rufaa Mbeya, Dkt Godlove Mbwanji alieleza kuwa ujenzi wa jengo hilo unatokana na Fedha za ndani za Hospitali hiyo pamoja na michango ya wadau mbalimbali wa maendeleo ya Mbeya. Na kuwa jengo hilo litakuwa na vitanda 76 na hivyi kumaliza kabisa tatizo la wagonjwa kulala chini.

Kupitia hadhara hiyo Mhe Waziri Ummy aliwaagiza waganga Wakuu wa Mikoa, Wilaya na waganga wafawidhi wote wa Hospitali za Umma nchini kuhakikisha wanatumia vizuri rasilimali zilizopo katika  maeneo yao ili kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili utoaji huduma za afya kwa wananchi badala ya kusubiri fedha kutoka   Serikali kuu.

Mhe Ummy yupo Mkoani Mbeya kwa ziara ya Kazi ya siku 2 ambapo kesho atakuwa Mgeni Rasmi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yanayofanyika kitaifa Wilayani Mbarali.

Mh Ummy Mwakinu akifungua jiwe la msingi
Mh Ummy Mwalinu akizungumza na madaktari na manesi pamoja na wadau waliojitokeza hapo.
Mh ummy mwalimu waziri wa Afya akipeaba mkono wa pongezi.

No comments:

Post a Comment