Home » , , » Tuzo ya Mo Ibrahim imekosa mshindi

Tuzo ya Mo Ibrahim imekosa mshindi

Written By peterdafi.blogspot.com on Monday, October 15, 2012 | 12:15 PM



Mo Ibrahim

Mwaka huu hakuna mshindi wa tuzo ya Mo Ibrahim ambayo hutolewa kwa viongozi wa Afrika walioonyesha uongozi bora
Tuzo hiyo ya dola milioni tatu nukta mbili, hutolewa kwa kiongozi wa Afrika aliyechaguliwa kwa njia ya demokrasia na ambaye aliimarisha hali ya maisha ya wananchi wake na kisha kuondoka ofisini kwa khiari.
Kamati iliyokutana kumteua mshindi iliafikiana kuwa hakuna kiongozi aliyetimiza matakwa yote yaliyohitajika kuweza kuwa mshindi wa tuzo hiyo.
Mwaka jana Rais wa Cape Verde Pedro Verona Pires ndiye alishinda tuzo hiyo.
Aliongoza vita dhidi ya watawala wa kikoloni wa Ureno , aliongoza siasa za vyama vingi na kusifiwa kwa kuimarisha maisha ya wananchi wake.
Tuzo hiyo hutolewa katika kipindi cha miaka kumi na mshindi hupokea dola laki mbili kila mwaka maishani mwake.
Rais wa Cape Verde Pedro Pires
Akitangaza uamuzi huo, Ibrahim alisema "mtu hutandika anapotaka kulala. Ikiwa lengo letu ni kutoa tuzo kwa uongozi bora, lazima tutii vigezo vyetu wenyewe. Hatuwezi kujihujumu wenyewe''
''Sisi hatupo kwenye biashara ya kutoa ujumbe mzuri usio na manufaa, ikiwa tutafanya kinyume na kazi yetu, basi tutapoteza ushawishi wetu. Kamati ya tuzo hiyo ilitizama baadhi ya washidani lakini hakuna aliyetimiza matakwa yetu yote. '' alisema mwanachama wa kamati ya tuzo hiyo, Salim Ahmed Salim.
Washindi wengine wawili, katika miaka sita tangu kuzinduliwa kwa tuzo hiyo, walikuwa marais wa Botswana Festus Mogae na aliyekuwa Rais wa Msumbiji Joaquim Chissano.
Mapema mwezi huu wakfu wa Mo Ibrahim ulimtuza tuzo maalum ya dola milioni moja, Askofu mstaafu wa Afrika Kusini Desmond Tutu kwa kupigania haki za wananchi wa Afrika Kusini.
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. peterdafi - All Rights Reserved
Template Created by Eddie Sucre Published by Bongoclanblog
Proudly powered by Blogger