"Tusisubiri CNN Waiambie Dunia Mchango Wa Tanzania Kwa Ukombozi Wa Afrika...!
Kazi hiyo tuifanye sisi wenyewe. Jana usiku sana nilimwona Rais wa
Ghana John Dramani Mahama akihojiwa na CNN kuhusiana na Mandela. Mara
tatu Rais huyo wa Ghana aliutaja mchango wa Tanzania katika ukombozi wa
Afrika ikiwemo Afrika Kusini ya Nelson Mandela.
-Hivi ni
wangapi wanajua kuwa kiongozi wa kwanza wa chama cha ukombozi katika
nchi huru ya Kiafrika ambaye Mandela alikutana nae anaitwa John Mwakangale. Huyu alikuwa kiongozi katika TANU na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
-Hivi ni wangapi wanajua kuwa Mji wa kwanza katika nchi huru ya
Kiafrika ambayo Mandela alikanyaga ardhi yake unaitwa Mbeya. Hivyo basi,
Tanganyika ndio nchi huru ya kwanza ya Kiafrika ambapo Mandela
alikanyaga ardhi yake.
- Hivi ni wangapi duniani wanajua, kuwa
Julius Nyerere ndiye Rais wa kwanza katika nchi huru ya Kiafrika ambaye
Mandela alikutana nae. Na ni Julius Nyerere baada ya kumkubali Mandela,
ndiye aliyemsaidia Mandela kwa kumtambulisha kwa Mfalme Haille Selassie
wa Ethiopia?
Haikuwa ajabu, kuwa baada ya kutoka gerezani, kwa Mandela Tanzania ikawa nchi ya kwanza kuitembelea.
Kumbukumbu hizi muhimu za kihistoria na nyinginezo Watanzania hatupaswi
kuisubiri CNN na vyombo vingine vya habari vya kimagharibi viitangazie
dunia.
Ni jukumu letu wenyewe".
Post a Comment