Jamhuri: Pinda agongana na bilionea Dar!
- Ni Ally Awadh wa kampuni ya mafuta ya Lake Oil
- Atuhumiwa kumfanyia unyama mtumishi wake
- Polisi Oysterbay, Kanda Maalumu wamgwaya
Mlalamikaji anayedaiwa kupigwa na mabaunsa wa mfanyabiashara bilionea Ally Awadh (Lake Oil)
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ameamua “kujipima uzito” dhidi ya bilionea
Mtanzania, Ally Edha Awadh ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Lake Oil ya
Mikocheni jijini Dar es Salaam inayoagiza, kuuza na kusafirisha mafuta
na biashara nyingine nyingi.Awadh anayetajwa kama mmoja wa mabilionea
vijana nchini, amefunguliwa mashitaka Polisi ya kumteka, kumdhalilisha
kinyume cha maumbile na kumpora mali mmoja wa wafanyakazi wake.
Uamuzi wa Waziri Mkuu Pinda umekuja baada ya Jeshi la Polisi nchini,
katika kile kinachoonekana ni kumgwaya bilionea huyo, kupuuza kumsaidia
mlalamikaji huyo mwenye umri wa miaka 32. Kwa sababu za kiutu na za
kitaaluma, jina la mlalamikaji tunalihifadhi kwa sasa.
Hatua ya Pinda imetokana na barua ya mlalamikaji ya Novemba 29, mwaka
jana aliyomwandikia baada ya Jeshi la Polisi-kuanzia Kituo cha
Oysterbay, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na hata Makao Makuu, kupuuza
kumsaidia mlalamikaji ili aweze kutendewa haki.
Baada ya kuipata barua ya mlalamikaji, Pinda alimwagiza msaidizi wake,
Leila Mgonya, amwandikie barua Katibu wa Waziri wa Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi. Kazi hiyo ilifanywa Desemba 29, mwaka jana.
Katika barua hiyo ya Pinda iliyoandikwa kwa niaba yake na Mgonya,
inasema, “Miongoni mwa mambo aliyofanyiwa mlalamikaji na mwajiri wake
(Awadh) ni pamoja na kupigwa na kujeruhiwa mwili mzima kama picha
zilizoambatanishwa na barua ya mlalamikaji zinavyoonyesha, kudhalilisha
pamoja na kudhulumiwa mali zake kama inavyobainishwa katika barua ya
mlalamikaji.
“Kwa kuwa suala hili limejikita zaidi katika utendaji wa Jeshi la
Polisi, imeelekezwa kuwa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ishughulikie
suala hili kikamilifu kwa lengo la kumsaidia mlalamikaji kupata haki
yake kwa mujibu wa sheria na kuona kuwa haki inatendeka.
“Aidha, Mheshimiwa Waziri Mkuu angependa kupata mrejesho kuhusu suala
hili. Tafadhali mfikishie Mheshimiwa Waziri maelekezo hayo ya Mheshimiwa
Waziri Mkuu.”
Pamoja na maagizo hayo ya Waziri Mkuu, JAMHURI imebaini kuwa hakuna
hatua zozote za maana zilizokwishachukuliwa dhidi ya Awadh na washirika
wake.
Barua ya mlalamikaji kwa Waziri Mkuu
Mlalamikaji katika barua yake kwa Waziri Mkuu, anaanza kwa kusema,
“Mheshimiwa, jina langu lipo hapo juu ni kijana wa Kihidi (Mtanzania)
umri wangu ni miaka 32 mzaliwa wa Tanga, nina mke na watoto.
“Mheshimiwa, nimesomea uhasibu na nimefuzu mwaka 2004 masomo yangu… na
nikaajiriwa na Ally Edha Awadh katika kampuni yake iitwayo Lake Oil Ltd
Septemba, 2010 na kuwa Finance Manager (Meneja Fedha) katika kampuni
yake.
“Bila matarajio yangu, ilipofika Mei 2, 2013 mwajiriwa mwenzangu aitwaye
Ahmed alifika ofisini kwangu na kuniarifu ya kwamba naitwa na
Mkurugenzi Ally Edha, ilikuwa saa 11:30 za jioni Alhamisi na bila kusita
nikaongozana naye hadi kwa Ally Edha nikifahamu naitwa kwa ajili ya
kazi kiofisi.
“Nilishangaa nilipofika tu ofisini kwake akahitaji simu yangu, nikampa
mara akamuagiza stafu mwingine aitwe Fahim akafuate laptop yangu na
vifunguo ya gari yangu ofisini kwangu na ofisini kwake tulipobaki mimi,
yeye na Ahmed. Alianza kunitukana na kuniambia mimi ni mwizi nimemwibia
dola milioni 10 za Marekani (Sh bilioni 16).
Mara ilipoletwa laptop yangu na funguo za gari akanichukua na kuniagiza
nimfungulie e-mail yangu. Nilikataa na kumwambia hii ni mail yangu
binafsi na siyo ya ofisi yake, siwezi kufungua pana kazi za wateja wangu
wengine (mimi ni mhasibu wa wengi). Akanitishia kunipeleka Polisi, nami
nikamkubalia.
“Mheshimiwa, tukifuatana na wafanyakazi wake wengine, Ahmed, Fahim, yeye
na K.V Choudry, tulishuka chini na kuingizwa katika gari ya Ahmed. Gari
ikawashwa na mara akamuagiza dereva Ahmed lile gari tulilopanda
lipelekwe godown (ghala) ili abadilishe gari kwenda Polisi. Cha
kushangaza nikaamrishwa nishuke pale godown na kuingizwa ndani, pamoja
na wale tuliofatana nao. Nilishangaa kuwakuta wengine wawili (yeye Ally
Awadh anadai ni mabaunsa wake) wanaitwa Waitey na mwingine ni Abeid.
Mabaunsa waanza kumlawiti
“Mheshimiwa, wakajumuika pamoja wakanivua nguo, wakanilawiti. Wakanipiga
sana kwa kutumia nondo, mikanda mizito, makonde ya nguvu na huku huyo
mtumishi mwenzangu Ahmed akiwa ameielekeza pistol (bastola) kichwani
kwangu kwa kuniambia leo ni kifo changu endapo nitakataa kuyakubali
anayotaka bosi wake, yaani Ally.
“Mheshimiwa, mateso haya yalikuwa zaidi ya masaa mbili na nusu (zaidi ya
saa mbili na nusu) nikilazimishwa nikubali kutoa kila kitu changu
(assets) nimpatie yeye, vinginevyo wataniua na wakanionesha picha za
maiti wawili zilizokuwepo katika simu ya baunsa wake akidai (Ally)
angeniua kama hao, na kunifunga katika mfuko wa plastiki na kunipeleka
shambani kwake Soga kunizika.”
Mlalamikaji anaendelea kumweleza Waziri Mkuu kwamba kutokana na mateso
makali na vitisho alivyopewa, alilazimika kukubaliana na maelekezo
aliyopewa, yote hiyo ikiwa ni mbinu ya kunusuru uhai wake.
Apigwa picha akiwa uchi
“Ndipo Ally Edha akanipiga picha nikiwa uchi na kusema endapo nitaenda
Polisi, yeye atazitoa hizo picha kwenye mitandao ya intaneti
kunidhalilisha. Hivyo nikapewa shati langu nivae na kupelekwa ofisini
kwake na kulazimishwa niandike kukubali kwamba vitu vyangu vichukuliwe,”
anasema.
Mlalamikaji anayedaiwa kupigwa na mabaunsa wa mfanyabiashara bilionea Ally Awadh (Lake Oil)
Kwa mujibu wa mlalamikaji, mali zilizochukuliwa ni:
A: Nyumba yangu na mke wangu iliyopo Nairobi, Kenya
B: Gari zangu mbili (i) Toyota IST T786 BZG (ii) Toyota Fortuner T503 BQC
C: Bastola yangu 6mm niliyonunua Mzinga.
D: Fedha taslimu dola 100,000 (Sh zaidi ya milioni 160)
E: Mkataba wangu wa nyumba na duka (vyangu) vilivyoko Uhuru Heights
F: Ofa zangu tatu za viwanja Kigamboni
Asainishwa kwa nguvu
“Ndipo nikasainishwa; na majira ya saa 3 za usiku wakanitia katika gari
aina ya Navara nyekundu mali ya kampuni –dereva akiwa Ahmed wakiwamo
mabaunsa wawili, Ally Edha, na mimi. Hadi nyumbani kwangu Upanga.
“Mheshimiwa, inasikitisha kwa sababu mke wangu alipopiga simu nikiwa kwa
Ally alinilazimisha niongee na mke wangu kwa lugha ya Kiingereza, na
siyo Kihindi. Alikuwa anapiga kwa kutoamini kwa nini niongee Kiingereza
badala ya Kihidi hadi simu ikaisha pesa ndipo tulipofika tukamkuta yupo
chini anangoja aletewe vocha na mlinzi.
“Wakanibadilisha shati na kunivisha la Abeid (langu lilijaa damu).
Wakamweka chini ya ulinzi mke wangu. Tukapanda juu nyumbani hadi sitting
room wakamnyang’anya simu na kumkalisha chini. Ally Edha akanilazimisha
nimpeleke bedroom (chumba cha kulala), ndiye akazichukua documents
(nyaraka) zote na hizo pesa na mara wakaingia Choudry, Sree Kumar na
Ramana ambao wote ni wafanyakazi wake; na ni Wahindi wakiwa na laptop na
printer.
“Ghafla wakiwa na hizo laptop huyo Choudry na Kumar wakaelekezwa
kuandika maneno ya mkataba ambayo mimi na mke wangu tukalazimishwa
kuweka sahihi zetu kukubali kuzitoa mali zetu kwa huyo jambazi Ally.
Nakumbuka hata watoto wanalia kutaka maziwa nyumbani Ally Edha alizuia
wasipewe.”
Mlalamikaji anaendelea kusema kwamba akiwa na maumivu makali, Ally Edha
alitaka siku ya pili amtolee pesa katika akaunti yake iliyopo katika
Benki ya STANBIC, Tawi la Nyerere Road; na akasema angezifuata hizo
fedha siku ya Jumamosi.
“Alizijua hizo fedha kwa sababu ni akaunti niliyoitumia kuweka pesa za
mshahara. Mshahara wangu ulikuwa Sh. milioni 6 kwa mwezi. Kama hilo
halikutosha, alikuta chumbani kwangu vitabu vitatu vya hundi za akaunti
ya pamoja na mke wangu; Standard Chartered (Nairobi, 2), Benki ya Exim
(3), Benki ya NBC, akatulazimisha tuzitie sahihi zetu- na tukafanya
hivyo.”
Mlalamikaji, mkewe waonywa watauawa
“Siku hiyo aliniambia mimi na mke wangu kwamba kama angesikia
tumemueleza mtu yeyote haya mambo, angetuua. Kweli tukaogopa sana hadi
siku ya tarehe 4, 2013 ndipo alipomtuma Sree Kumar kuja kuchukua zile
milioni 22 alizoagiza nizitoe katiba akaunti yangu ile siku ya tarehe 2
Mei 2013. Nilimkabidhi Sree Kumar akampelekea Ally Awadh.
“Mheshimiwa, nakumbuka namna tarehe 8 Mei, 2013 Choudry (Mfanyakazi wa
Ally Awadh) alinitumia meseji mbili kwa kutumia simu yake kwamba
angependa aje nyumbani waniletee pochi waliyochukua siku ya tukio
nyumbani kwangu ambayo ni ya mke wangu yenye kadi yake ya ATM na kopi ya
leseni ya udereva. Nikawaambia sitokutana nyumbani, tukapanga anikute
Mtaa wa Morogoro/Jamhuri akaleta akanikabidhi bila ya kunisalimu.”
Danadana za Polisi Oysterbay
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, siku ya Jumamosi tarehe 4 Mei 2013 nilipatiwa
wakili aitwaye Mwanganga. Nikamueleza, akaamua tukamuone RPC Kova
(Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam). Tulifika saa za mchana,
nikamueleza na nilipotaka kumwonyesha majeraha yangu alikataa na kusema
kuangalia majeraha sio kazi yake ila alipiga simu Oysterbay akatuagiza
twende. Tukafuatana na wakili hadi Oysterbay.
“Mheshimiwa, hiyo tarehe 4 Mei 2013 tulifika Oysterbay tukamuona ofisa
mmoja simfahamu jina ila sura namfahamu (wakili wangu anamfahamu).
Hakuonekana kujali sana, ndipo akatupeleka ofisi nyingine (wakili
anaifahamu). Hapo huyo askari akamuita mama mmoja polisi ndipo
akatupeleka ofisi nyingine, ofisa akamuagiza andike maelezo naye
akanisikiliza na akanipeleka kwa ofisa mwingine. Huyo ndiye aliandika
maelezo yangu.
“Cha kushangaza huyo ofisa alianza kusema ‘wewe tayari umetajwa kwenye
kesi nyingie ya Lake Oil’, lakini tukamwambia aandike maelezo yangu.
Yeye alidai ‘pana Mhimdi mmoja, Mukesh ambaye ni Internal Auditor
(Mkaguzi wa Ndani) wa Lake Oil yupo ndani rumande hapo, na wewe pia
unapaswa uwekwe ndani’. Lakini huyo ofisa na mwanasheria wangu walitoka
nje. Cha kunishangaza wakili akanimbia eti inatakiwa niweke dhamana
nikatibiwe ili Jumatatu nirudi au nipelekwe kutibiwa nirudishwe rumande.
Lakini wakili baadaye alinifahamisha wameyamaliza- kampatia Sh 100,000;
hivyo ningepaswa nimrejeshee hizo pesa.
“Hivyo statement (maelezo) iliandikwa na nikapewa medical examination
report yenye case file no. OB/RB/7853/2013 ya tarehe 4 Mei, 2013. Ndipo
nilipoenda Sinza Hospitali kwa matibabu.”
Woga wamfanya akimbilie Zanzibar
Mlalamikaji anasema kutokana na woga wa ahadi za mateso zaidi au kuuawa
kama alivyoahidi Awadh, aliamua Mei 5 aende mafichoni Zanzibar.
“Tarehe 6 Mei nilipigiwa simu na Mutafungwa aliyejitambalisha kwangu
kwamba yeye ni OCD wa Kinondoni akisema amesikitishwa kuisoma statement
yangu na angependa kukuona. Hivyo nikarejea Dar es Salaam na tarehe 7
Mei nikaenda na kaka yangu na wakili wangu. Tukamwona, akaagiza kwa
ofisa mwingine wa CID kumweleza hiyo kesi ni ya ukweli kwa hiyo
wakamatwe wahusika mara moja na kuniagiza nishirikiane naye.
“Baada ya siku mbili, yaani Mei 9, nikapigiwa siku na Salum (CID
Osysterbay) akanieleza yeye ndiye mpelelezi wa kesi yangu na angependa
kuniona. Tahere 12 Mei nilimuona Salum. Kwa sababu ya kuwa Zanzibar
ndiyo maana nilichelewa kumuona. Akanisikiliza na kusema angepeleleza
hiyo kesi na angeniita.
“Mheshimiwa, kila mara huyu Salum hakunipa msaada ipasavyo kwa madai
kwamba hajamuona Ally Edha. Nilishangaa sana sababu ofisi ya Ally Edha
ipo, wanaijua na iweje waseme hawamuoni? Baada ya muda, katikati ya
Mwezi wa Ramadhani, Salum aliniita na kuniambia mwenzake aitwae James
angeweza kunisaidia kuipata silaha yangu kutoka kwa Ally na nikamuona
huyo James ambaye aliahidi Ally Edha akirudi safari yake kwa asilimia 90
nitapata pistol (bastola) yangu. Akasisitiza pia akimuona siku ya
kwanza tu Ally angenipatia hiyo bastola.”
Aombwa chochote akishasaidiwa
“Nakumbuka katikati ya Oktoba, mwaka jana Salum alinipigia simu akasema
James anauliza endapo akinisaidia kuipata hiyo bastola mimi ningempa
zawadi gani. Nikamjibu, ‘Nitampatia anachotaka’ ilimradi nipate bastola
na vitu vyangu.
“Mheshimiwa, Nashangaa tangu wakati huo walipoanza kutaka chochote kwangu, hawajanipigia tena, wala kunisaidia.
Nami nilishajiandaa kuwakamatisha kwa rushwa. Nikaendelea kupata
matatizo ya kujificha kwa kuamini Ally Edha ana mamlaka ndani ya Jeshi
la Polisi na anaweza kunifanyia chochote atakacho.
“Mheshimiwa, Nikashauriwa niende kutoa taarifa Makao Makuu ya Polisi
(wizarani). Hivyo tarehe 27 Novemba, mwaka jana nilienda huko nikamuona
Bwana Laizer ambaye ni Kamishna. Nikamueleza na nikamuonesha vielelezo.
Alisikitika sana na hapo alimuagiza RPC wa Kinondoni ashughulikie hilo
jambo na amueleze kwa kila kinachoendelea.
“Hadi leo tarehe 29 Novemba, nimeamua nikatumie barua hii na vielelezo
vyangu ili unisaidie, kwani polisi hawanisaidii tangu nifanyiwe unyama
huu. Najiuliza na kujiona mkiwa kwa kuamini kwamba huyu Ally Adha Awadh
yupo juu ya sheria? Iweje polisi wamlinde tangu Mei 2013 hadi leo pasipo
kukamatwa? Mheshimiwa Naomba msaada wako.”
Barua hii ya mlalamikaji aliweza kupeleka nakala kwa Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Waziri wa Katiba na Sheria, Waziri wa Utawala Bora,
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Katibu Mkuu
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), na Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa.
Kwa upande wake, Awadh amegoma kuzungumza na JAMHURI. Mara kadhaa
amepigiwa simu yake, lakini amekataa kuzungumza hata pale simu
ilipopokewa. Ametumiwa ujumbe kwa nyakati na siku tofauti, lakini hadi
tunakwenda mitamboni alikuwa hajajibu.
Ujumbe mmoja ulisema, “Habari za kazi.
Hapa ni gazeti JAMHURI. Tuna habari za kesi ya … dhidi yako. Tunaomba
kujua kama hili suala unalijua kabla hatujaichapisha. Tangu jana
tunaomba utupatie majibu- bila mafanikio. Tumetekeleza wajibu wetu
kitaaluma kwa hiyo hatustahili lawama. Mhariri”.
CHANZO: Gazeti la Jamhuri
Post a Comment