Home »
siasa
» TAARIFA ALIYOITOA MP JOHN MYIKA KWA VYOMBO VYA HABARI...!!!
TAARIFA ALIYOITOA MP JOHN MYIKA KWA VYOMBO VYA HABARI...!!!
MP wa Ubungo, John Mnyika
Ameanza kwa kusema haya...!!
"Awali ya yote niwatikie nyinyi wanahabari kheri ya sikukuu na kupitia
kwenu nifikishe salamu kwa ndugu zetu waislam na watanzania wote katika
kuadhimisha Iddi Ell-Hajj.
Tarehe 15 Oktoba 2012 nilitoa taarifa
kwa umma kuwa niliwasilisha kwa Katibu wa Bunge kusudio la kuwasilisha
Muswada Binafsi wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii (The Social Security Laws (Ammendments) Act wa mwaka 2012 kwa
hati ya dharura kwa mujibu wa Kanuni ya 81 ya Kanuni za Kudumu za Bunge
(Toleo la Mwaka 2007) iwapo Serikali haitatoa kauli kwa umma ya ratiba
ya kupata mapendekezo toka kwa wadau wa hifadhi ya jamii pamoja na
kamati husika ya kudumu ya Bunge na kuwasilisha muswada husika bungeni
kama ilivyoazimiwa bungeni tarehe 6 Julai 2012.
Kufuatia hatua
yangu na hatua za wadau wengine Serikali kinyume na msimamo wa awali
ambalo ulielezwa na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira Makongoro Mahanga
tarehe 14 October 2012 ambaye alieleza kuwa marekebisho ya kurejesha fao
la kujitoa hayatafanyika mpaka mkutano wa kumi wa Bunge mwezi Februari
mwaka 2013; Serikali imechapa katika gazeti la Serikali Muswada wa
Marekebisho ya Sheria Mbalimbali na. 40 Juzuu namba 93 ambao katika
sehemu ya 6 vifungu vya 13, 14 na 15 imependekeza kurejesha fao la
kujitoa kwa upande wa mfuko mmoja wa mashirika ya umma (PPF) hata hivyo
muswada huo haujawasilishwa kwa hati ya dharura kama ilivyoazimiwa na
kuahidiwa.
Kwa upande mwingine, sehemu hiyo ya sita ya muswada
huo wa marekebisho ya sheria mbalimbali haijakidhi mahitaji na matakwa
ya azimio la bunge la tarehe 6 Agosti 2012 lililoungwa mkono na wabunge
katika kikao cha 41 cha Mkutano wa Nane wa Bunge na itasababisha mgogoro
mwingine katika ya serikali na wafanyakazi kwa upande mmoja,
wafanyakazi na waajiri kwa upande mwingine na kuathiri uchumi wa nchi na
maisha ya wafanyakazi katika maeneo mbalimbali nchini kwa kutoresha fao
la kujitoa katika mifuko mingine ikiwemo NSSF, PSPF na LAPF.
Kwa kuzingatia kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara
imeeleza kuwa Rais ndiye mkuu wa Nchi na Kiongozi wa Serikali na Ibara
ya 34 imeeleza kwamba mamlaka yote yapo mikononi mwake na kwamba
madaraka hayo yanaweza kutekelezwa na watu wengine kwa niaba yake na
kwamba Ibara ya 35 imeeleza bayana kwamba shughuli zote za serikali
zitatekelezwa na watumishi wa serikali kwa niaba yake; wakati umefika
sasa wa wafanyakazi na wadau wengine kuchukua hatua za kuwezesha Rais
kuingilia kati kabla ya mkutano wa Bunge kuanza tarehe 30 Oktoba 2012
kutumia madaraka na mamlaka yake kuondoa udhaifu uliojitokeza wa Waziri
wa Kazi na Ajira Gaudencia Kabaka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Fredrick
Werema na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii (SSRA) Irene Isaka kutokutekeleza kwa wakati na kwa ukamilifu
mapendekezo na maamuzi ya Bunge pamoja na ahadi za Serikali kwa wabunge.
Mosi; Rais azingatie masharti ya Kanuni za Kudumu za Bunge na kutia
saini hati ya dharura ya kuwezesha muswada wa marekebisho ya sheria
mbalimbali wenye vifungu vya nyongeza vinavyowezesha fao la kujitoa
kurejeshwa kwa mifuko yote ikiwemo NSSF, PSPF na LAPF kuwasilishwa
bungeni. Kanuni ya 80 Fasili ya 4 inaelekeza kwamba “Muswada wowote wa
sheria wa Serikali wa dharura hautaingizwa kwenye shughuli za Bunge bila
ya kuwa na hati iliyowekwa saini na Rais inayoelekeza kuwa muswada
uliotajwa kwenye hati hiyo ni wa dharura”.
Iwapo Rais hataweka
saini hati ya dharura au Serikali haitawasilisha bungeni hoja kwa
mujibu wa Kanuni ya 93 fasili ya 4 bunge litabanwa na fasili ya 1 ambayo
inakataza bunge kushughulikia hatua zaidi ya moja katika mkutano mmoja
wa bunge; tafsiri yake ni kwamba sheria hii itasubiri kupitishwa katika
mkutano wa kumi wa Bunge mwezi Februari 2012 na hivyo wafanyakazi
kuendelea kunyimwa mafao ya kujitoa kinyume na azimio la Bunge.
Pili, Rais atengue tangazo na agizo la Mamlaka ya Udhibiti wa Hifadhi
ya Jamii (SSRA) kueleza kuwa “kufuatia kuanza kutumika kwa Sheria hiyo
(ya 13 Aprili 2012) maombi mapya ya kujitoa yamesitishwa kwa kipindi cha
miezi sita hadi pale miongozo itakapotolewa ili kuwezesha Mamlaka na
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa elimu kwa Wadau” ambalo limesababisha
mifuko yote kuacha kutoa mafao ya kujitoa hata kwa wafanyakazi .
Hii ni kwa sababu marekebisho ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii
kwa upande wa kusitisha fao la kujitoa yaliyofanyika tarehe 13 Aprili
2012 yalihusu zaidi Mfuko wa Mashirika ya Umma (PPF); hivyo hayakupaswa
kabisa kutumika kama sababu ya kusitisha mafao kwa mifuko yote ikiwemo
NSSF, PSPF na LAPF na kwa upande mwingine wafanyakazi wanaodai mafao
hayo kabla ya kujiunga na mifuko hiyo walijiunga wakiwa wameelezwa kama
kati ya haki na stahili zao ni pamoja na kupata fao la kujitoa mazingira
yakilazimisha hivyo kabla ya pensheni ya uzeeni. Hivyo, kusubiriwa kwa
marekebisho ya sheria hakupaswi kuwa kisingizio cha kuendelea kusitisha
mafao yao ya kujitoa, ama sivyo Rais aeleze sababu za ziada za kuzuia
mafao ya kujitoa kwa kuzingatia Taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali juu
ya uendelevu wa mifuko katika siku chache zijazo kufuatia kushindwa kwa
makampuni na Serikali yenyewe iliyokopeshwa na mifuko ya hifadhi ya
jamii kuheshimu matakwa ya malipo ya mikopo kutoka mifuko husika ambayo
fedha zake zinatokana na makato ya pensheni toka kwa wafanyakazi na
waajiri.
Rais arejee kumbukumbu rasmi ya Bunge (Hansard) ya
tarehe 7 Agosti 2012 za kikao cha 42 cha Mkutano wa Nane wa Bunge ambao
nilishika mshahara wa Waziri Bunge lilipokaa kama kamati na “nilitaka
ufafanuzi wa kisera wa Serikali pamoja na uamuzi wa kuahidi kwamba
kwenye mkutano wa Bunge ujao italeta Muswada wa dharura kuhusiana na Fao
la Kujitoa, nilitaka kauli ya Serikali juu ya agizo lilitolewa na SSRA
la kusitisha utoaji wa mafao ya kujitoa katika kipindi hiki cha miezi
sita (6) na kuhusiana na wafanyakazi waliosimamishwa katika hatua ya
kudai hayo mafao.
Sasa iwapo Wizara inatoa kauli ya kutengua
sitisho hilo na vilevile inatoa kauli ya kutaka kurejeshwa kwa
wafanyakazi waliosimamishwa katika hatua ya madai ya fao hili la
kujitoa”. Waziri wa Kazi na Ajira alijibu kuwa “tutalifanyia kazi agizo
hilo”, hata hivyo mpaka sasa agizo hilo la SSRA halijatenguliwa na
wafanyakazi waliosimamishwa wengine hawajarudishwa mpaka hivi sasa na
baadhi wamefukuzwa kazi kabisa kutokana na mgogoro uliosababishwa na
Serikali kusitisha fao la kujitoa bila kuzingatia haki za binadamu,
mazingira ya ujira nchini na ushirikishwaji wa wafanyakazi na wadau
wengine muhimu wa hifadhi ya jamii."
Wenu katika utumishi wa umma,
John John Mnyika (Mb)
26/10/2012
Hayo nimaneno ya MP Mnyika
Post a Comment