Mbinu za kuishi zaidi ya miaka 100 zagunduliwa
Send to a friend
Sunday, 19 February 2012 10:30
0diggsdigg
Na Florence Majani
WAKATI taifa likikabiliwa na ongezeko la vifo vinavyotokana na maradhi, ajali na hata baadhi ya watu kujiua, wataalamu na wanasayansi nchini wametaja mbinu mbalimbali ambazo binadamu akizifuata, anaweza kuishi zaidi ya miaka 100. Wataalamu hao, kutoka vitengo mbalimbali vya Sayansi ya Jamii na Viumbe hapa nchini, wamesema mtu akiishi bila kuathirika akili na mwili, anaweza kuishi maisha marefu zaidi kuliko yule anayeathirika katika vitu hivyo. Wasomi hao wamebainisha kuwa mgawanyo wa mwili, akili na roho, ni mambo muhimu katika mwili wa mwanadamu yaliyo na uwiano unaoingiliana na havitenganishiki.
Kukabili msongo wa mawazo
Akizungumza na Mwananchi Jumapili, Mtaalamu wa Saikolojia na Mkuu wa Kitengo cha Sosholojia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Joyce Nyoni aliitaja mbinu ya kwanza ya kuongeza maisha kuwa ni kukabiliana na msongo wa mawazo. Daktari huyo alisema akili ya mtu huweza kuathiri mwili. Wengi wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na maradhi yanayotokana na msongo wa mawazo, kama vile maradhi ya moyo au vidonda vya tumbo. “Wengi wetu tuna msongo wa mawazo, jambo dogo linaweza kumfanya mtu akashindwa hata kula au kulala, ni lazima tujifunze kukubaliana na hali halisi ya maisha, huku tukiamini kuwa, hakuna jambo lisilo na utatuzi,” alisema Dk Nyoni.
Alisema wapo wanawake wengine ambao hupoteza maisha kwa sababu ya waume zao kuwatesa au kuwatelekeza. “Ni lazima tufahamu kuwa maisha hata siku moja hayawezi kunyooka, ni lazima viwepo vikwazo vya hapa na pale, kwa hiyo hatuna budi kujifunza kuzikabili changamoto za maisha,” alisema. Utafiti uliwahi kufanyika na kuonyesha kuwa, wanawake chini ya miaka 50 na walio katika kipindi cha kufunga hedhi, (menopause) ambao hawawezi kukabiliana na msongo wa mawazo, wanaugua maradhi ya moyo. Alisema yeye kama mtaalamu wa masuala ya saikolojia, huwashauri watu kutulia na kukubaliana na matokeo yoyote katika maisha.
Kuishi mfumo chanya, kucheka
Jambo lingine ambalo mtaalamu huyu alishauri ni kuishi katika mfumo chanya. Alisema watu wengi hawatosheki na kile kidogo wanachopata, badala yake wanaishi kwa kulalama jambo ambalo kwa asilimia kubwa, huchangia maradhi ya moyo. “Mara kwa mara huwa nawaeleza wanafunzi wangu, ukimwona mwanamke kavaa mikufu, bangili na hereni nyingi masikioni, vyote vya dhahabu, huyo ni mgonjwa, kwa sababu ukimnyang’anya au akiibiwa ujue ataugua,” alisema Dk Nyoni. Alisema, ni vyema watu waishi kwa kuridhika na chochote wapatacho, badala ya kutoridhika na hali yao na kutamani maisha ya wengine.
“Namthamini mwanamke anayetoka nyumbani, amechana nywele zake kawaida, amepaka mafuta, lakini anajiamini, kuliko yule ambaye anataka atazamike kuwa ni wa thamani na mwenye fedha, mbele za watu, kwa kuvaa nguo za thamani kubwa au kuendesha magari ya kifahari,” alisema .Mtaalamu huyo alitaja mbinu nyingine ya kurefusha maisha kuwa ni kucheka au kuwa na furaha
Mazoezi, usingizi wa kutosha
Naye Dk Nandera Mhando, wa Kitengo cha Sosholojia na Athropolojia cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema hakuna ubishi kuwa zipo tabia ambazo husababisha baadhi ya watu kukumbwa na maradhi na kufa katika umri mdogo. “Wapo ambao hawana kabisa tabia za kufanya mazoezi, hawa huwa na uzito mkubwa na miili yao inapokuwa na mafuta mengi, maradhi ya moyo huwa yamepata nyumba, lakini pia kutopata usingizi wa kutosha nalo ni tatizo,” alisema.
Tabia ya mtu, vyakula
Dk Mhando alisema, tabia ya mtu ni sababu nyingine inayoweza kumfanya mtu awe na maisha mafupi, kwa mfano, kupenda kufanya ngono, kuvuta sigara, na ulevi ni mambo yanayosababisha maradhi na kuleta kifo.
“Kama mtu tayari ameathirika, halafu anandelea kufanya ngono kwa kiasi kikubwa, si ajabu mtu huyo kufa mapema, lakini wanaokunywa pombe na kuvuta sigara kwa wingi, nao mara nyingi huugua maradhi ya figo, mapafu, ini nk.,” alisema. Daktari huyu aliongeza kwamba, aina za vyakula tunavyokula nayo vinachangia kupima afya ambayo kimsingi ni kipimo cha maisha ya binadamu.
Alisema wanaokula vyakula asilia, kama mboga za majani, kunywa maji na kula matunda kwa wingi, si rahisi kushambuliwa na maradhi, tofauti na wanaokula wanga peke yake ambao wanakuwa katika hatari ya kupata maradhi, hatimaye kifo. Imethibitishwa kuwa, Mwanabaolojia mmoja, wa nchini Marekani, Ancel Keys, hata baada ya kustaafu, aliendelea kufanya kazi za bustani nyumbani kwake kwa kiasi kikubwa jambo lililomfanya kuishi miaka 100. Alifariki mwaka 2004.
Dini
Mtaalamu wa Sosholojia ya Dini kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Thomas Mwendaluka, alisema, dini ni moja ya maeneo ambayo huweza kuchangia mtu kuishi maisha marefu.
“Dini ina pande mbili, hasi na chanya, kwa sababu kwa upande mmoja inatoa tumaini. Inamsaidia mtu kiimani kuishi maisha marefu na vilevile ni chanzo cha kufupisha maisha,” alisema Mwendaluka. Alisema, watu huweza kujengwa kiroho na kuamini uponyaji wa magonjwa yaliyoshindikana. Kwa mfano tangu UKIMWI ulipoingia , waathirika wengi wamekimbilia katika taasisi za dini na kule hujengwa kiroho na kiimani na kujisikia wamepona na kuongeza siku za kuishi. “Lakini baadhi ya imani, kwa mfano Boko Haram, zinawataka waumini wajitoe muhanga kuua, hilo hufupisha maisha ya wengi,” alisema Mwendaluka. David Larson, Mshauri wa Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili wa nchini Marekani, alifanya utafiti wake mpana juu ya uhusiano wa moja kwa moja uliopo kati ya dini na afya.
Uchunguzi wake ulionyesha wazi kwamba upo uhusiano wa moja kwa moja kati ya muumini aliyejitoa kwa moyo katika imani husika na afya yake. Alishangaa kubaini kwamba, wale wanaohudhuria kanisani wanaishi muda mrefu kuliko wale wasiohudhuria. “Nilishangazwa kujua kuwa kutumainia uweza wa Mungu ndio msingi wa ustawi wa kweli na maisha ya afya yenye furaha,” alisema Larson.
Kunywa maji mengi
Daktari wa Kitengo cha Patholojia katika Hospitali ya Muhimbili, Innocent Mosha anasema maji ni jambo lingine linaloweza kukupa afya na kukuepusha na maradhi. “Kazi ya maji ni kusafisha ini na figo, kwa hiyo si ajabu mtu asiyekunywa maji ya kutosha akawa na afya mbaya kwa sababu uchafu hubaki katika damu,” alisema Dk Mosha. Matabibu wengi wanashauri kuachana na aina za vyakula kwa mfano, nyama ya wanyama yenye mafuta ya majimaji (saturated fat) na mafuta mazito (cholesterol), ambavyo huongeza hatari ya kupata shinikizo la damu, kupooza
(stroke), ugonjwa wa moyo, kansa, unene usio wa kawaida, kisukari na magonjwa mengineyo. Mwandishi wa kitabu cha ‘The Blue Zones’ Dan Buettner, ambaye alifanya utafiti kuhusu siri ya ya kuishi maisha marefu katika nchi za Bara la Australia, Greece na China, aligundua kuwa, watu wa nchi hizo wana tabia za kufanana ambazo bila shaka huwafanya waishi maisha marefu. Alisema wote hula milo yenye kiasi kidogo cha nyama na wanafanya mazoezi. Mwisho…
Post a Comment