Sudan na Sudan Kusini zimetia saini makubaliano kuhusu biashara, mafuta na usalama ingawa hazijakubaliana kuhusu mipaka.
Baada ya mazungumzo ya siku ya nne, nchi hizo mbili zimeafikiana kuruhusu usafirishaji wa mafuta kutoka kusini kupitia mabomba ya Kaskazini na kuondoa wanajeshi mpakani.
Lakin maswala kadhaa muhimu yangali kutatuliwa ikiwemo kuafikia makubaliano kuhusu mipaka inayozozaniwa ikiwa ni mojawpao ya kilichosababisha mgogoro ambao nusura utumbukize nchi hizo kwenye vita mapema mwaka huu.
Baada ya mapigano kuzuka kuhusu mzozo wa mafuta na mipaka, Umoja wa mataifa ulitishia kuziwekea pande zote mbili vikwazo ikiwa hazitaafikia makubaliano ya kina.
Wapatanishi wa Muungano wa Afrika wangali kuthibitisha kuwa makubaliano yameafikiwa lakini rais wa Sudan Omar al-Bashir na mwenzake wa Kusini Salva Kiir, wanatarajiwa kutia saini makubaliano hayo hii leo.
Maelezo yametolewa tu kwa mukhtasari lakini wapatanishi wa pande zote mbili, walisema kuwa wamekubaliana kuhusu eneo la nchi hizo mbili ambalo halina ulinzi wa kijeshi.
Pia makubaliano ya kiuchumi yaliafikiwa kuruhusu Sudan Kusini kuanza tena shughuli zake za kuzalisha mafuta.
Lakini mwafaka haukupatikana kuhusu eneo linalozozaniwa la Abyei wala mipaka mingine mingi ambayo nchi hizo zinazozania.
Kwa hivyo makubalino hayo hayajaweza kutimiza masharti ya Umoja wa Mataifa kwa nchi hizo kuafikia mkataba unaotatua mzozo huo kwa kina.
Post a Comment