Tume ya mishahara nchini
Kenya, imesema kuwa makarani wa bunge wenye jukumu la kuwalipa
mishahara wabunge huenda wakapatikana na hatia ya kutumia vibaya mamlaka
yao na kufuja pesa za umma ikiwa watawalipa mishahara ya juu wabunge
kinyume na ile iliyoratibiwa na tume hiyo katika gazeti rasmi la
serikali.
Mwenyekiti wa tume hiyo, Sarah Serem ameonya
kuwa makarani wa bunge la taifa Justin Bundi na yule wa Senate, Jeremiah
Nyegenye huenda wakapatikana na hatia ya matumizi mabaya ya mamlaka
ikiwa watakiuka agizo hilo.Bi Serem alisema kuwa tume hiyo ilichapisha mishahara watakayopokea wabunge kwenye gazeti rasmi la serikali kwa nia nzuri.
"SRC haikushurutishwa kuchapisha taarifa hiyo katika gazeti rasmi la serikali. Lakini tuliamua kufanya hivyo kwa njia njema na ili wananchi waweze kupata habari hiyo.'' aliongeza Bi Serem
Tume hiyo hata hivyo iliwapongeza Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kwa kusisitiza kuwa serikali ipunguze matumizi ya pesa za uma.
Bi Serem alisema kuwa hatua hiyo ilichukuliwa na wawili hao ili kutenga pesa kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Onyo la tume limekuja siku moja baada ya wabunge kupiga kura kupinga tangazo la tume hiyo kwenye gazeti rasmi la serikali kuhusu kiwango cha pesa watakachopokea wabunge.
Tangazo hilo lilisema kuwa kila mbunge atapokea shilingi laki tano za Kenya ambazo ni dola elfu sita. Wabunge hao wanapigania kulipwa dola elfu kumi na kuwafanya kuwa miongoni mwa wabunge wanaopokea kiasi kikubwa sana cha mishahara duniani
Post a Comment