Kama
ni lazima kuamini kwamba Zitto na wenzake ni wasaliti, je Marehemu
Chacha Wangwe alikuwa ni msaliti pia kwa kudai yale yale wanayoyadai
wakina Zitto sasa?
WARAKA WA CHACHA WANGWE.
UTANGULIZI
Jumamosi, June 28 mwaka huu wajumbe kadhaa wa Kamati Kuu ya CHADEMA walidai kuwa wamesitisha
Umakau Mwenyekiti wangu katika kikao kilichofanyika mjini Dodoma siku
hiyo. Kesho yake Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Mhe. FREEMAN MBOWE
akaitisha mkutano wa waandishi wa habari na kutaja sababu za
kunisimamisha uongozi.
Inatosha tu kusema kuwa sababu zote alizotoa
ni za uzushi kama ile inayodai kuwa mimi navujisha siri za chama kwa
viongozi wa CCM bila hata kutaja siri hizo, au kusema nimezitoa lini,
wapi, na kwa kiongozi yupi?Kikao hicho kinachosemekana kunisimamisha
uongozi, kilikuwa na wajumbe 31 ambao takribani nusu hawakuwa na uhalali
wa kupiga kura kinyume cha katiba na kanuni za CHADEMA kwa vile
walikuwa wameandaliwa kwa kazi hiyo. Wajumbe 7 walikataa kushiriki njama
hizo.
Kufuatia jaribio hilo la kunivua uongozi kutokubalika kwa
wanachama walio wengi wa CHADEMA , Mwenyekiti MBOWE na wafuasi wake
wameendelea kuhaha kwa kuongeza sababu nyingine mbalimbali ili
kuhalalisha njama zao. Sasa hivi wameingia hatua ya kuwashawishi
wanachama wa Tarime eti wanifukuze uanachama.Kwa kuzingatia katiba,
kanuni na taratibu za CHADEMA, nilichokifanya mimi baada ya kubaini
njama zao ni kukata rufaa kwa Baraza Kuu la Chama, kupinga upotoshaji
unaofanywa chini ya uongozi wa Mhe. MBOWE anayeonekana kutaka kuendesha
chama kinyume na matarajio ya wanachama walio wengi.Hivyo basi zipo
habari za uhakika kuwa kikao hicho cha Baraza Kuu hakitaitishwa ama
kabisa, au kitacheleweshwa kwa makusudi, kwa visingizio mbalimbali
ikiwemo kutokuwa na fedha za kukidhi gharama za kikao hicho.
Naomba
nikiri kuwa ninakerwa sana na mtiririko mzima wa sakata hili linalozua
mgogoro unaokiyumbisha chama. Ukweli ni kwamba mimi niligombea Umakamu
Mwenyekiti nikiwa na agenda ya kufufua uhai wa chama kwa kukaripia
vitendo visivyostahili katika kuendesha chama. Agenda yangu
haijabadilika. Yote niliyoyasema wakati nagombea nafasi hii yanafahamika
kwa wana CHADEMA wote.
Walikuwepo walioyalalamikia na walikuwepo
walioyapongeza matamshi yangu hayo.Mwisho wa yote wana CHADEMA
waliridhika kuwa ajenda yangu ilikuwa sahihi na hivyo wakanichagua kuwa
Makamu Mwenyekiti. Hivyo basi hata kama ni kweli kuwa ulikuwepo mvutano
wakati wa kampeni ile, lakini hilo ni jambo la kawaida katika uchaguzi.
Nijuavyo mimi hayo yalitakiwa yawe si ndwele nasi tugange yajayo kwani
wanachama walikwisha fanya uamuzi halali kupitia kura zao.
Baada ya
kuingia kwenye wadhifa wa Makamu Mwenyekiti Taifa, nilifanikiwa
kuzungumza na Mhe. MBOWE kuhusu mambo, hususan yale, niliyoyapigania
wakati wa kinyang?anyiro kile na kumuomba tukae chini na kutafuta jinsi
ya kufanikisha azma hiyo.Ni imani yangu kuwa waraka huu utawasaidia
wanaCHADEMA wenzangu na watanzania wote kwa ujumla, kuelewa vizuri
ukweli wa mambo niliyoyapigania kabla ya kuwa Makamu Mwenyekiti, na
ninayoendelea kuyasimamia hivi sasa nikiwa Makamu Mwenyekiti, na
inshallah nitakayoyatekeleza baadae kama Taifa Mwenyekiti wa CHADEMA.
Kimsingi mambo tunayotofautiana na Mhe. MBOWE ni haya yafuatayo:-
MATUMIZI YA RUZUKU
CHADEMA hupata ruzuku ya Tshs. 66,000,000 kwa mwezi (Milioni sitini na
sita). Mimi nasema si haba hasa tukizingatia chama kilikotoka. Naamini
kuwa kiasi hiki cha fedha kikisimamiwa vizuri kinaweza kukirahisishia
chama kujieneza katika ngazi zote toka Tawi, Wilaya, Mkoa na Taifa.
Si kweli kwamba matatizo yote yatamalizwa na fedha hizi lakini basi
hata ofisi za chama zinaweza kuwa hai nchi nzima kitu ambacho kwa sasa
hakipo. Mahesabu yanaonesha kuwa mtaji wa laki moja (Tshs.100,000/=) kwa
wilaya moja nchini inatosha, hivyo kwa Wilaya 126 kwa mwezi jumla yake
ni Tshs. milioni 12 (Tshs. 12,600,000/= ) zinahitajika ( Wilaya 126 x
100,000 kila wilaya = 12,000,000/=)Hata tukisema tupeleke kiasi hicho
kwa kila jimbo la uchaguzi jumla yake ni Tshs. Milioni 23 (Tshs.
23,000,000/=) kwa maana ya majimbo 213 x 100,000 = 23,000,000/=.
Mhe. MBOWE anasema hizo ni pesa nyingi sana kwa uimarishaji wa chama.
Mimi nasema hapana, kiwango hiki kwa kila Wilaya au Jimbo la uchaguzi ni
muafaka kwani haba na haba hujaza kibaba.Chini ya uongozi wa Mhe. MBOWE
na wafuasi wake hawastaajabu kuwa kati ya Tshs. 374,144,000.40
zilizopatikana kama ruzuku katika ya Januari 1 na Juni, 30, 2008, Tshs.
350,000,000/= zilitumika Makao Makuu ya CHADEMA na Tshs. 25,000,000/= tu
ndizo zilikwenda Wilayani kuimarisha chama.Mimi naona mgao huu
unayatukuza Makao Makuu ya
CHADEMA isivyostahili wakati huo huo ukidhalilisha chama nchi nzima.
MADENI YA UCHAGUZI
Kufuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, Mhe. MBOWE alitufahamisha
wanachama kuwa alikuwa anakidai chama US $ 181,949.00 sawa na Tshs.
218,338,546. Mpaka sasa chama kimekwisha mlipa Tshs. 175,000,000/=Baada
ya kupata wadhifa wa Makamu Mwenyekiti, na kwa kuzingatia takwimu
zionekanazo hapo juu katika kulinganisha matumizi ya fedha Wilayani na
Makao Makuu niliamua kumshauri MBOWE asitishe kujilipa deni kutokana na
fedha za ruzuku kwani siamini kuwa kulipa madeni yaliyopita kunaendana
na utaratibu wa usimamizi wa fedha za ruzuku kwa vyama vya siasa toka
serikalini.
Mhe. MBOWE alichachamaa na ndipo nilipomshauri kuwa
kama ni hivyo basi atuthibishie pesa hizo anazodai alikikopesha chama
ziliingia kwenye akaunti gani ya CHADEMA, kupitia hundi ipi, na lini?
Nilimuomba pia kutaja ni kikao gani cha chama kiliidhinisha matumizi ya
fedha hizo kwani kama hakuna ushahidi wa maidhinisho, ni dhahiri kuwa
matumizi hayo hayakudhibitiwa na chama na kwa mantiki hiyo kuyafanya
kuwa matumizi binafsi ya Mhe. MBOWE.Vilevile, nilimueleza kuwa matumizi
ya fedha hizo alizodai alikikopesha chama yalikuwa yakinuka harufu ya
UFISADI.
Stakabadhi zote kuhusiana na matumizi hayo zilionesha
kuwa gharama za aidha ununuzi na / au ukodishaji wa vifaa hivyo,
hazikutofautiana na viwango wanavyolipishwa watalii kwa huduma kama
hizo, kwa maana ya gharama ya juu sana.Na kwa kuwa hata baada ya kuwa
Mhe. MBOWE amekwisha lipwa zaidi ya nusu ya deni alilodai kuikopehsa
CHADEMA, vifaa vyote yakiwemo magari, vipaza sauti na kadhalika
vimebakia kuwa mali yake binafsi, basi bila kumficha nilimueleza kuwa
huko ni kukinyonya chama kwa kukigeuza kitega uchumi cha watu
binafsi.Kuhusu suala la kulipa madeni kupitia ruzuku ya serikali,
nilimuomba Mhe. MBOWE afuatilie kwa Msajili wa Vyama vya siasa ili
tupate ufafanuzi kama kweli fedha za ruzuku ya serikali kwa vyama vya
siasa, inaweza kutumika kulipia madeni ya viongozi wa vyama hivyo
yatokanayo na uchaguzi ili CHADEMA isiathirike kisheria.
Niseme
kweli hapa kwamba, kwa vile wanaCHADEMA wengi walinichagua kuwa Makamu
Mwenyekiti, na hata mimi mwenyewe tulikuwa wagombea wa nafasi za ubunge,
udiwani n.k katika uchaguzi wa mwaka 2005 ningefarijika sana iwapo na
sisi tungerejeshewa angalau chochote cha kufidia gharama zetu, kwa maana
kwamba kama chama kimeamua kurudisha gharama hizo kiwalipe wote badala
ya kulipa madeni kwa wateule wachache.
UTEUZI WA WABUNGE WA VITI MAALUM
Naamini ukweli wa suala hili hauna mjadala. Kwamba Mhe. MBOWE na
wafuasi wake walighushi orodha ya majina ya viti Maalum badala ya
kupeleka yaliyopendekezwa na Kamati Kuu sio siri.
Naamini hata Mhe.
MBOWE anakubaliana nami kuwa suala hili si moja ya siri anazodai
nimevujisha! Yamesemwa mengi juu ya mtafaruku uliojitokeza kuhusu viti
maalum hadi baadhi ya waasisi wa chama wakataka kujitoa na hivyo
kumlazimisha Mwenyekiti Taifa ( FREEMN MBOWE) na Katibu Mkuu (DR
WILBROAD SLAA) kukiomba radhi kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kwa
kukiuka katiba, kanuni na maadili ya chama katika suala hili la kugushi
viti maalum.
Ni ukweli ulio wazi kuwa kitendo hicho cha upendeleo
bado kina iumiza taswira ya CHADEMA. Chama kinaonekana kuendekeza ujanja
ujanja kiasi kwamba watu na binti zao, wakwe zao, shemeji zao, waume
wenzao, wachumba wa shemeji zao, wake wenza na kwa kiwango kikubwa watu
wa kabila moja ndiyo wamekuwa sura ya CHADEMA bungeni.Katika hili
nilichoweza kumueleza Mhe. MBOWE ni kuwa chaguzi mbalimbali tangu za
Mitaa, Ubunge na Urais zinakaribia ni vizuri tufanye bidii kusambaza
nguvu zetu nchi nzima tuwe na mtaji wa kura maeneo mengi ili kashfa kama
hii isijirudie. Hii ni kwa msingi kuwa chama kikijitanua kutakuwa
hakuna sababu ya kuwaona watu wa eneo fulani tu kuwa ndiyo mhimili wa
CHADEMA na hivyo zikitokea fursa itakuwa rahisi chama kuwakilishwa na
mtandao wake mpana badala ya koo au kabila fulani.Sasa kwa kuwa
kuimarisha chama kitaifa maana yake ni matumizi ya fedha, nalo hili
likawa nongwa ingawa kwa mtazamo wa Makao Makuu kulipa madeni kwa
wateule wachache si nongwa.
Cha ajabu ni kwamba Mhe. MBOWE
hakukana kuwa hili la viti maalum na hata upangaji wa ajira kwa ukabila
una leta athari mbaya kwa mustakabali wa CHADEMA.Katika maongezi yangu
nae nilikuwa wazi nilipotahadharisha kuwa:
1. Watanzania
wakiendelea kuona kwamba CHADEMA inaendeshwa kwa misingi ya kikabila
hawatajiunga na chama chetu na tutakosa wafuasi.
2. Watanzania
wakiona kuwa sisi tumeweka mbele ukabila kuliko utaifa hawatatupa
madaraka na kutawala kwa kuhofia yale yanayotokea nchi jirani kama
Rwanda, Burundi, Kenya na kadhalika ambako nafasi za raia wote
zimehodhiwa na kabila moja na hatma yake watu wamechinjana kama kuku kwa
kupinga hilo.
Pia nilimwambia kwamba, kwa jinsi sura ya uteuzi wa
Wakurugenzi na watendaji wengine wa Makao Makuu inavyoonekana, sasa
tayari chama chetu kimebatizwa jina la CHAMA CHA WACHAGA, na hii si
kuwatendea haki raia wengine na makabila yao ambao wataonekana kama
punguani kujihusisha na chama na ukabila.Yote haya ninayosema kuhusu
ukabila, upendeleo na kadhalika sio dhana tu. Kufuatia malalamiko mengi
yaliyokuwa yakisikika nchi nzima kuhusu masuala haya, Kamati Kuu ya
CHADEMA ilikwisha unda Tume kutafuta ukweli wa mambo hayo. Tume hiyo ya
watu watano iliongozwa na Mhe. Merky Lugendo Mziray ambaye ni mjumbe wa
Kamati Kuu ya CHADEMA nayo imekwisha toa taarifa yake kwamba Makao Makuu
ya CHADEMA yanatawaliwa na ubaguzi wa kikabila, kidini na kielimu.
UTENDAJI WA KIBABE
CHADEMA ni chama kilicho njia panda kwa sasa kutokana na utendaji wa
kibabe wa Mhe. MBOWE. Ninafahamu jinsi vyama vingine vya upinzani hapa
nchini kama vile NCCR ? Mageuzi vilivyoporomoka haraka haraka mithili ya
nyumba ya mabua. Chama NCCR ? Mageuzi kilifikia mahali pazuri tu hadi
watu wakaanza kufikiria kuwa kingekuwa chama mbadala kwa CCM.
kwa
bahati mbaya uchu wa madaraka, ulafi wa ruzuku, na tabia za kimangimeza
kwa pamoja vikakiathiri hadi kupoteza umaarufu wake.Na hata vyama
vingine vya upinzani vina dalili hizo hizo japo kwa viwango
vinavyotofautiana. Ila badala ya kujichunguza na kujua kasoro zetu, kila
siku vyama vyetu, vimekuwa vikidai kuwa ni chama tawala ndicho
kinachoviroga, kama ambavyo Mhe. MBOWE ameanza kuweweseka kupitia vyombo
vya habari.Napenda kuthibitisha kuwa katika mgogoro unaopaliliwa sasa
na Mhe. MBOWE ndani ya CHADEMA kutokana na ufisadi, ufuska, ulevi wa
madaraka na umangimeza chanzo chake ni tabia yake ya kuendesha chama
kibabe. Mathalan kumzuia Martin Mung?ong?o Mkurugenzi aliyechaguliwa kwa
kura kutofanya kazi zake ndani ya chama, madai ya kupigana na watendaji
wa chama ndani ya baa na vitendo vingine vya aina hiyo ni ushahidi
tosha wa hulka hii.
Hadi sasa Mhe. MBOWE amefanikiwa kukizuia
chama hiki kisifanye kazi ya siasa mkoa wa Dar es salaam kwa miaka
minne.Ninavyoongea hivi sasa CHADEMA imekuwa ikikimbia vikao vya
Democratic Union of Afrika (DUA), Muungano wa Vyama Vya Upinzani,
uliofanikisha CHADEMA kujuana na Conservative Party ya Uingereza na
Republican ya Marekani. Vyama dada hivi vyote vinaulalamikia uongozi wa
CHADEMA kwa kufuja fedha ya misaada na kuwasilisha kwao risiti za
kugushi, kama ilivyofanyiwa Conservative Party baada ya kutoa msaada wa
Tshs. 78,000,000 kwa ajili ya ununuzi wa baiskeli na pikipiki ambazo
hazikununuliwa.Katika mkutano wa Kamati Kuu ya CHADEMA huko Dodoma hivi
majuzi tu, Mhe. MBOWE kwa kauli yake aliwatisha wajumbe kuwa alikuwa
amethibiti uwezekano wowote wa wajumbe kujisikia huru kwa kutoa mawazo
ambayo yangepingana na ajenda yake aliyoitoa ghafla kikaoni
kunisimamisha Umakamu Mwenyekiti.
Mhe. MBOWE Alikifahamisha kikao
kuwa alitoa taarifa kwa IGP, SAID MWEMA kuwa kuna wahuni ambao walitaka
kuuchafua mkutano wake, naye IGP akahakikisha kuwa mkutano ule unalindwa
kwa kiwango cha kushtua kama ambavyo hata vyombo vya habari
vimethibitisha.Hayo ni baadhi tu ya mambo yanayobainisha Mhe. MBOWE ni
kiongozi wa aina gani.
HITIMISHO
Kama nilivyokwisha sema
hapo awali, sijaacha na sintoacha ajenda yangu ya kufufua uhai wa
CHADEMA kwani ndiyo ahadi iliyofanikisha kuchaguliwa kwangu kuwa Makamu
Mwenyekiti Taifa. Nilipopata wadhifa huo nilianza kuitekeleza ajenda
hiyo kupitia mahojiano na Mwenyekiti MBOWE kuhusu matumizi ya ruzuku,
madeni ya uchaguzi, uteuzi wa wabunge wa viti maalum, nafasi za ajira
Makao Makuu, na kuhusu mwenendo wa chama Mkoa wa Dar es salaam.
Nilijikuta katika mvutano mkubwa kila nilipogusa eneo lolote katika
haya. Nakiri kuwa kwa kiwango kikubwa sikuwa na uwezo wa kubadili mambo
hayo yaliyokuwa yakiratibiwa kwa ukaribu na Mhe. MBOWE na wafuasi wake
kwani sikupewa ushirikiano wa aina yoyote na chama pale Makao Makuu.
Ni vigumu kuamini, lakini ni kweli kuwa sikuwa na ofisi Makao Makuu,
sikupewa vitendea kazi kama magari, vipaza sauti na/au vyombo vya
habari, na sikuwahi kupata taarifa yoyote ya kiutendaji toka Makao
Makuu.Kwa kuzingatia yote hayo, naomba nichukue fursa hii kuwashukuru
kwa dhati wanachama wa CHADEMA mkoa wa Dar es salaam ambao kwa pamoja
tulisimama kidete kufufua uhai wa chama hapa jijini. Niseme tu
ushirikiano wao wa hali na mali uliniwezesha kushughulikia masuala
muhimu ya kitaifa na kimataifa.
Rai yangu kwa wana CHADEMA na wale
wote wanaokitakia mema chama chetu na nchi yetu kwa ujumla ni kwamba
kazi ya kupigania demokrasia ya kweli ndani na nje ya chama, kukiepusha
chama na vitendo vya ukabila, migogoro, ubadhirifu, umangimeza, ufisadi
na ubaguzi wa aina yoyote bado inaendelea na nawaombeni mniunge mkono
kwa hali na mali katika vita hii. Naamini tutashinda.Mungu Ibariki
CHADEMA Mungu Ibariki TANZANIA Mungu Ibariki AFRIKA
Post a Comment