Mrembo aliyewahi kushika taji la Miss Tanzania ,Faraja Kotta Nyalandu akiwa na msanii wa muziki wa Bongo Fleva Ambwene Yesaya "AY"katika viwanja vya hosptali ya wilaya ya Hai. |
Mrembo aliyewahi kushika taji la Miss Tanzania ,Faraja Kotta Nyalandu akiwa na msanii wa muziki wa Bongo Fleva Ambwene Yesaya "AY" wakati wa kutangazwa kuwa mabalozi wa UNICEF. |
Mwakilishi wa Unicef Tanzania Dk Jamal Gulaid akimkabidhi barua msanii wa muziki wa Bongo Fleva Ambwene Yesaya "AY" ya kuwa balozi wa UNICEF katika kampeni ya Tokomeza Ukatili dhidi ya watoto. |
Mabalozi
wa UNICEF ,Faraja Kotta Nyalandu na Ambwene Yesaya "AY wakijadiliana
jambo muda mfupi baada ya kutangazwa kuwa mabalozi wa UNICEF katika
kampeni ya Tokomeza Ukatili dhidi ya watoto. |
Mrembo aliyewahi kushika taji la Miss Tanzania ,Faraja Kotta Nyalandu akizungumza mara baada ya kuteuliwa balozi wa UNICEF katika kampeni ya Tokomeza Ukatili dhidi ya watoto. |
Msanii wa Muziki wa Bongo fleva Ambwene Yesaya ."AY" akizungumza mara baada ya kuteuliwa balozi wa UNICEF katika kampeni ya Tokomeza Ukatili dhidi ya watoto. |
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hai,Clement Kwayu akiteta jambo na Mrembo aliyewahi kushika taji la Miss Tanzania ,Fraja Kotta Nyalandu muda mfupi baada ya kutangazwa balozi wa UNICEF. |
Msanii Oscar Peter maarufu kama Oscer Nyerere akitoa burudani kwa wananchi wa wilaya ya Hai(hawako pichani)wakati wa sherehe ya kutangazwa kwa mabalozi wa UNICEF. |
Mrembo aliyewahi kushika taji la Miss Tanzania ,Fraja Kotta Nyalandu akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa kupambana na ukatili wa wanawake na watoto. |
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Hai,Clement Kwayu akimzungumzia Mrembo aliyewahi kushika taji la Miss Tanzania ,Fraja Kotta Nyalandu kuhusu kitabu chake alichozindua hivi karibuni. |
Katika kusherehekea
siku ya Mtoto wa Afrika tarehe 16 Juni, Halmashauri ya Wilaya ya Hai,
ikishirikiana na viongozi wa serikali, UNICEF na Save the Children,
imezindua Kituo cha Huduma Jumuishi, kitakachowasaidia wanawake na
watoto ambao wameathiriwa na ukatili.
“Katika kituo hiki,
huduma za kuwasaidia wahanga wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya
watoto ikiwa ni pamoja na huduma za afya, msaada wa kisaikolojia,
ulinzi/usalama na msaada wa kisheria vinaweza kutolewa hapo katika eneo
moja ndani ya kituo cha afya zikiwa zimeratibiwa vizuri Zaidi,” alisema
Charles Pallangyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Aliongeza, “kituo
hiki kitasaidia kupunguza madhara zaidi ya ukatili kwa sababu wahanga wa
ukatili wataweza kupata huduma zote muhimu katika eneo moja na
hawatakuwa na sababu ya kurudiarudia kuwaeleza watoa huduma mbalimbali
walio katika maeneo tofauti yale mambo mabaya waliyoyapitia, au kutakiwa
kwenda na kurudi kutokana na ukosefu wa uratibu na uwezo wa watendaji
wa sekta mbalimbali katika kuwahudumia wahanga wa ukatili kwa
ukamilifu.”
Mwakilishi wa UNICEF
Tanzania, Dk. Jama Gulaid, anaamini kuwa kama tukifanya kazi kwa
ushirikiano na serikali na wadau wengine, tunaweza kupata suluhu katika
kumaliza ukatili dhidi ya watoto. “Ukatili dhidi ya watoto uko kila
mahali na hatuwezi kuendelea kuufumbia macho. Watoto wote hapa Tanzania
wanahaki ya kuishi na kukua katika mazingira yasiyo na ukatili. Kama
sisi sote tukifanya kazi kwa kushirikiana pamoja, sina shaka tutaweza
kumaliza ukatili dhidi ya watoto.”
Katika tukio hili
huko Hai, UNICEF Tanzania imemteua msanii mahiri wa bongo flava Ambwene
Yessyah, anayejulikana zaidi kama AY, pamoja na aliyewahi kuwa Miss
Tanzania, Faraja Kotta Nyalandu kama Mabalozi wao katika ‘Kampeni ya
Tokomeza Ukatili Dhidi ya Watoto.’ Wote wameahidi kusaidia
kampeni ya ‘Kampeni ya Tokomeza Ukatili Dhidi ya Watoto’ na wameonyesha
kuhamasishwa na heshima hii waliyopewa kutoa sauti zao kutetea ulinzi wa
mtoto.
“Nimepewa heshima
kubwa kwa kuteuliwa kwangu kuwa Balozi wa UNICEF Tanzania na nitajitoa
katika kutumia sauti yangu na umaarufu wangu kusaidia kutokomeza ukatili
dhidi ya watoto hapa Tanzania,” alisema AY alipokuwa akikubali wadhifa
huo.
Kwa kuwateua AY na
Faraja Kotta Nyalandu kama Mabalozi wa UNICEF Tanzania wa kampeni ya
‘Kampeni ya Tokomeza Ukatili Dhidi ya Watoto’, UNICEF inategemea
kuongeza uzito na muonekano zaidi wa suala la ulinzi wa mtoto katika
mijadala inayoendelea kuhusu ukatili dhidi ya watoto na kuonyesha kuwa
kuna suluhisho la tatizo hili.
Kama mwazo wa kazi
yao katika shughuli za UNICEF Tanzania, AY na Faraja Kotta Nyalandu
walitembelea Dawati la Jinsia na Watoto katika kituo cha Polisi cha Hai
kuona wenyewe kazi inayofanywa kusaidia wanawake na watoto waliofanyiwa
au kuathiriwa na ukatili.
Utafiti juu ya
Ukatili Dhidi ya Watoto, uliozinduliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii,
Jinsia na Watoto mwaka 2011, unaonyesha mambo yanayopelekea uhatarishi
wa watoto kwenye ukatili kimwili na kingono hapa Tanzania – wastani wa
msichana 1 kati ya 3 na mvulana 1 kati ya 7 wamefanyiwa vitendo vya
ukatili wa kingono, na zaidi ya asilimia 70 ya wasichana na wavulana
wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kimwili kabla hawajafikia umri wa
miaka 18. Hata hivyo, wahanga wengi hawajamwambia mtu yeyote ukatili
waliofanyiwa na ni kesi chache sana zimefikishwa polisi.
Kumekuwa na maendeleo
katika kuboresha hali hii. UNICEF inasaidia serikali ya Tanzania
kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii kuanzisha na kuboresha ‘mifumo ya
Ulinzi wa Mtoto’ katika halmashauri 13.
Katika halmashauri
hizi, afya, ustawi wa jamii, polisi, sekta za elimu na mahakama,
magereza, wanasheria, asasi za kiraia pamoja na mifumo ya kijamii isiyo
rasmi wanaunda Timu ya Halmashauri ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto na
wanashirikiana kuhakikisha kuwa kesi za ukatili wa watoto
zinashughulikiwa vyema na pia wanazuia ukatili kwa kuongeza uelewa wa
jamii juu ya ukatili dhidi ya watoto.
Lengo la Idara ya Ustawi wa Jamii ni kupanua utaratibu wa mfumo huu katika halmashauri 30 ifikapo mwaka 2016.
Na Dixon Busagaga wa globu ya jamii kanda ya kaskazini
Post a Comment