Home » » TAARIFA YA KIPINDUPINDU IMETOLEWA NA MH UMMY MWALIMU 30 MEI, 2016

TAARIFA YA KIPINDUPINDU IMETOLEWA NA MH UMMY MWALIMU 30 MEI, 2016

Written By peterdafi.blogspot.com on Monday, May 30, 2016 | 9:59 PM

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO




TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU (MB); WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, TAREHE 30 MEI, 2016.

Ndugu wanahabari,

Serikali kupitia Wizara yangu inaendelea na utaratibu wa kutoa taarifa ya mwenendo wa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu nchini kila wiki kama tulivyoahidi. Takwimu za ugonjwa huu zinaonyesha kuwa hadi kufikia tarehe 29 Mei 2016, kulikuwa na jumla ya wagonjwa 21,634 ambao wametolewa taarifa ya kuwa na ugonjwa huu, na kati ya hao, ndugu zetu 338 wamepoteza maisha.

Kwa kuwa tumefikia mwishoni wa mwezi Mei Wizara yangu inapenda kutoa tathimini ya ugonjwa huu kwa kulinganisha na mwezi Aprili. Tumefarijika kuona takwimu za mwezi uliopita hadi mwezi Mei 2016 zinaonyesha kuwa, kasi ya ugonjwa wa kipindupindu imepungua kwa asilimia 34 ambapo idadi ya wagonjwa mwezi Aprili ilikuwa 1024 na vifo 16 ukilinganisha na mwezi Mei ambao kumekuwepo na wagonjwa 524 na vifo 7. Aidha katika mwezi Aprili jumla ya mikoa 13 na Wilaya 42 ziliripoti ugonjwa wa kipindupindu, ukilinganisha  na Mikoa 9 na Wilaya 22  zilizoripoti ugonjwa mwezi Mei.  Mikoa hiyo ni pamoja na Morogoro 185, Manyara 74, Kilimanjaro 72, Lindi 71, Dar es Salaam 55, Mara 39, Pwani 18, Kagera 5 na Iringa 5. Kwa takwimu hizi ni dhahiri kuwa idadi ya wagonjwa na vifo vimepungua na pia idadi ya Mikoa na Wilaya zenye wagonjwa zimepungua.

Ndugu wanahabari,
Kupungua kwa idadi ya wagonjwa kusirudishe nyuma juhudi za kuuzuia ugonjwa huu, bali tunatakiwa kuzidisha jitihada ili tuweze kuuondoa, tusiwe na wagonjwa kabisa. Tuendelee kuzuia maambukizi, na pia kuendelea kutoa taarifa za ugonjwa kila siku, hata kama hakuna wagonjwa, na kusimamia kikamilifu hatua mbalimbali za udhibiti wa mlipuko huo kwa mujibu wa miongozo mbalimbali iliyotolewa na Wizara.

Ndugu wanahabari,

Wizara inaendelea kutoa rai kwa wananchi wote kuzingatia kanuni za usafi binafsi na usafi wa mazingira. Aidha Wizara inatoa elimu ya afya kwa njia ya kupiga simu kupitia namba 117 na kwa njia ya kutuma ujumbe wenye neno KIPINDUPINDU kwenda 15774. Huduma hizi zinatolewa bila malipo kupitia mitandao yote.

Ndugu wanahabari,
Tunaendelea kuisihi jamii kuungana na Halmashauri, Mikoa pamoja na Wizara katika juhudi za kupambana na kuenea kwa ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia yafuatayo:
        Kujenga na kutumia vyoo bora katika maeneo tunamoishi ili kupunguza hatari ya kuenea kwa ugonjwa huu.
        Kunawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni kabla ya kula, baada ya kutumia choo na baada ya kumsafisha mtoto aliyejisaidia.
        Mamlaka za maji zihakikishe upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.
        Kuhakikisha maji ya kunywa yanachemshwa au kutibiwa kwa dawa katika ngazi ya kaya.
        Kuzingatia ushauri na elimu sahihi kuhusu ugonjwa wa kipindupindu, ili jamii iondokane na imani potofu kuhusu kipindupindu. Viongozi wa dini, watu mashuhuri na waganga wa tiba mbadala wasaidie kuhamasisha jamii zao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huu,
        Kufikisha wagonjwa wa Kipindupindu mapema katika vituo vya kutolea huduma ili wawahi kupata matibabu.
        Kuzingatia matumizi sahihi ya ORS kwa wagonjwa walioanza kuonesha dalili ili kupunguza athari za ugonjwa.
        Watumishi wa afya kutoa takwimu sahihi na kamili za ugonjwa kwa kuzingatia miongozo inayotolewa na Wizara.


Hitimisho

Wizara inaendelea kutoa wito kwa wadau wote katika ngazi zote kushirikiana kwa pamoja katika juhudi za kutokomeza kipindupindu. Aidha, inawapongeza na kuwashukuru wadau wote kwa jitihada za dhati zinazoendelea kutekelezwa na katika kusimamia kikamilifu miongozo inayotolewa na Wizara ili kuutokomeza ugonjwa huu, wakiwemo wataalamu wa sekta mbalimbali, Mashirika ya Kimataifa, Watumishi, Mikoa na Halmashauri pamoja na waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla.

Asanteni sana

Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. peterdafi - All Rights Reserved
Template Created by Eddie Sucre Published by Bongoclanblog
Proudly powered by Blogger