Dar es Salaam.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Makumba Kimweri na Msanifu Mkuu, Richard Maliyaga, kila mmoja kulipa faini ya Sh15 milioni au kwenda jela miaka tisa baada ya kuwatia hatiani kwa matumizi mabaya ya madaraka na kuruhusu ujenzi wa jengo la ghorofa 18 karibu na Ikulu.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo
alisema jengo hilo lilipaswa kuwa la ghorofa sita na kuamuru kubomolewa
kuanzia ghorofa ya saba kwenda juu.
Hakimu Fimbo alisema baada ya kupitia ushahidi
uliotolewa na mashahidi 13 wa upande wa mashtaka, vielelezo 20
vilivyowasilishwa na ushahidi wa utetezi uliotolewa na washtakiwa
wenyewe, upande wa mashtaka ulithibitisha pasipo shaka mashtaka dhidi ya
vigogo hao waliodaiwa kuruhusu ujenzi wa ghorofa 18.
Hivyo aliwahukumu washtakiwa hao kila mmoja kulipa
faini ya Sh5milioni au kutumikia kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa
lililokuwa likiwakabili. Kila mshtakiwa alilipa kiasi cha Sh15 milioni
mahakamani hapo na kuepuka kifungo.
Baada ya hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai
alisema ndani ya kipindi cha miezi sita baada ya hukumu hiyo kutolewa,
Kifungu cha 40, namba 1 na 2 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
kinawaruhusu kutaifisha jengo hilo.
Washtakiwa hao walikuwa wakitetewa na Mawakili Majura Magafu na Paschal Kamala.
Post a Comment