Home » , » UKWELI WA KUVAMIWA NA KUKAMATWA KWA DK. HAMISI KIGWANGALLA JIMBONI NZEGA.

UKWELI WA KUVAMIWA NA KUKAMATWA KWA DK. HAMISI KIGWANGALLA JIMBONI NZEGA.

Written By peterdafi.blogspot.com on Tuesday, March 25, 2014 | 9:46 AM





RASLIMALI, MADARAKA, MIPAKA DHULUMA NA UTAWALA BORA

Naomba nichukue fursa hii adhimu ili kuweza kuandika japo kwa ufupi mambo mengi yanayotokea katika nchi hii, hasa katika ukiukaji wa haki za binadamu ama kwa sababu ya upofu na umbumbumbu wa sheria wa baadhi ya watawala wetu, Rushwa miongoni mwa watawala, uzembe wa viongozi na watawala wetu, chuki na visasi miongoni mwa watawala na masuala mengine kama haya. Nipate kuweka bayana ya baadhi ya mambo yaliyofichika hasa katika maeneo muhimu yenye neema kwa taifa ambako, raslimali za taifa zimekuwa zikiondolewa mikononi mwa wanaNchi na kuwekwa mikononi mwa madhulumati wachache.
Ardhi ni ralimali muhimu kwa ustawi wa taifa. Ardhi yenye rutuba ni bora kwa shughuli za kilimo, ardhi yenye madini ni maeneo muhimu ya uwekezaji, na ardhi iliyoko katika miji, manispaa na majiji ni kwa ajili ya ukuaji na uendelezaji makazi na miji husika. Miongoni mwa kero kubwa zinazolikera taifa hili na hasa linalowakera raia wazalendo wa taifa hili Tanzania ni matumizi ya ardhi yasiyozingatia ustawi wa Mtanzania ambaye ni maskini na badala yake kuzingatia kuwagawia ardhi yote wawekezaji. Uwekezaji umekuwa ndio mgongo na mbeleko kubebea wizi, unyang'anyi, rushwa, ufisadi, dhuluma, mauaji ya raia wasiokuwa na hatia. Mauaji mengi yamekuwa yakitekelezwa ama moja kwa moja, ama kwa jinsi ambavyo, "wawekezaji" hawawezi kudhibitiwa ili kuzuia sumu kutoka katika viwanda vyao yasiingie katika mifumo ya maisha ya watanzania. Tumeshuhudia tafiti mbalimbali zikitangaza kuwa dhana ya uwepo ama wa sumu ama uhatarishaji wa maisha ya wananchi kutokana na mabaki ya uchafu wa viwanda si hatari kwa maisha ya wananchi. Tumeyashuhudia haya katika migodi ya madini hasa dhahabu huko Geita, Kahama, Bulyanhulu, Buzwagi na katika viwanda mbalimbali huko Dar es Salaam na miji mingine kuliko na viwanda.
Waswahili tuna Msemo "Kila Mjenga Nchi ni Mwananchi na Kila Mbomoa Nchi ni Mwananchi". Maana halisi ya usemi huu ni kuwa, wananchi ndio kila kitu kwa ama ustawi ama ufu wa taifa lolote lile duniani na kwamba nguvu ya wananchi kwa wingi au uchache wao ni muhimu katika kusimamia raslimali zilizopo jinsi zinavyotumika, sababu ya kutumika na mipangilio ya uendelevu wake. 

Nimeshika kalamu kuandika makala haya kwa sababu kuu moja, kuhoji uhalali wa jeshi la polisi nchini kupiga, kufunga na kutesa raia na viongozi wao kwa kisingizio cha uvunjifu wa amani huku wao ndio wanavunja hiyo amani kwa sababu zinazoweza kuelezeka kiurahisi zaidi ukiziita rushwa. Mahali pengi Tanzania tumeshuhudia viongozi wa watu (Wabunge) walio katika mstari wa mbele kutetea haki za raia waliowachagua wakiteswa, kuwekwa kwenye rumande za polisi, kufunguliwa mashtaka na mbaya zaidi hata kudhalilishwa utu wao. Haya yanatokea sana hasa pale kunapokuwa hakuna maelewano kati ya wawekezaji na viongozi wa wananchi.

Leo Tanzania tupo katika kipindi muhimu sana cha ustawi wa taifa letu. Ni kipindi ambacho ama tutaamua mustakabali chanya wa taifa letu, ama ufu wa taifa letu. Tupo katika mchakato wa kutengeneza katiba mpya, katiba ambayo itakidhi mahitaji ya Tanzania kwa sasa. katiba ambayo itatambua raslimali za taifa na kuainisha kwa uwazi bila kificho kwamba raslimali zitatumika kwa ajilia ya manufaa na maendeleo ya Tanzania na Watanzania. Katika mambo tunayotakiwa kuyaweka sawa ni umiliki, umilikishaji na umilikishwaji wa ardhi yenye madini kwa wananchi (hasa wachimbaji wadogo) na uzuiaji ardhi hii kuchukuliwa na serikali kwa namna ambayo italeta manung'uniko na hata kufikia hatua ya kuhatarisha amani ya nchi. Kutafsiri ardhi iliyopo kwa matumizi ya wakulima na matumizi ya wafanyakazi na kutambua maeneo mahsusi kwa kazi hizi. Mauaji tuliyokwisha kushuhudia, ambayo yametokana na mapigano ya wakulima na wafugaji, yalitokana sana na sababu ya kutotambua maeneo muhimu wa ajili ya shughuli za wakulima na wafugaji.

Tanzania ya sasa tunashuhudia nguvu kubwa wanayotumia polisi wetu katika matumizi ya silaha dhidi ya raia wao eti kwa kigezo kuwa raia wamewazidi nguvu. Matumizi ya mabomu ya machozi, risasi za moto na aina ya vifaa vinavyotumika kudhibiti wananchi wasio na chupa za maji tu ni kubwa kuashiria weledi katika jeshi la polisi haupo tena ama kama upo basi kwa "Maelekezo maalum" unatumika isivyopaswa. Haya yametokea sehemu mbalimbali mfano huko Iringa, Mbeya, Mwanza, Mtwara na hivi juzi huko Nzega Tabora ambako Mbunge wajimbo hilo Mh. Hamisi Kigwangala (HK) alitupwa rumande wakati akiwa kwenye utekelezaji wa majukumu yake ya kawaida.

Katika tukio la Nzega, kuna mambo yaliyojitokeza ambayo hayaelezeki ama maana yake kabisa ama taathira na mwelekeo wa maana yake. Mbunge alitoa taarifa kupitia mtandao wa jamii "facebook" kuwa....... amenusurika kuuawa....... na kwamba yule aliyetaka kutekeleza hayo mauaji ndiyo aliyemwambia ...... lakini kilichomponya HK ni, shabaha ndogo ya Mlenga shabaha (huyo) polisi ambapo risasi iliyomkosa Kigwangala ilimpata raia (kijana) katika paji la uso. 
Mheshimiwa Mbunge aliandika "Nimenusurika kuuawa muda mfupi, askari kwenye gari ananiambia, bahati yako nilikulenga kichwa....." Sasa hii aliwataarifu nyie Ndugu zangu lakini mimi nilikuwepo Nae eneo la tukio hii ni hatari sana Jamani.
Mkuu wa Wilaya hakuwepo wilayani na kwamba hata alipotafutwa alijibu  
"Nipo nje ya wilaya na OCD hajanipa taarifa yoyote nasubiri nipewe taarifa". 
Hapa ndipo penye tatizo,
1.   Je OCD kumkamata Mbunge alitekeleza agizo la nani, ama katika kutimiza wajibu wake alishauriana na na nani;
2.   Mbunge alikuwa katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazohusu majukumu yake ya kibunge jimboni kwake. Na kwamba jambo alilokuwa anashughulikia ni mgogoro wa uchimbaji madini uliopo katika wilaya ya Nzega, je Mkuu wa Wilaya hakuwa na taarifa na hilo hadi aliposikia Mbunge amekamatwa?
3.   Kinga ya Mbunge inaishia wapi hasa anapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yake?
4. Kwanini umkamate Mbunge kwa Kumdhalilisha kama vile na tena bila kuwasiliana na katibu au Mwenyekiti wa Bunge?
5. Lakini pia kwanini umkamate na Mwandishi wa Habari kwa kuwepo tu eneo la tukio?
6. Kwanini baadhi ya waandishi walifukuzwa kutishiwa na kusukumwa pia kutusiwa na askari?
7. Kwanini Askari,,,! Askari anamtukana Mbunge kwa matusi makubwa makubwa na kumsukumizia Lumande, kwa jeuli ipi hasa?
8. Je..!! Ni sawa na usemi usemao mti wenye matunda ndo hupigwa mawe! HK amefanya mengi jimboni tena yale ya misimamo na kusaidia wanyonge hii manake Mkoa na Wilaya ya Nzega Viongizi wao Baadhi si waadilifu na wanakiuka Taratibu za Ufanyaji kazi wa Umma? 

Nimeamua kuweka mfano wa tukio la Tabora kama rejea angalau kwa ufupi maana mimi ni mhanga wa tukio nzima na nililiona lilivyotokea mwanzo hadi mwisho. Taaluma yangu ya uandishi wa habari ilinipeleka katika mikutano ya mheshimiwa Mbunge, lakini pia kwa kuwa mimi ni mkazi wa Nzega, nililazimika kwenda katika mikutano hii. Kwa nafasi yangu ya uandishi mimi ni mwandishi na mmiliki wa blogspot inayoitwa peterdafi.blogspot.com. na uvccmtz.blogspot.com. Lakini pia Baada ya Mheshimiwa Mbunge kukamatwa, ilinilazimu kulifuatilia hilo tukio kwa ukaribu hivyo nililazimika kwenda hadi kituo kikuu cha Polisi Nzega. Nilipofika tu, nikakamatwa na kuwekwa chini ya Ulinzi eti nilionekana na Mbunge wakati wa Mikutano. Maelezo kwamba mimi ni mwandishi wa habari hayakusaidia bali walidai kitambulisho wakati hata aliyekwa ananidai kitambulisho hakunionyesha kitambulisho. Ushahidi wa kutaka kuifungua blogspot yangu ili waithibitishe walikataa, hapo nikajua lengo lilikuwa kuniweka ndani. 

Nilitoka na Mh. Kigwangalla Dodoma siku ya jumamosi 22/03/2014 saa 14:45 PM tukajaza mafuta Gari yake na safari ilianza saa 15:15 PM, Kuelekea Nzega kupitia Igunga ambako Mama yake Dk, Hamisi Kigwangalla alikuwa amelazwa kwa Kupasuliwa KIDOLE TUMBO, Mama aliugua Gafla na kulazwa Hospitali ya Igunga, Ikiwa Mwanae alikuwa Nje ya Nchi kwa Shuguli zake, alikatisha ziara na kurudi Tanzania kwa Kero za WanaNzega kufukuzwa katika Mashimo yao ya kuchimbia dhahabu. Basi tulifika Hospitali ya Wilaya Igunga Saa Mbili za Usiku na Kumuona Mama kalazwa akiwa anaendelea Vyema tu na Matibabu, tulimjulia hali na kisha, Tuliondoka na Kufika Nzega usiku wa saa 22:30 kisha nikachukua Chumba katika Hotel Moja na kwenda kupata Chakula Grand Villa hapo, nilimnukuu jamaa mmoja aliekuwa akizungumza habari za Kuvuruga Mkutano wa Kigwangalla wa Kesho yake Nzega ndogo na kisha uko Mwanshina Hapo HK alikuwa Nyumbani kwake nimemuacha na nilikuwa na Dereva wake ambae alisikia habari za kuharibu kikao cha kesho yake nilimjuza HK yote hayo na Kisha kunukuu kuwa Jamaa alikua akiongea habari za kuvuruga mkutano na kisha alipokea Simu ya Bashe na kuzungumza nae kifichoni. Kesho yake tulienda Nzega ndogo tukafanya mkutano wananchi wakatoa malalamiko ya kunyanyaswa kwao na viongozi, Hapo nilishuhudia Hisia za zawatanzania wakilia kwa kunyanyaswa na kupokonywa mali zao, inauma sana kuona Mtu mzima akilia kwa uchungu, Mbunge aliomba askali tuongozane naokuelekea Sehemu Migodi ilipofukiwa kwa ajili ya kumalizia Mkutano wake wa Pili hapo, Askali walitangulia na kwenda nao wakiwa wanatulinda kwani watu walikuwa wakitembea kwa makundi makundi tu na kubadilishana mawazo hapo Mbunge nae alisema "ntatembea na wananchi wangu kwani wao wanatembea na mimi ntatembea pia" Tulienda na kukalibia sehemu ya tukio tulishangaa kukuta askali wamejipanga wakiwa na Masiraha mazito mazito na gafla tulianza kushambuliwa bila kupewa wala kutangaziwa Onyo la aina yeyote ile, Tulipigwa Risasi za moto na Mabomu na Muheshimiwa alikamatwa kama Jambazi na kudhalilishwa kisha kusukumwa katika Gari la Police na kupelekwa Kituo kikuu cha Polisi Nzega Mjini.

Nirudi kwenye mada ya msingi. Inatokea hivi, hapa na pale katika Jamhuri kwamba wananchi wanaonewa, serikali ipo na hakuna kuheshimiana miongoni mwa viongozi wa serikali, Je hii inatokana na nini?
Inakuwaje kiongozi wa kuteuliwa na asiyewajibika kwa wanannchi anaowaongoza ashindwe kumheshimu kiongozi wa kuteuliwa mbele ya raia wake bali tu amdhalilishe kuwa yeye si lolote si chochote? Ama;...

Je...!! busara ya kukaa mezani na kuzungumza viongozi imetowekea wapi hasa wale wateule kukaa meza moja na wenye ridhaa ya wananchi? Ama;
Ni nani aliyewaambia, kwa kuwa Wakuu wa Vituo vya Polisi na Wakuu wa Polisi Wilaya na Mikoa ni Wateule wa Mteule wa Rais (kwa taathira), na kwa kuwa Rais wa Jamhuri ana Madaraka makubwa, na kwa kuwa kwa mujibu wa Katiba Rais hawezi kushtakiwa mahakamani akiwa madarakani, basi na wao wana nguvu hiyo na wana kinga hiyo? ama...... 

Ni nani aliyewadanganya kwamba, kwa kuwa wamepewa Mabomu, Pingu na Risasi, basi ni lazima vyote vitumike kwa sababu yoyote? Na alafu,
Ni nani kawaambia kila tukio basi matumizi ya risasi ni muhimu?
Ifike mahali itoshe na ionekane inatosha maana chuki ni kubwa miongoni mwa viongozi na wapo wanaojiona kwa vile wao mamlaka yao ya uteuzi ni rais wa jamhuri, basi na wao ni Marais wa Jamhuri kwa zile nafasi walizoteuliwa kuzishika. Huu ni Wendawazimu na Ujuha ambao unalitafuna taifa. Taifa hili kwa uchanga wake kiuchumi linahitaji mshikamano wa hali ya juu kati ya viongozi wa ngazi zote, kuheshimiana na kuwajibika sawa moja kwa moja kwa wananchi na si kukaa na kuendekeza ubabe usio na tija.

Tunahitaji wananchi waone kwamba viongozi wao wanaheshimiana wao kwa wao kwanza, wanawaheshimu wananchi wanaowaongoza na wanafanya kazi pasipo makinzano. Rushwa ina tabia ya upofushaji, na ikiwaingia watawala itawapofusha kabisa. Mapambano kati ya watawala na viongozi yataishia katika watawala kupokea rushwa kwa wafitini wa uchumi wa wananchi na kisha watawala kutumia nguvu zao zote kinyume na ubinadamu dhidi ya viongozi na mwisho wa siku kutaibuka machafuko ambayo hatuwezi kuyatuliza kwa kauli za kitoto. Mapigano ya wakulima na wafugaji hayaishi, wachimbaji wadogo na wawekezaji hayaishi, dhuluma ya ardhi haikomi, hili linatokana na watawala kujiona wao ni wakuu wa viongozi maana nafasi zao hazitegemei miaka baada ya uchaguzi bali ni kazi na taaluma za kudumu.
Naa haya ni mawazo ya Kijinga.

Peter Dafi
peterdafi.blogspot.com



Share this article :

Post a Comment

 
Copyright © 2011. peterdafi - All Rights Reserved
Template Created by Eddie Sucre Published by Bongoclanblog
Proudly powered by Blogger