Bagamoyo. Mwigizaji wa filamu na mtangazaji wa kipindi cha redio cha Paradise, Irene Uwoya, amesema licha ya kwamba wasanii wanafanya bidii kuyafikia mafanikio, kikwazo kikubwa katika safari yao ni kutokuthamini muda.
Akizungumza katika mafunzo maalumu ya wasanii na
wafanyakazi wa Kampuni ya uzalishaji na usambazaji wa filamu 5 Effect,
Uwoya alisema kinachokwamisha tasnia ya filamu kufika katika nafasi za
juu kimafanikio ni kutokujali muda.
“Tatizo kubwa ni kutokuthamini muda, unakuta
mmekubaliana kwamba mkutane saa nane mchana katika eneo la kutengenezea
filamu (Location), unafika pale mtu unayetakiwa kushirikiana naye katika
(Scene) kile kipande hajafika, anafika saa kumi jioni, kazi inachelewa
kuanza na muda unapotea,” alisema Uwoya.
Alisisitiza kwamba ikiwa tasnia hiyo itajali muda
ipasavyo, inaweza kupiga hatua kubwa kwa mwaka huu, hasa ukizingatia
sanaa imerasimishwa na Serikali hivyo ni kazi inayotambulika kwa sasa.
“Serikali yetu imerasimisha sanaa, kwa sasa ni
kazi kama ya ofisini, inatakiwa sisi wasanii tulitambue hili na kila
mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha anatekeleza majukumu yake ipasavyo.Pia
mtu wa kamera naye lazima ajue script (muswada) inasema nini.
Vivyo hivyo kwa upande wa masoko na wasambazaji
tunahitaji watu wenye uelewa na elimu kuhusu kazi hizi ili tusonge
mbele,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa viongozi ni kama dira, hivyo
wanapaswa kutoa mwongozo mzuri kwa wasanii na kusimamia kampuni vema ili
kujikwamua na wizi wa kazi za sanaa nchini.
“Lazima tuondoe dhana kuwa bila watu wa jamii ya Asia hakuna usambazaji,” anasema.
Post a Comment