JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TAMKO LA MHE. UMMY MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKOMA DUNIANI TAREHE 29/1/2016
Ndugu Wananchi,
Kwa zaidi ya miaka 62, Siku ya Ukoma Duniani imekuwa ikiadhimishwa ulimwenguni kote kila Jumapili ya mwisho ya mwezi Januari. Siku hii iliasisiwa na Mwandishi wa Habari Mfaransa Raoul Follereau aliyetumia muda wake mwingi kuzunguka Dunia kueleza hali duni ya maisha ya watu walioathirika na ugonjwa wa ukoma. Siku hii ilianzishwa ili kuhimiza jamii kutoa kipaumbele kwa kuwapatia huduma stahiki wagonjwa wa ukoma na watu wenye machungu ya athari za ukoma. Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) huadhimisha siku hii.
Ndugu Wananchi,
Lengo kuu la maadhimisho haya ni kukumbusha umma wa Watanzania juu ya ugonjwa huu. Ni dhahiri kuwa, ugonjwa wa ukoma umekuwa ukiogopwa sana katika jamii yetu toka enzi na enzi hasa kutokana na ukweli kwamba unasababisha ulemavu wa kudumu mwilini na kufanya waathirika kuwa tegemezi na kutothaminiwa.
Ndugu Wananchi,
Tanzania ni miongoni mwa nchi 17 Duniani ambazo bado zina viwango vya juu vya ugonjwa wa ukoma. Mwaka 2013, nchi yetu ilisaini makubaliano katika mkutano uliofanyika Bangkok Thailand yaliyoazimia kuwa na Dunia bila ugonjwa wa ukoma (Bangkok declaration towards a leprosy - free world). Serikali itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kubaini na kuendeleza jitihada sahihi za kutokomeza ukoma nchini.
Ndugu Wananchi,
Siku hii inatupa fursa ya kutathmini mwelekeo wa jitihada zetu nchini na zile za Kimataifa katika kupambana na ugonjwa huu. Kauli mbiu katika maadhimisho ya mwaka huu ni “TANZANIA ISIYOKUWA NA MAAMBUKIZI MAPYA YA UKOMA”. MAAMBUKIZI SIFURI, WAGONJWA WAPYA SIFURI NA BILA ULEMAVU UTOKANAO NA UKOMA. (“TOWARDS A WORLD FREE OF LEPROSY”. ZERO CASES, ZERO MORBIDITY AND ZERO DISABILITY). Kauli mbiu hii, inatutaka kuimarisha mapambano yetu dhidi ya ukoma na kubuni mikakati endelevu ili tuweze kutoa utatuzi wa changamoto zilizobaki katika kuutokomeza kabisa ukoma nchini hususani katika maeneo ambayo hayajafikia viwango vya utokomezaji.
Ndugu Wananchi,
Dalili ya awali kabisa ya ukoma ni baka au mabaka kwenye ngozi yasiyo na uwezo wa kuhisi. Kwa kawaida hayawashi wala hayaumi. Mabaka haya hukosa hisia ya joto, mguso au maumivu.
Dalili nyingine za ukoma ni pamoja na vijinundu vyenye rangi ile ile ya ngozi sehemu yoyote ya mwili. Naomba kutoa rai kwa wananchi kuwa, kila uonapo mojawapo ya dalili hizi unashauriwa kwenda kwenye kituo cha huduma za afya kilicho karibu na wewe kwa uchunguzi na matibabu. Hii itawawezesha Wataalam wa Afya kuchunguza na kubainisha kama mgonjwa ana ukoma katika hatua za awali ili apate tiba sahihi mapema na kupona na hata kuepusha ulemavu usio wa lazima.
Ugonjwa wa ukoma hutibiwa na dawa mseto (Multi drug therapy au MDT). Tiba ya ukoma inachukua kati ya miezi sita hadi mwaka mmoja kulingana na aina ya ukoma. Mgonjwa ambaye ameanza tiba, siyo rahisi kuambukiza mtu mwingine na hivyo hakuna sababu ya kumtenga na anaweza kuendelea na shughuli za kawaida za maisha. Ukoma unatibika na mgonjwa kupona kabisa. Tiba ya ukoma inapatikana nchini kote na hutolewa bila malipo kwa wagonjwa wote.
Ndugu Wananchi,
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2014, jumla ya wagonjwa 2,134 wa ukoma waligunduliwa ambapo 271 kati ya hao ambao ni sawa na asilimia 13 walikuwa na ulemavu daraja la pili. Bado kuna Wilaya 17 za Tanzania Bara na 2 za Tanzania Visiwani zinazogundua idadi kubwa ya wagonjwa wa ukoma. Kwa upande wa Tanzania Bara Wilaya hizo ni pamoja na Liwale, Ruangwa, Lindi Mjini, Lindi Vijijini, Masasi Vijijini, Newala, Nanyumbu, Namtumbo, Tunduru na Nkasi. Nyingine ni Mkinga, Muheza, Korogwe, Musoma Vijijini, Chato, Shinyanga Manispaa na Rufiji. Kwa Tanzania Visiwani ni Mkoa wa Mjini Magharibi katika Wilaya za kati na Kusini. Hata Hivyo, wagonjwa wengi hawajitokezi kutafuta huduma kutokana na unyanyapaa mkubwa dhidi ya wagonjwa hao ambao bado ni tatizo miongoni mwa jamii zetu.
Napenda kutoa rai kwa Halmashauri hizi ambazo bado zina wagonjwa wengi kutenga fedha kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi kutambua dalili za awali za ukoma ili kuwahi matibabu na kuzuia maambukizi mapya. Kumbuka ukoma ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na vimelea aina ya bakteria na unaenezwa kwa njia ya hewa kutoka kwa mgonjwa kwenda kwa mtu anayeishi naye au aliye karibu naye. Mtu yeyote anaweza kuambukizwa, maana ukoma haubagui. Hivyo basi, ni muhimu kuhimizana na kumwelekeza mtu mwenye dalili kwenda katika kituo cha huduma kufanyiwa uchunguzi na kupata tiba mapema ili kukata mnyororo wa maambukizi.
Ndugu Wananchi,
Athari kuu ya ugonjwa wa ukoma ni kusababisha ulemavu wa kudumu ambao vile vile ndiyo kiini cha unyanyapaa na ubaguzi unaoelekezwa kwa wagonjwa wa ukoma. Ulemavu unatokana na kuchelewa kwa uchunguzi na matibabu sahihi. Hapa Tanzania asilimia kumi na tatu (13%) ya wagonjwa wapya wa ukoma wanaojitokeza katika vituo vyetu kwa ajili ya uchunguzi na kuanza matibabu wanakuwa tayari wana ulemavu wa kudumu. Aidha, mgonjwa yeyote wa ukoma akigundulika tayari ameshapata ulemavu, ni dalili mbaya. Hii ina maana kuwa mgonjwa amechelewa kugundulika mapema na akapata ulemavu. Vile vile, ameendelea kueneza vimelea vya ukoma katika jamii na kuwaambukiza wengine. Kwa miaka mitano mfululizo,Tanzania imekuwa inapata kila mwaka walemavu wapya wasiopungua 250 kutokana na ukoma.
Wito wangu kwenu leo hii, sote tujenge tabia ya kuchunguza miili yetu na pale tunapoona mabadiliko yoyote yanajitokeza twende mapema katika vituo vyetu vya huduma za Afya kuchunguzwa ili tupate ushauri wa kitaalam na matibabu stahili.
Ndugu Wananchi,
Zipo changamoto ambazo zinarudisha nyuma juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa ukoma nchini. Changamoto hizo ni pamoja na unyanyapaa kwa wale waliougua na walioathirika na ukoma. Sababu kuu ni Imani na mila potofu na ukosefu wa uelewa kuhusu ugonjwa huu. Ukweli ni kwamba ukoma ni ugonjwa unaoambukizwa kwa njia ya hewa, husababishwa na vimelea aina ya bakteria na chanzo cha maambukizi ni mgonjwa wa ukoma ambaye hajagunduliwa wala kuanza matibabu. Mgonjwa akianza na kuzingatia matibabu hawezi kuambukiza tena na wale wote wanaouguza athari za ukoma baada ya kukamilisha matibabu ni walemavu wa viungo na siyo wagonjwa. Changamoto nyingine ni uhaba wa fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za kudhibiti ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa elimu kuhusu ukoma kwa watumishi wa Afya.
Ndugu Wananchi,
Ili kutatua changamoto zilizotajwa hapo juu ambazo zinapelekea kuibua wagonjwa wachache ndani ya jamii, Wizara ikishirikiana na wadau mbalimbali inafanya yafuatayo:
Kuendeleza programu ya mafunzo na uelimishaji kwa watumishi wa Afya.
Kutekeleza mpango wa uchunguzi katika ngazi ya kaya na kutoa dawa za kinga kwa watu ambao wameambukizwa ukoma na hawana dalili hasa wale wanaoishi na wagonjwa wa ukoma katika baadhi ya Wilaya zenye idadi kubwa ya wagonjwa.
Kuhakikisha dawa zinapatikana wakati wote na kusambazwa nchi nzima katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali zote.
Huduma kwa wagonjwa wa ukoma zinapanuliwa kwa kushirikisha Taasisi zisizo za Kiserikali na kutolewa bila usumbufu wowote kwa wagonjwa.
Tiba na huduma sahihi kwa wale waliopata ulemavu utokanao na ukoma inatolewa ipasavyo.
Ndugu Wananchi,
Tunapofanya maadhimisho haya napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Serikali ya Tanzania kuyashukuru Mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya nchi kwa michango yao katika kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukoma hapa Tanzania. Aidha, inatubidi kukabili changamoto zilizopo na kuongeza ubunifu na kuibua mbinu mpya za kuongeza kasi ya kuukabili ukoma na athari zake na kuhakikisha tunakuwa na Tanzania isiyo na maambukizi mapya ya ukoma.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
Post a Comment