HOTUBA YA RAIS KIKWETE KWA TAIFA -31 JULAI 2014(KUHUSU MCHAKATO WAKATIBA).
SOMA, UTAFAKARI NA UPIME KAMA ANACHOSEMA RAIS WETU NI KWELI. KISHA, CHUKUA HATUA.Mchakato wa Katiba MpyaNdugu Wananchi;Kama tujuavyo, Bunge Maalum la Katiba lililoahirishwatarehe 25 Aprili, 2014 kupisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi kushughulikia bajeti za Serikali husika, litakutana tena tarehe 5Agosti, 2014 kuendelea na kazi yake ya kutunga Katiba Mpya. Kwa vile Bunge Maalumu la Katiba halikuweza kumaliza kazi yake ndani ya siku 70 zilizotengwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, nimeliongezea Bunge hilo siku 60 kwa ajili ya kukamilisha kazi yake. Nimefanya hivyo kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa na Sheria hiyo hiyo.Hatua Iliyofikiwa Kabla ya Kuahirishwa kwa BungeNdugu Wananchi;Itakumbukwa pia kuwa, tarehe 16 Aprili, 2014, baadhi ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba hasa kutoka vyama vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi walisusia mjadala uliokuwa unaendelea Bungeni na kutoka nje. Wakati wanatoka Bungeni, kazi kubwa ilikuwa imefanyika. Tayari Kamati zote 12 za Bunge hilo zilikuwa zimekamilisha kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita za Rasimu ya Tume. Sura hizo zinazungumzia utambulisho wa nchi na muundo wa muungano. Kamatizote zilipiga kura ya kupitisha uamuzi wao kuhusu sura hizo mbili. Kamati kadhaa ziliweza kupata theluthi mbili ya kura kwa Wajumbe wa pande zote mbili za Muungano, jambo lililoonyesha dalili njema kwamba Katiba mpya inaweza kupatikana.Baada ya hapo, taarifa ya kila Kamati iliwasilishwa kwenye Bunge zima. Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, maoni ya wachache nayo yaliwasilishwa.Kazi iliyokuwa inafuatia,kwa mujibu wa Kanuni za Bunge ni kwaKamati ya Uandishi kukamilisha taarifayake na kuiwasilisha kwenye Bunge zima kwa ajili ya kujadiliwa. Baada ya Wajumbe kujadili taarifa hiyo itafuatia kupiga kura ili kuamua kuhusu Sura hizo mbili. Kama yalivyo masharti ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, uamuziutafanywa kwa theluthi mbili ya kura za kila upande wa Muungano wetu.Sababu za Baadhi ya Wajumbe KususiaBunge Maalumu la KatibaNdugu Wananchi;Sote tumewasikia Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba waliosusia vikao vya Bunge hilo wakielezea sababu zilizowafanya watoke Bungeni. Walitoa matamko kwenye vyombo vya habari na pia katika mikutano ya hadhara waliyoiitisha na kuhutubia sehemu mbalimbali nchini. Sababu walizotoa zimekuwa zikiongezeka na kubadilika kadri siku zinavyosonga mbele na upepo wa kisiasa unavyokwenda.Hivi sasa wanazungumzia mambo mawili. Kwanza, kwamba Bunge Maalumu halina mamlaka ya kuifanyia mabadiliko yo yote Rasimu ya Katiba iliyowasilishwana Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa maoni yao, kazi ya Bunge Maalumu la Katiba ni kujadili na kupitisha tu Rasimu ya Katiba ya Tume na siyo kubadili cho chote. Pili, wametoa sharti la wao kurudi Bungeni ni kuhakikishiwa kwamba, kitakachojadiliwa Bungeni ni Rasimu ya Tume. Bila ya sharti hilo kukubaliwa,wamesisitiza kutorudi Bungeni.Mamlaka ya Bunge Maalum la KatibaNdugu Wananchi;Mimi nimehusika katika kubuni wazo lakuwa na mchakato wa kuandika Katiba Mpya, na katika maandalizi ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ya kuongoza na kuendesha mchakato huo. Kwa kweli sikumbuki wakati wo wote katika vikao vya Baraza la Mawaziri kujadili Rasimu ya Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba tulipozungumziaRasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa haiwezi kufanyiwa marekebisho na Bunge Maalumu la Katiba.Mimi siyo Mwanasheria na hivyo nakirikwamba naweza kuwa na upungufu katika kuelewa maana ya baadhi ya maneno ya kisheria. Hata hivyo, sikumbuki kuwepo kwa kifungu cho chote katika Sheria kinachosema kuwa Bunge Maalumu la Katiba halina mamlaka hayo. Tangu tulipoyasikia maneno hayo yakisemwa nimeuliza nithibitishiwe ukweli wa madai hayo bado sijaambiwa vinginevyo. Kama ukweli huo upo naomba anisaidie. Badala yake naambiwa kuwa maneno yaliyotumika katika Sheria haiakisi dhana inayotolewa kuwa kazi ya BungeMaalum la Katiba ni kubariki Rasimu na siyo kufanya vinginevyo. Nimeambiwa kuwa sheria inasemaTume itaanda Rasimu ya Katiba na Bunge Maalum la Katiba litatunga Katiba iliyopendekezwa.Ndugu Wananchi;Tarehe 30 Desemba, 2010, nilipozungumziadhamira yangu ya kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba Mpya nilieleza wazi nia ya kuwepo kwa uwakilishi mpana wa Watanzania katika mchakato huo. Ndiyo maana katika Sheria tukaweka ngazi nne katika mchakato wa kutunga Katiba. Ngazi ya kwanza ikiwa ya wananchi kutoa maoni yao juu ya kila wanachotaka kijumuishwe katika Katiba ya nchi yao. Ngazi ya pili, ni ya wananchi kupitia wawakilishi wao katika Mabaraza ya Katiba ya Wilaya naMabaraza ya Kitaasisi kutoa maoni yaokuhusu Rasimu ya kwanza ya Katiba iliyotayarishwana Tume.Ngazi ya tatu inajumuisha wawakilishi wa wananchi waliopo kwenye Mabaraza ya Kutunga Sheria ya Sehemu zetu mbili za Muungano, yaaniBunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi, wakichanganyikana Wawakilishi wa makundi mbalimbali ya jamii ya Watanzania kutoka pande zote mbili zaMuungano. Hawa ndio wanaounda Bunge Maalumu la Katiba, lenye jukumu la kutunga Katiba inayopendekezwa.Mamlaka ya kutunga Katiba kwa mila na desturi za Mabaraza ya Kutunga Sheria ni uwezo wa kurekebisha, kubadili, kufuta na hata kuongeza kilichopendekezwa. Ingekuwa kilichokusudiwani kubariki tu lisingetumiwa neno la kutunga Katiba. Hali kadhalika, lisingewepo sharti la kupiga kura na msisitizo wa kupata theluthi mbili kwa kila upande wa Muungano. Aidha, kama ingekuwa jukumu la Bunge Maalumu ni kubariki tu Rasimu lisingepewa siku 70 za kazi na Rais kupewa mamlaka ya kuongeza siku zaidi kadri aonavyo yeye inafaa.Ngazi ya nne na ya mwisho, tuliweka kura ya maoni ya wananchi kukubali aukukataa Katiba inayopendekezwana Bunge Maalumu la Katiba. Kama ingekuwa Rasimu ya Tume haiwezi kubadilishwa hata nukta kwa nini basi tuweke kura ya maoni ya kuwahusisha wananchi wote?Ndugu Wananchi;Tulizibuni ngazi hizi nne kwa dhana kwamba kile ambacho hakikuonekana au hakikuwekwa sawa katika ngazi moja kitaonekana na kurekebishwa katika ngazi inayofuata katika ngazi ziletatu za mwanzo. Na, iwapo Katiba iliyotungwa haitawaridhishawananchi wanayo haki ya kuikataa. Kwa kufanya hivyo, wananchi ndiyo waliopewa turufu ya mwisho.Ndugu wananchi;Kwa kweli, napata shida kuelewa mkanganyiko unatoka wapi na hasa wale wanaoongoza kuhoji mamlaka ya Bunge Maalumu kuwa ni wale wale waliotunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba tena hatua kwa hatua. Nashangazwa zaidi ninapoona wale wale waliotunga Kanuni za Bunge Maalumu ndiyo wanaoongoza kuhoji uhalali wa kile walichokitunga.Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, Ibara ya 33 (8) inasema: Nanukuu: “Wakati wa mjadala, Mjumbe yoyote anaweza kutoa mapendekezo ya marekebisho, maboresho au mabadiliko yaliyomo katika Sura za Rasimu ya Katiba zinazojadiliwa kwa utaratibu ufuatao: (a) Ikiwa ni marekebisho, maboresho au mabadiliko yanayobadilishajambo la msingi, au yanayobadilishamaudhui yaIbara, mapendekezo ya marekebisho yatapelekwa kwa maandishi kwa Katibu siku moja kabla ya mjadala wa Ibara husika. (b) Ikiwa ni marekebisho madogo, ambayo hayabadili msingi au maana, mapendekezo ya marekebisho yatawasilishwa na mjumbe wakati wa mjadala baada ya kupata ruhusa ya Mwenyekiti”. Mwisho wa kunukuu.Kanuni hii ilipotungwa, Wajumbe wote wa Bunge Maalumu pamoja na wale ambao baadae walisusia vikao vya Bunge walikuwepo Bungeni na walishiriki kuipitisha. Tena basi, baadhi yao walikuwa Wajumbe wa Kamati ya Kanuni iliyopendekeza Kanuni hizo. Unapowaona watu wale wale sasa wanakuwa vinara wa kuhoji mamlaka ya Bunge Maalumu la Katiba, unajiulizamaswali mengi kuhusu watu hao bila ya kupata majibu yaliyo sahihi na kutosheleza akili na ufahamu wetu.Ndugu Wananchi,Unaposoma Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Kanuni za Bunge Maalumu, hii ni dhahiri kwamba wote walikuwa na uelewa wa pamoja kuhusu mamlaka ya Bunge Maalumu ya kujadili Rasimu iliyoandaliwa na Tume na kutunga Katiba inayopendekezwakwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa kura.KinachojadiliwaBungeni ni Rasimu ya TumeNdugu Wananchi;Yapo madai yanayotolewa na kuenezwa na Wajumbe waliosusia Bunge Maalumu la Katiba kwamba kinachojadiliwaBungeni siyo Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ndiyomaana basi wanaweka sharti la kujadiliwa Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba ndipo warudi Bungeni. Madai haya nayo yananipa taabu kuyaelewa. Ndugu zetu hawa walishiriki siku zote 19 za Kamati 12 zilipokutana kujadili Sura ya Kwanza na ya Sita za Rasimu yaTume. Halikadhalika. walikuwepo na kushiriki kwa ukamilifu wakati taarifa za Kamati, tangu ya Kwanza mpaka ya 12, zilipowasilishwa kwenye Bunge zima. Aidha, na wao walishiriki kutoa maoni ya wachache kwa dakika 20 na kutoa ufafanuzi kwa muda wa dakika 30 kwa kila Kamati. Haya maneno ya sasa kwamba kinachojadiliwaBungeni siyo Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba bali nyingine kabisa ambayo wanadai eti ni ya CCM yanatoka wapi.Mimi nadhani kuwa huenda katika Kamati kumefanyika marekebisho kwenye Rasimu ambayo hayakuwapendeza. Kama hivyo ndivyo, wawe wakweli kuhusu jambo hilo kuliko kusema mambo yasiyowakilishaukweli halisi wa Rasimu inayojadiliwa. Matokeo yake ni kuwafanya wafuasi wao na wapenzi wao na hata watu wengine waamini kuwa kinachojadiliwasiyo Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba bali nyingine tenani ya CCM. Jambo hilo si kweli na wenyewe wanajua kwamba si kweli ila sijui kwa nini wameamua kupotosha ukweli.Ndugu Wananchi;Kinachonishangaza, zaidi ni kwamba, kama hawakuridhishwana yaliyofanyika, kwa nini wasingetumia mifumo waliyojitengenezea wenyewe kwenye Kanuni kumaliza tofauti zao? Kanuni zinaelekeza kuwa mambo wasiyoridhika nayo yajadiliwe kwenye Kamati ya Mashauriano na Maridhiano. Ukiacha mifumo ya maridhiano ndani ya Bunge ukaenda nje kwa wananchi au vyombo vya habari na mitandao si jawabu la tatizo.Ndugu Wananchi;Ndiyo maana nashawishika kuunga mkono wale wote wanaowasihi Wajumbe wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi na wengine warejee Bungeni. Watumie mifumo maalum ya Bunge iliyowekwa na Kanuni kutafuta maridhiano. Hali kadhalika, wasichoke kuwa na mawasiliano na vyama vingine vya siasa na hasa CCM kutafutamaelewano. Mimi niko tayari kusaidia pale watakapoona inafaa kufanya hivyo kama ambavyo nimekuwa nikifanya ziku za nyuma.Nililolisema mwanzoni kabisa mwa mchakato na nalirudia tena leo kwamba, ili tuweze kufanikiwa kupata Katiba Mpya ambayo sote tunaitaka, maelewano baina ya wadau wakuu wa kisiasa ni jambo lisilokuwa na badala yake. Vinginevyo kupata theluthi mbili kwa pande zote mbili za Muungano haitawezekana. Ndiyo maana nampongeza sana Msajili wa Vyama vya Siasa, Mheshimiwa Jaji Francis Mutungi, kwa uamuzi wa kuvikutanishavyama vinne vikuu vya siasa kujadili namna ya kuondoa mtihani uliopo sasakatika mchakato wa Katiba.Ombi langu kwa viongozi wa vyama hivyo ni kuitumia vyema fursa ya majadiliano kuukwamua mchakato kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake. Hali kadhalika nampongeza sanaMwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Mheshimiwa Samwel Sitta, kwa kuitisha kikao cha Kamati ya Mashauriano na Maridhiano. Bahati mbaya ni kwamba Wajumbe wa vyamavilivyosusia Bunge Maalumu hawakushiriki. Ni matumaini yangu kuwa Mheshimiwa Sitta hatokata tamaa kuendeleza juhudi za mashauriano na kwamba katika vikao vijavyo na wenzetu hawa watashiriki.Ndugu Wananchi;Hivi karibuni kumekuwepo pia madai yanayoelekeza lawama kwangu. Kwanza nalaumiwa eti kuwa mambo yalikuwa yanaenda vizuri mpaka pale nilipotoa hotuba ya ufunguzi wa Bunge Maalumu ndipo yalipoharibika.Pili nalaumiwa kwamba nawezaje kuikana Rasimu ya Katiba ambayo na mimi ni mmoja wa watu waliotia sahihi katika Rasimu hiyo.Niruhusuni nianze na hili la pili. Nadhani ndugu zetu wanaotoa madai haya yameitafsiri isivyo sahihi yangu katika Gazeti la Serikali lililotangaza rasmi Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba baada ya Tume kumaliza kazi yake ya kuandika Rasimu ya Katiba, Rais wa Jamhuri ya Muungano amepewa kazi tatu kufanya. Kwanza, kupokea Rasimu hiyo na Taarifa ya Tume kutoka kwa Mwenyekiti jambo ambalo lilifanywa tarehe 30 Desemba, 2013. Pili, amepewa kazi ya kuitangaza rasmi Rasimu ya Katiba na Taarifa ya Tume kwa watu wote kuiona na kuisoma ndani ya siku 30. Alipewa sharti la kuitangaza katika Gazeti la Serikali na vyombo vingine vya habari. Hili nalo lilifanywa hivyo tarehe 22 Januari, 2014.Ndugu Wananchi;Katika kutangaza katika Gazeti la Serikali sharti linamtaka anayetangaza ajitambulishe kuwa yeye ni nani na atiesahihi yake. Kwa kufanya hivyo, hakumfanyi yeye kuwa naye ni mhusika na maudhui ya kila kinachopendekezwa na Tume. Sahihi zilizomo ndani ya Rasimu na Taarifa ya Tume ni za Wajumbe wa Tume, kamwesahihi ya Rais haimo hivyo hawezi kulaumiwa kuwa anaikana sahihi yake. Yeye ametimiza wajibu wake wa kutangaza, akaiweka hadharini kwa umma wa Watanzania kuiona na kusoma Rasimu ya Katiba na Taarifa yaTume vilivyotayarishwa na kutiwa sahihi na Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kazi ya tatu ni kuitisha Bunge Maalumu ambayo nayoimekamilika tangu tarehe 18 Februari, 2014.Ndugu Wananchi,Jambo lingine linalofanana na hilo ni yale madai kwamba nilikuwa napata taarifa ya maendeleo ya mchakato ndani ya Tume mara kwa mara, iweje leo nitoe maoni tofauti kama niliyoyatoa katika hotuba yangu kwenye Bunge Maalumu. Ni kweli kabisa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba, Makamu wake, Mheshimiwa Jaji Agustino Ramadhani na Mheshimiwa Dkt. Salim Ahmed Salim wamekutana na mimi kwa nyakati mbalimbali kuzungumzia mwenendo wa mchakato. Lakini, hayakuwa mazungumzo ya kina kuhusu nini kiwe vipi katika maudhui na mapendekezo ya Tume. Ukweli ni kwamba Rasimu zote mbili nilizipata mara ya kwanza nilipokabidhiwarasmi, tena kwa uwazi. Napenda watu wasijenge dhana kuwa nilipewa Rasimuna kuisoma kabla ya kukamilika na hivyo nilitoa maoni yangu. Tume hii ilikuwa huru na niliiacha iwe hivyo. Sikuiingilia kwa namna yo yote ile kupenyeza mambo ninayotaka yawemo. Kuthibitisha dhamira yangu ya kutaka Tume iwe huru katika kufanya kazi zao hata pale waliponitaka nitoe maoni niliwaomba tusifanye hivyo ili nisiwakwaze katika kufanya kazi zao, wakapata taabu ya kuwianisha wanayofikiria na mawazo yangu.Ndugu Wananchi;Kuhusu madai kwamba mambo yalikuwa yanakwenda vizuri na kwamba hotuba yangu iliyavuruga, napenda kusema wazi kuwa lawama hizo hazina ukweli wo wote. Ni madai yasiyokuwa na msingi. Kwani mimi hasa siku ile nilifanya lipi la ajabu. Ukweli ni kwamba nilisema yale yale ambayo Tume yenyewe imeyasema katika Rasimu ya Katiba na Taarifa za Tume. Niliyoyasema kuhusu malalamiko ya watu wa pande zetu za Muungano na uzuri na changamoto za miundo ya Serikali mbili na Serikali tatuni yale yale yaliyomo kwenye taarifa zaTume. Nimetumia takwimu zile zile za Tume. Pengine kilichoonekana kuwa kibaya ni jinsi nilivyozifasiritaarifa hizona mapendekezo ya Tume.Jambo lingine ambalo nimelifanya ni kutoa maoni yangu kuhusu baadhi ya vipengele vya Rasimu hususan uandishi na dhana mbalimbali zilizokuwamo. Silioni kosa langu kwa kufanya hivyo, kwani Rasimu imetolewa hadharani kwa watu kuijadili. Na mimi kama raia ninayo haki ya kufanya hivyo kama wafanyavyo wengine. Kwa nini nilaumiwe kwa kutumia haki yangu hiyo.Lakini, pia mimi ndiye Rais wa nchi yetu, ninayo dhamana ya uongozi na ulezi wa taifa letu. Itakuwaje kwa jambo kubwa la hatma ya nchi yetu nilinyamazie kimya. Watanzania wangeshangaa na wangekuwa na haki ya kuhoji Rais wao ana maoni gani. Bahati nzuri nilitoa maoni yangu mahali penyewe hasa, na kwa uwazi, kwenye Bunge Maalumu la Katiba. Hata hivyo, ni muhimu kusisitiza kuwa namna nilvyotoa maoni yangu sikuwa natoa maagizo wala kushurutisha, ndiyo maana kila wakati niliwakumbusha Wajumbe kuwa mamlaka ya uamuzi ni yao. Yangu yalikuwa maoni tu wanahiyari ya kuyakubali au kuyakataa. Niliwataka Wajumbe wasome na kuielewa vyema Rasimu. Nilisema wasome sura kwa sura, mstari kwa mstari na neno kwa neno. Niliwaomba wajiridhishe kuhusu uandishi na dhana mbalimbali. Nilitoa mifano ya mambo yahusuyo uandishi ambayo ni vyema wayatazame. Pia nilitoa mifano ya dhana ambazo niliwasihi wajiridhishe juu ya kufaa kwake kuwepo.Kuhusu muundo wa Serikali tatu, nilieleza wazi kuwa sina tatizo nao kama ndiyo matakwa ya Watanzania. Lakini, nilieleza hofu yangu kuhusu mapendekezo ya Tume na kuwataka Wajumbe wafanye kazi ya ziada kuondosha udhaifu iwapo wataukubali muundo unaopendekezwa.Nilieleza nia yangu ya kutaka tuwe na Serikali yaMuungano yenye ukuu unaoonekana, yenye nguvu ya kuweza kusimama yenyewe, inayoweza kuwa tegemeo kwa nchi Washirika, Serikali isiyokuwa tegemezi wala egemezi kwa nchi washirika na ambayo inavyo vyanzo vya uhakika vya mapato. Hivi kwa kutoa ushauri huo kwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba inageuka kuwa nongwa. Kwa kweli sielewi lawama ni ya nini?.Naamini sistahili lawama bali pongezi kwa kuwa muwazi na kutoa ushauri wamsingi ambao utasaidia nchi kupata Katiba nzuri inayojali maslahi ya watu wa nchi yetu na ya nchi zetu mbili zilizoungana miaka 50 iliyopita.HitimishoNdugu Wananchi;Mwisho, ni maoni yangu ya dhati kuwa mgogoro uliopo sasa katika mchakato wa Katiba hauna sababu ya kuendelea kuwepo. Naamini hayo yote ambayo Wajumbe wa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi wanayalalamikiayanaweza kushughulikiwa kwa ukamilifu katika mifumo ya Bunge Maalumu la Katiba iliyotengenezwana Wajumbe wote na wao wakiwemo. Nawasihi waitumie. Hali kadhalika, kwakupitia mazungumzo wanayofanya na wenzao wa Chama cha Mapinduzi wanaweza kutengeneza nguvu ya pamoja kutatua changamoto za sasa na zitakazojitokeza baadaye. Kilicho muhimu ni kwa pande zote kuwa na dhamira ya dhati ya kutoka hapa tuliposasa. Kama utashi wa kisiasa upo kwa kila mmoja wetu, hilo ni jambo linalowezekana kabisa. Narudia kuahidi utayari wangu wa kusaidia kadri inavyowezekana tusonge mbele.Mungu Ibariki Afrika!Mungu Ibariki Tanzania!
Hotuba ya Rais 31 Julai 2014
Written By peterdafi.blogspot.com on Tuesday, August 5, 2014 | 12:35 AM
Labels:
kitaifa
Post a Comment