Home » » Uhuru ataka kesi ICC ianze upya

Uhuru ataka kesi ICC ianze upya

Written By peterdafi.blogspot.com on Monday, March 18, 2013 | 11:51 AM



Uhuru Kenyatta mahakamani ICC
Wanasheria wa rais mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta, wameiomba Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, ICC, kumfutia mashitaka yanayomkabili mbele ya mahakama hiyo.
Bwana Kenyatta amekanusha kuchochea ghasia baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Kikao maalum cha mahakama hiyo kimefanyika wiki moja baada ya mashitaka dhidi ya mtuhumiwa mwenzake, Francis Muthaura, kutupiliwa mbali.
Mawakili wa Kenyatta wanasema kuachiwa kwa Muthaura, pia kunafuta mashitaka dhidi ya Kenyatta, lakini mwendesha mashitaka wa ICC amesema ana ushahidi zaidi dhidi ya Uhuru Kenyatta.
Kesi dhidi ya Bwana Kenyatta, ambaye alishinda uchaguzi mkuu uliofanyika mapema mwezi huu, na kutangazwa rais mteule baada ya kupata asilimia kidogo juu ya 50%, imepangwa kuanza kusikilizwa mwezi Julai.
Baada ya matokeo ya uchaguzi wa Desemba mwaka 2007 - wakati Bwana Raila Odinga aliposhindwa dhidi ya Rais wa sasa Mwai Kibaki, zaidi ya watu 1,000 waliuawa na wengine 600,000 kuachwa bila makaazi.
Bwana Kenyatta, mtoto wa mwasisi wa taifa la Kenya, Jomo Kenyatta anatuhumiwa kupanga mashambulio dhidi ya makundi ya kikabila yaliyokuwa yakimuunga mkono Bwana Odinga kufuatia uchaguzi wa mwaka 2007.

Shahidi muhimu 'haaminiki'

Zaidi ya Wakenya 1,000 waliuawa baada ya uchaguzi wa mwaka 2007. Wiki iliyopita, mwendesha mashitaka wa ICC, Fatou Bensouda alisema kesi dhidi ya Bwana Muthaura imetupiliwa mbali kufuatia baadhi ya mashahidi kuogopa kutoa ushahidi wao, huku mwingien akikana sehemu ya ushahidi wake na kukiri kupokea rushwa.
Shahidi muhimu - akijulikana kama shahidi namba nne - alikuwepo katika mkutano ambako BwanaMuthaura na Bwana Kenyatta walituhumiwa kupanga kuwatumia kikundi cha Mungiki kinachoogopewa nchini humo kuwashambulia Wakalenjin, ambao walionekana kuwa wafuasi wa Bwana Odinga katika uchaguzi wa mwaka 2007.
Kiongozi wa mawakili wa Bwana Kenyatta, Stephen Kay anesema kwa kuwa shahidi namba nne ndiye aliyemhusisha Kenyatta na kikundi cha Mungiki, kwa hiyo kujitoa kwake katika ushahidi kuna maana kwamba Kenyatta hana kesi ya kujibu.
Uhuru Kenyatta ashinda Urais Kenya
"kwa kiasi fulani tumepoteza imani katika utoaji maamuzi kama tulivyotahadharisha kikao cha kwanza cha mahakama cha kuthibitisha mashitaka, kutokana na aina ya ushahidi uliokuwa ukitolewa , na tukapuuzwa," Bwana Kay tameiambia mahakama ya ICC, ripoti kutoka shirika la AFP.
"Ushahidi dhidi ya Bwana Muthaura ambao umelazimisha kuondolewa kwa mashitaka dhidi ya Kenyatta ni sawa sawa na Bwana Kenyatta," amesema.
Amewaomba majaji kurejesha kesi ya Bwana Kenyatta kwenye mahakama ya kuthibitisha kesi ili majaji waweze kupitia ushahidi uliobakia kabla ya kuanza kesi kusikilizwa na kuamua kama kuna ushahidi kamili unaothibitisha kesi hiyo kusikilizwa.
Mwandishi wa BBC Anna Holligan kutoka The Hague anasema baada ya kufutwa kwa kesi dhidi ya mtuhumiwa mwenzake, Francis Muthaura, kumekuwa na uvumi kwamba mashitaka dhidi ya Bwana Kenyatta huenda pia ikatupiliwa mbali.

Chanzo ni BBC
Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. peterdafi - All Rights Reserved
Template Created by Eddie Sucre Published by Bongoclanblog
Proudly powered by Blogger