STAA wa Taifa Stars, Mbwana Samatta Poppa, amelilia bahati ya wachezaji wenzake wa timu ya TP Mazembe, Stoppila Sunzu na Rainford Kalaba ambao timu yao ya taifa la Zambia, iliifunga Ivory Coast katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika, mapema mwaka huu.
Samatta anayecheza na nyota hao katika timu hiyo ya Jamhuri ya Kidemekrasia ya Congo anatarajiwa kuongoza mashambulizi ya Taifa Stars leo Jumamosi kwenye mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia.
Mechi hiyo itafanyika katika Uwanja wa Felix Houphet-Boigny jijini Abidjan. Anaamini kuwa wenzake Sunzu na Kalaba walikuwa na bahati kuichapa Ivory Coast kwa matuta jijini Libreville, Gabon na ana matumaini atafuata nyayo zao.
�Kaka sikia, wale akina Sunzu na Kalaba walikuwa na bahati kuichapa Ivory Coast. Hata mimi nahitaji bahati hiyo kwa sababu jamaa (Ivory Coast) wametimia sana. Lakini tumuombe Mungu tu kwani hakuna kisichowezekana,� alisema Samatta, ambaye anatazamiwa kucheza nafasi ya mshambuliaji wa kati.
Samatta alisema alizungumza na Sunzu na Kalaba kuhusu uwezekano wa kuifunga Ivory Coast kama wao walivyofanya, lakini amekiri kwamba mazingira ya mechi hii ni tofauti na ya akina Kalaba.
Katika pambano hili, Samatta anatarajiwa kushirikiana na mshambuliaji mrefu, John Bocco ambaye katika mazoezi ya juzi Alhamisi mara tu baada ya kutua jijini Abidjani, kocha Kim Poulsen aliwapanga kwa pamoja.
Mrisho Ngassa, amekuwa akipewa mazoezi ya kufanya mashambulizi ya kushtukiza katika lango la Ivory Coast akitokea upande wa kushoto ambako beki wa kulia wa Ivory Coast ni nyota wa zamani wa Arsenal, Emmanuel Eboue, ambaye kwa sasa anachezea Galatasaray ya Uturuki.
Post a Comment